28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

MOYO KUKAA UPANDE WA KULIA SI TATIZO KIAFYA

Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM



KATI ya Novemba 25 hadi Desemba mosi, 2017 Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), ilifanya upasuaji mkubwa wa moyo wa kihistoria nchini.
Madaktari Bingwa wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa Taasisi ya Open Heart International kutoka nchini Austraria waliwafanyia upasuaji wagonjwa 16 wenye matatizo mbalimbali ya moyo.
Kati ya wagonjwa hao, tisa walikuwa watoto na saba watu wazima, ambao walifanyiwa upasuaji wa kubadilisha milango ya moyo iliyokuwa imeharibika na kuwekewa milango ya chuma.
Miongoni mwa watu wazima waliofanyiwa upasuaji wapo waliopandikizwa mishipa ya damu iliyovunwa kutoka miguuni na kwenda kuzibua ile iliyokuwa imeziba.
“Upasuaji huo kitaalamu unaitwa ‘bi-pass surger,’ hii si mara ya kwanza kwa taasisi yetu kufanya kwani tayari wagonjwa wapatao 30 wamefanyiwa kwa mwaka huu pekee,” anasema Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi.
Anasema: “Watoto waliofanyiwa upasuaji walikuwa na umri wa kuanzia miezi minne wakiwa na uzito wa kuanzia kilo nne hadi 12, kati yao, mmoja alikuwa amezaliwa akiwa na moyo upande wa kulia.”
Profesa Janabi anasema kibaiolojia moyo wa binadamu unapaswa kuwa upande wa kushoto hata hivyo, hutokea mara chache mtoto kuzaliwa moyo ukiwa upande wa kulia.
Anasema hadi sasa bado haijajulikana wazi nini hasa husababisha mtoto kuzaliwa moyo ukiwa upande wa kulia.
“Duniani, tafiti zinaonesha kati ya watoto 2000 wanaozaliwa basi mmoja huwa katika uwezekano wa kuzaliwa moyo wake ukiwa upande wa kulia,” anasema.
Anasema hata hivyo hakuna madhara yoyote yanayoweza kumpata mtoto ambaye moyo wake umeumbwa ukiwa upande wa kulia.
“Anaweza kuishi vema kabisa kama binadamu wengine ambao wameumbwa wakiwa na moyo katika upande wa kushoto,” anabainisha.

Mtoto aliyefanyiwa upasuaji
Profesa Janabi anasema mtoto ambaye walilazimika kumfanyia upasuaji alikuwa na matatizo makubwa mawili ya moyo.
“Moyo kuumbwa upande wa kulia haikuwa tatizo kubwa kwake, isipokuwa tulibaini mishipa yake ya damu ilikuwa haifanyi kazi inavyopaswa.
“Katika moyo kuna mishipa inayoingia upande wa kulia ambayo kazi yake kuu ni kubeba damu chafu yenye hewa ya kabondaioksaidi na kuna inayoingia upande wa kushoto yenyewe hubeba damu safi yenye oksijeni,” anabainisha.
Anaongeza: “Huyu mishipa yake ilikuwa inachanganya damu safi na chafu kwa pamoja jambo ambalo lilikuwa ni hatari kwa maisha yake.
“Ni kama vile uchukue maji safi na taka halafu uyachanganye kwa pamoja kisha unywe, kamwe mwili hauwezi kuhimili mchanganyiko huo.
“Sasa yeye badala ya damu chafu kupita katika upande unaostahili ili ikasafishwe huchanganyika pamoja na damu safi iliyokwisha safishwa kisha iende mwilini kutumika, ni tatizo,” anasema.
Anasema pamoja na tatizo hilo, tatizo jingine lilikuwa ni mapigo yake ya moyo yalikuwa chini mno kutokana na kiwango kidogo cha umeme kilichopo kwenye moyo wake.
“Kutokana na hali hiyo, ilibidi tumpandikize betri ndani ya moyo wake, hii ni oparesheni ya tatu kwa watoto na sasa mapigo yake yanakwenda vema,” anasema.
Anasema ilichukua takriban saa tisa kukamilisha upasuaji huo kwa sababu kwa kesi kubwa kama hiyo huwalazimu ‘kuusimamisha’ moyo wake kwa saa kadhaa.

Mwili kuwa na rangi ya bluu
Anasema damu safi na chafu inapochanganyika ni lazima mwili wa mgonjwa ubadilike rangi na kuwa bluu.
“Kitendo cha kubadilika na kuwa rangi ya bluu maana yake ni kwamba kile kiwango cha oksjeni kinachohitajika mwilini huwa hakitoshelezi,” anabainisha.

Dalili zake
Anataja dalili za awali kwa mtoto aliyezaliwa na tatizo la moyo ambazo mzazi anaweza kuziona ni pamoja na kushindwa kunyonya vizuri.
Anasema hii huwatokea zaidi watoto walio katika umri wa kunyonya, lakini kwa wenye umri wa kwenda shule wengi huchoka mara kwa mara.

Makuzi baada ya upasuaji
Anasema mtoto waliyemfanyia upasuaji ataendeelea vizuri na kwamba ataishi na kulelewa kama ilivyo kwa watoto wengine wasio na tatizo.
“Kila mshipa wa damu sasa unafanya kazi yake kama inavyotakiwa na mfumo wa umeme upo sawa sawa baada ya kumpandikiza betri.
“Lakini kama asingetibiwa mapema basi kidaktari naweza kusema wazi kwamba asingefika na kusherehekea sikukuu yake ya kuzaliwa ya mwaka mmoja.
“Ila kwa kuwa tumewahi kumfanyia upasuaji tunaamini Mungu akimjalia basi atasherehekea sikukuu yake ya mwaka wa kwanza na kuendelea,” anasema.

Masharti
Anasema mtoto huyo ambaye ni mchanga, ataishi na kula kila kitu isipokuwa amepewa masharti kadhaa.
“Tumempatia kadi maalumu ya utambuzi, hatatakiwa kupita katika maeneo yenye sumaku kubwa kama vile uwanja wa ndege kwa sababu ile nguvu inaweza kukiwasha na kuyafanya mapigo ya moyo kubadilika na kwenda kasi,” anasema.

Ushirikiano zaidi
Mkufunzi wa Wagonjwa Mahututi na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa OHI, Russel Lee anasema wataendelea kushirikiana kwa ukaribu na JKIC katika kutoa matibabu.
“Kila ninapokuja Tanzania naona JKCI inazidi kufanya matibabu kwa kiwango cha juu zaidi ya awali, hili ni jambo linalotia faraja kubwa, OHI tutaendelea kushirikiana nao pia kwa kuwapatia mafunzo wataalamu wake ili wazidi kufanya vizuri zaidi,” anasema.
Daktari Bingwa wa Upasuaji Magonjwa ya Moyo kwa Watoto wa JKCI, Godwin Sharau anasema faida kubwa wanayopata katika kambi hizo za matibabu ni kubadilishana ujuzi.
“Kuna baadhi ya magonjwa ya moyo ambayo ni magumu na JKCI tunahitaji kupanda hatua kwa hatua ili tuweze kuwahudumia vizuri watoto na wakubwa wenye matatizo haya.
“Tunataka twende sambamba na wenzetu katika teknolojia ya kutibu magonjwa ya moyo ili kufikia adhma ya serikali kupunguza idadi ya wagonjwa wanaoenda kutibiwa nje ya nchi,” anasema.

Wito
Anawasihi wazazi wanapoona dalili hizo wawahi kuwapeleka watoto wao hospitalini kwa uchunguzi zaidi.
“Ukimpeleka hospitalini watabaini tatizo na kama anastahili kuletwa JKCI watampa rufaa kuja huku, kuendelea kukaa naye nyumbani kutahatarisha zaidi maisha yake hatimaye kifo.
Anasema katika kipindi cha mwaka huu pekee wamewafanyia upasuaji watoto 300 wenye matatizo ya moyo, ukijumlisha na watu wazima idadi yao inazidi 600.
“Watoto waliopoteza maisha ni wanne tu, hivyo wasiogope kuja kuwafanyia uchunguzi na upasuaji watoto wao,” anawasihi.
Profesa Janabi anawahimiza pia wataalamu wa afya kuhakikisha wanawapa rufaa mapema kwenda JKCI watoto wanaowapokea wakiwa na dalili za maradhi makubwa ya moyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles