27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

MOI WAPONGEZWA KWA HUDUMA BORA


NA VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

BODI ya Wadhamini ya Taasisi ya Mifupa, Upasuaji wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu (MOI), imewapongeza wafanyakazi wa taasisi hiyo kwa kazi kubwa wanayofanya ya kuwahudumia Watanzania waliopata matatizo mbalimbali, hasa kutokana na magonjwa ya ajali.

Pongezi hizo zilitolewa mwishoni mwa wiki na Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Zakia Meghji, alipozungumza na wafanyakazi na viongozi waandamizi wa taasisi hiyo wakati alipokuwa akitoa salamu za kuuaga mwaka 2017 na kuukaribisha mwaka 2018.

Alisema anatambua kazi kubwa na ngumu wanayofanya madaktari, wauguzi na wafanyakazi wa vitengo mbalimbali kuokoa maisha ya Watanzania wanaofikishwa katika taasisi hiyo.

“Natambua kazi kubwa inayofanyika hapa usiku na mchana ili kukabiliana na ongezeko la wagonjwa wanaotokana na ongezeko la ajali hapa nchini,” alisema.

Aliongeza: “Sisi kama bodi tunatambua kazi kubwa na nzito mnayofanya, kwa waliopo nje ya MOI si rahisi kutambua hilo. Nawapongezeni sana, na niwatie moyo kwamba tutashirikiana ili kupambana na changamoto zinazojitokeza.”

Alisema ana imani kwamba kazi kubwa zilizofanyika mwaka 2017 zitaendelea na kuboreshwa zaidi katika mwaka 2018 ili kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora hapa hapa nchini.

Aliishukuru Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli kwa kurahisisha upatikanaji wa vifaa, vifaa tiba na kuweka mazingira rafiki kwa wagonjwa na watoa huduma.

“Sasa hivi hakuna msongamano wodini au wagonjwa kulala chini kwa kukosa vitanda,” alisema.

Naye, Makamu Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Profesa Bakari Lembariti, aliwapongeza wafanyakazi hao kwa kuendelea kutimiza dira ya MOI kuwa kituo cha weledi Afrika na kuendeleza ubunifu katika utoaji huduma ambazo hazifanyiki katika nchi nyingi za Kiafrika.

“Hatua hiyo imeifanya MOI kuwa kituo cha weledi Afrika katika tiba ya mifupa, upasuaji wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu, mnastahili pongezi,” alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa MOI, Dk. Respicious Boniface, aliihakikishia bodi hiyo kwamba katika mwaka 2018 watafanya kazi kwa weledi na bidii kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora kwa wakati mwafaka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles