27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Morsi ahukumiwa kifungo cha maisha

Mohamed Morsi, president of EgyptCAIRO, MISRI

MAHAKAMA nchini Misri imemhukumu kifungo cha maisha jela Rais wa zamani wa nchi hiyo, Mohamed Morsi huku washitakiwa wenzake sita wakihukumiwa kifo.

Wakili wake Abdel Moneim Abdel Maksoud ameliambia Shirika la Habari la Ufaransa (AFP) kwamba mahakama hiyo ya Cairo imemfutia Morsi mashtaka ya kuipatia Qatar nyaraka za siri lakini imemhukumu kwa kuliongoza kundi lililopigwa marufuku.

Qatar ilikuwa muungaji mkono mkuu wa Morsi na kundi lake la Udugu wa Kiislamu wakati kiongozi huyo alipokuwa madarakani mwaka 2012 hadi Julai 2013 alipopinduliwa na jeshi kabla ya kukamatwa.

Morsi alikuwa amehukumiwa kifo katika kesi tafauti kutokana kinachodaiwa ushiriki wake kutorosha wafungwa kutoka gerezani na mashambulizi dhidi ya vituo vya polisi wakati wa uasi wa mwaka 2011 uliomwondoa madarakani kiongozi aliyetawala kwa muda mrefu nchini humo Hosni Mubarak.

Pia aliwahi kuhukumiwa kifungo cha maisha na kifungo cha miaka 20 jela katika kesi nyingine mbili tofauti.
Mahakama hiyo pia imethibitisha hukumu za kifo dhidi ya washtakiwa wengine sita wakiwemo wanahabari wawili waliokuwa wakishtakiwa bila ya wenyewe kuwepo mahakamani kwa madai ya kusaidia kuziwasilisha nyaraka hizo za siri kwa Qatar.

Waandishi hao wametambuliwa kuwa Ibrahim Mohamed Hilal na raia Jordan Alaa Omar ambao wote wawili ni waajiriwa wa Kituo cha Televisheni cha Al Jazeera chenye makao yake nchini Qatar.

Mwandishi wa tatu ni mwanamke anayetambulika kwa jina la Asmaa Mohamed al-Khatib wa kijarida cha Raasd kinachomilikiwa na kundi la Udugu wa Kiislamu.

Washtakiwa wengine watatu waliohukumiwa kifo ni mtayarishaji wa filamu simulizi, Ahmed Afifiy, mfanyakazi wa ndani ya ndege wa Shirika la Ndege la Misri Mohammed Keilany na mwanazuoni Ahmed Ismail.

Jaji Mohamed Shirin Fahmy amekuwa akipendekeza hukumu hiyo ya kifo kwa kipindi cha cha miezi sita sasa.
Kwa mujibu wa taratibu za Misri hukumu hizo za kifo zinatumwa kwa Mufti Mkuu wa nchi hiyo ili kuidhinishwa lakini si lazima maoni yake yatekelezwe.

Fahmy ameikariri ofisi ya mufti ikisema washtakiwa hao sita walikuwa wakitaka kuiletea nchi madhara wakati walipotoa kwa taifa la kigeni taarifa kuhusu walipo wanajeshi wa Misri na ripoti zilizotayarishwa na mashirika ya ujasusi ya nchi hii.

Uhusiano wa Misri na Qatar umekuwa mchungu tangu kupinduliwa kwa Morsi ambaye alikuwa akiungwa mkono na taifa hilo dogo lakini tajiri la Ghuba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles