24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

MOTO WATEKETEZA BWENI SHULE YA UFUNDI MTWARA

bweni

NA FLORENCE SANAWA, MTWARA

MOTO ambao chanzo chake bado hakijabainika umeteketeza bweni la Shule ya Ufundi Mtwara, lenye vyumba 32, vitanda 232 na magodoro 193.

Akizungumzia tukio hilo jana, Mkuu wa Shule hiyo, Paul Kaji, alisema asilimia 75 ya bweni hilo la wanafunzi wa kike limeteketea, vikiwemo vifaa vya walimu waliokuwepo shuleni hapo kwa kazi maalumu ya usahihishaji wa mitihani ya Taifa ya Kidato cha Pili.

Alisema moto huo umeteketeza vitanda vya mbao 192, vitanda vya chuma 40 na magodoro 193 katika bweni hilo.

Kaji alisema alipata taarifa za kuungua kwa bweni hilo jana asubuhi na alipofika eneo la tukio alibaini kuwa, vyumba vinne vilikuwa vimeshika moto kwa kasi, hivyo haikuwezekana kuokoa chochote.

“Tutakapofungua shule hatutakuwa na sehemu ya kuwalaza wanafunzi wetu, tumepata pigo kubwa. Pia tumepoteza vitu vingi ambavyo vilikuwa vya walimu waliokuwa wakilala humo na wanafunzi walioko likizo. Hilo jengo tulijengewa kwa msaada wa Serikali ya Japan mwaka 2007, tukalikabidhi kwa wanafunzi wa kike ambao ndio waliokuwa wakilitumia kabla ya kwenda likizo ya mwisho wa mwaka huu. Hatujui chanzo cha moto, tunasubiri mamlaka husika zifanye uchunguzi kisha zitujuze,” alisema Kaji.

Kwa upande wake, Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto mkoani hapa, Elizabeth Mpondele, alisema baada ya kupata taarifa na kufika eneo la tukio walikuta moto ukiwaka kwa kasi kubwa.

Elizabeth alisema gari hilo lilizidiwa na hivyo kulazimu Jeshi la Polisi kutoa gari jingine lililoongeza nguvu na kufanikiwa kuuzima moto.

Alisema kutokana na moto kuwa mkali, walishindwa kuokoa mali zilizokuwamo ndani.

Pia aliitaka jamii kujifunza namna ya kutumia vifaa vya uokoaji pamoja na kuzingatia matumizi ya muda wake, ili moto unapotokea usisababishe madhara makubwa.

Naye Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Khatibu Kazungu, alisema kuungua kwa mabweni hayo ni janga kwa mkoa huo na hasa wanafunzi wa kike ambao vyumba vyao vimetekea vibaya kwa moto huo.

“Tukio limetusikitisha siyo tu kama viongozi, bali kama wazazi, hawa wanafunzi waliokwenda likizo wakirudi watakuwa wamepoteza baadhi ya vifaa vyao, hawatakuwa na uwezo wa kuvipata, hasa ukizingatia kuwa huu ni mwisho wa mwaka. Ndani hapakuwa na mtu hata mmoja, hivyo inaonekana ni hitilafu ya umeme,” alisema Kazungu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles