27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

MPINA ATANGAZA MAPAMBANO UVUVI HARAMU

NA JOSEPH LINO -DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, ametangaza vita mpya kukomesha uvuvi haramu kwa wote wanaotumia baruti, sumu na nyavu haramu.

Kauli hiyo aliitoa jijini Dar es Salaam jana katika ufunguzi wa mkutano wa 10 wa Chama cha Wanasayansi wa Ukanda wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi (WIOMSA), ambapo alisema uvuvi haramu umekuwa changamoto kubwa kwa sasa.

“Haiwezekani uvuvi haramu ukaendelea wakati watendaji wa Serikali wapo, licha ya kukamatwa kila siku, bado watu hawa wapo utadhani hatuna sheria za kutosha kuwashughulikia watu husika,” alisema Mpina.

Alisema kwa sasa Serikali inahamasisha wavuvi wadogo katika ufugaji wa samaki badala ya kwenda ziwani au baharini.

“Katika mpango huu tutausimamia ipasavyo ikiwamo suala zima la kupata mikopo kwa ajili ya ufugaji wa samaki ambapo uzalishaji wake ni mkubwa na faida kwa uwingi,” alisema.

Akizungumzia mkutano huo, alisema wanasayansi ambao ni wadau wa Bahari ya Hindi wanahakikisha utunzaji wa rasilimali ya bahari ili viumbe vyote viendelee kuishi kwa kizazi kilichopo na kijacho.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Maandalizi ya mkutano huo, Profesa Yunus Mgaya, alisema changamoto kubwa kwa upande wa bahari ya Tanzania ni joto linaloongezeka kutokana na shughuli za binadamu na rasilimali ya uvuvi.

Alisema usimamizi wa uvuaji samaki katika bahari yetu unaruhusu kila mwenye leseni kwenda kuvua ambao huleta ushindani wa kutoweka kwa samaki.

Hata hivyo, Mgaya alisema kuna fursa kubwa katika uvuaji wa samaki kwenye maeneo ya maji yenye kina kirefu ambako samaki wanakuwa wengi na wakubwa kuliko maeneo ya Pwani.

Mkutano wa siku tano unawakutanisha wadau zaidi ya 500 kutoka nchi 10 kama Kenya, Tanzania, Afrika Kusini, Msumbiji, Somalia, Madagascar, Mauritius, Comoro, Shelisheli na Reunion (Ufaransa).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles