23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Mo asimulia watekaji walivyotaka kumuua

ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM

MWAKA mmoja sasa tangu mfanyabiashara maarufu nchini, Mohamed Dewji ‘Mo’ alipotekwa na watu wasiojulikana, hatimaye amezungumzia kwa mara ya kwanza namna alivyokuwa mikononi mwa watekaji kwa siku tisa.

Mo anayetajwa na jarida maarufu duniani la Forbes kuwa ndiye anayeshika rekodi ya bilionea kijana Afrika, alitekwa nyara na watu wasiojulikana Oktoba 11, mwaka jana alipokuwa akiingia mazoezini katika Hoteli ya Colosseum iliyoko Oysterbay, Dar es Salaam.

Akizungumza juzi jioni na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kupitia idhaa yake ya Kiswahili, Mo alisema kwa kipindi kizima alihisi kwamba kuna uwezekano mkubwa asingeweza kuwa salama na kwamba mwisho wa maisha yake ulikaribia.

“Siku hiyo nilikuwa nimeenda kwenye mazoezi pale Hoteli ya Colosseum, sasa wakati naingia kulikuwa na gari nyuma yangu ambayo iliingia baada yangu, kwa hiyo nikapaki gari pale Gym. kuna askari wakawa wananielekeza ‘specific parking’ karibu na mlango wa Gym.

“Kwa hiyo ile kufunga mlango tu, kugeuka nimekuta watu wanne ambao wamevaa mask, wakawa wamepiga bunduki juu mara mbili halafu wameniwekea bunduki kichwani huku wananiambia wataniua.

“Zile saa 24 za kwanza baada ya kutekwa zilikuwa kama mwezi, imani ndiyo kilichonisaidia katika kipindi kizima.

“Mwanzoni nikafikiria labda hawa watu wanataka kuchukua gari langu au wanahitaji kitu, basi wakaniambia lala chini, mimi nikalala chini, cha kushangaza kwenye sekunde 60 tu wale watu wamekuja wamenibeba na kuniweka ndani ya gari.

“Sasa baada ya kuniweka ndani ya gari ndio tukaanza hiyo safari. Safari ilikuwa ngumu, baada ya kunifunga wakanivua nguo zote, kama dakika 20 nikaona tayari wamenipeleka ndani ya nyumba, hapo wameshanifunga uso.

“Walikuwa wanaongea lugha yao, haikuwa lugha ya ki-Tanzania kufika pale kwenye ile nyumba wakanipeleka ndani ya chumba, wakanifungua miguu ili niweze kutembea, ilikuwa ni ngumu sana.

“Walinifunga macho kwa siku tisa, walikuwa wananiambia nile, lakini nilikuwa siwezi kula kwa sababu nilikuwa na ‘shock’, asubuhi walikuwa wananifungua mikono, lakini wananifunga kwa mbele.

“Usiku ndio kulikuwa na mtihani zaidi, walikuwa wananifunga mikono nyuma, nikawa siwezi kulala, kwa hiyo lazima nilale kulia au kushoto na kwa kuwa walikuwa wananifunga na kukaza sana, dakika tano najikuta mikono inakufa ganzi,” alisema Mo.

Alisema katika kipindi hicho cha siku tisa, kazi kubwa aliyokuwa anafanya alikuwa akimwomba Mungu ili atoke salama.

Alipoulizwa endapo kama anawahisi waliomteka ni wapinzani wake kibiashara au siasa, Mo alisema; “Nchi yetu ya Tanzania hatujafikia hapo, ndio ushindani wa kibiashara upo, lakini hatujafika huko.”

Akizungumzia kuhusu siku aliporudishwa na kuachwa maeneo ya Gymkhana, alisema; “Tulipofika pale Gymkhana walini-push nikasimama, pale nikasikia gari imeondoka, nikatoa kitambaa usoni, ndio nikagundua pale ni Gymkhana.

“Pale kulikuwa hoteli, wakanipokea, wakampigia simu baba yangu na mdogo wangu ndio walikuja kunichukua, ninashukuru Mungu na pia ninawashukuru Watanzania kwa maombi yao kwa kipindi kile.”

ALIVYOTEKWA

Inaelezwa kuwa siku Mo alivyotekwa, watu waliomteka walifika hotelini hapo wakitumia gari aina ya Toyata Surf na walifyatua risasi mbili hewani kisha wakatokomea naye kusikojulikana.

Kutekwa kwake si tu kulitikisa nchi, bali hata katika mataifa mengine ya ndani na nje ya bara la Afrika.

Katika muda wote wa takribani siku tisa, idadi kubwa ya Watanzania walikuwa katika simanzi nzito, huku wengine wakifanya ibada wakimwombea aachiwe akiwa salama.

Mara tu baada ya kutekwa, Jeshi la Polisi liliwashikilia na kuwahoji watu 27 ambao kati yao wanane walikuwa bado wako chini ya uchunguzi.

Baadaye Oktoba 20, mwaka jana, Mo alirudishwa na watekaji hao katika viwanja vya Gymkhana, Dar es Salaam.

MAZINGIRA YA TUKIO

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, aliibuka kuzungumzia tukio hilo na maswali kadhaa yaliibuka kuhusu utata wa namna tukio hilo lilivyotekelezwa.

Kamanda Mambosasa alisema kuwa maswali hayo yanawasumbua na wanatafuta majibu yake.

Alisema; “Hebu tujiulize kamera (iliyopo katika Hoteli ya Colosseum) nayo imeshindwa kutupatia kila kitu, kuna upande tumeshindwa kuupata vizuri, tunajiuliza ilikwepeshwa makusudi?”

MATAJIRI SITA WALIOTEKWA 2018

Tukio la kutekwa kwa Mo lilitikisa Tanzania, lakini si jipya kwa mwaka jana barani Afrika.

Mo ni tajiri mkubwa wa saba barani Afrika kutekwa tangua mwaka 2018 ulipoanza.

Matukio mengine ya namna hiyo yametokea nchini Afrika Kusini, Msumbiji na Nigeria.

Shiraz Gathoo – Afrika Kusini

Mfanyabiashara huyu maarufu kutoka Afrika Kusini alitekwa Machi 10, mwaka jana, huku watekaji wake walijifanya kuwa ni askari wa usalama barabarani na kuweka kizuizi bandia barabarani na kumteka.

Liyaqat Ali Parker – Afrika Kusini

Julai, mwaka jana, Liyaqat Ali Parker mfanyabiashara kutoka Afrika Kusini, pia alitekwa jijini Capetown akiwa katika majengo ya ofisi yake na watu waliokuwa na bunduki.

Parker, 65, ni mwanzilishi wa Kampuni ya Foodprop Group ambayo humiliki maduka ya jumla ya Foodworld nchini humo. Anamiliki mali nyingine nyingi.

Alitekwa Julai 9, baada ya kufuatiliwa kwa muda na watu watano waliotumia gari aina ya double-cabin.

Alizuiliwa kwa miezi miwili hadi aliporejea nyumbani kwake Septemba 17.

Siku ya kutekwa, wanaume watano wasiojulikana wanadaiwa kulifuata gari lake hadi katika maegesho ya biashara yake, Fairway Close, N1 City chini ya jengo.

Babake John Obi Mikel – Nigeria

Baba wa mchezaji nyota wa Nigeria John Mikel Obi pia alitekwa Juni mwaka jana na watu waliokuwa na silaha eneo la Enugu.

Alikuwa ametekwa Juni 26, lakini akaokolewa na polisi Julai 2 baada ya makabiliano makali kati yao na waliokuwa wanamzuilia.

Andre Hanekom – Msumbiji

Raia wa Afrika Kusini anayefanya biashara nchini Msumbiji, Andre Hanekom, alitekwa katika Jimbo la Cabo Delgado Agosti katika mji wa Palma akiwa kwenye maegesho ya hoteli ya Amarula.

Mfanyabiashara huyo aliyekuwa ameishi Msumbiji kwa miaka 26, anadaiwa kuandamwa na wanaume wanne wasiojulikana na kufyatuliwa risasi mara kadha. Alikimbilia hotelini, lakini akakamatwa na kuingizwa katika gari na kutoroshwa.

Sikhumbozo Mjwara – Afrika Kusini

Sikhumbozo Mjwara, 41, mfanyabiashara kutoka jijini Durban, Afrika Kusini pia alitekwa Agosti na hadi sasa bado hajulikani alipo.

Robert Mugabe wa Uganda

Mmoja wa wafanyabiashara maarufu kutoka Wilaya ya Nakasongola, Robert Mugabe alitekwa nyara Agosti na watu waliokuwa wamevalia mavazi ya Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mugabe, 38, alitekwa alipokuwa anasafirisha samaki kutoka Kasese kwenda Ishasha katika wilaya Kanungu walipokuwa wanapitia mbuga ya taifa ya Malkia Elizabeth.

Aliachiliwa huru siku chache baadaye baada ya familia yake kudaiwa kulipa kikombozi cha pauni za Uingereza 7,500 ingawa awali waliomteka walidai pauni 20,000.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles