27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mnyika matatani

mnyikaaVERONICA ROMWALD Na JONAS MUSHI -DAR ES SALAAM

MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika, amedaiwa kuwaacha njia panda wadhamini  (majina tunayo) ambao walikubali kuidhamini kampuni ya Testa ambayo yeye alikuwa mwenyekiti wa bodi ya wadhamini.

Inadaiwa kwamba Mbunge huyo alichukua uamuzi wa kujiondoa kwenye kampuni hiyo baada ya kuona  inashindwa  kulipa deni la Sh milioni 300 ambalo linatokana na riba ya mkopo wa Sh milioni 222 ambazo   Testa ilikopeshwa na benki ya Standadr Chartered.

Habari za uhakika ambazo MTANZANIA limezipata zinaeleza kuwa kwa miaka mitatu sasa wadhamini hao wamekuwa wakihangaika kutafuta njia ya kujinasua kutoka kwenye deni hilo.

Inaelezwa kuwa nyumba za wadhamini hao ambazo ziliwekwa rehani   kupata mkopo huo zipo kwenye hatihati ya kupigwa mnada  kufidia deni hilo.

Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari, kampuni ya Testa ilikuwa ikijihusisha na uwakala mkubwa wa masuala ya huduma za fedha kupitia simu za mkononi.

Chanzo chetu hicho kilieleza kwamba Mnyika ndiye aliyekuwa mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa kampuni hiyo na ambaye aliridhia kukopwa  kiasi hicho cha fedha katika benki hiyo.

“Mnyika alikuwa mwenyekiti wa bodi ya wadhamini, alikuwa na hisa nyingi kuliko wenzake – ya zaidi ya asilimia 50 – na kwa nafasi hiyo ya uenyekiti saini yake ndiyo ilikuwa inatambulika kule benki ili kuchukua mkopo,” kilieleza chanzo hicho.

Kilieleza pamoja na Mnyika kudaiwa kujiondoa  katika kampuni hiyo siku nyingi hata hivyo hakuwasiliana na wadhamini wake na hata benki hiyo kuwaeleza juu ya uamuzi wake huo.

Nyaraka muhimu ambazo MTANZANIA imeziona zinaonyesha kampuni hiyo ilikubaliwa kukopeshwa fedha hizo baada ya kikao cha bodi   Januari 25, 2012,   Mnyika akiwa mwenyekiti.

“Kikao cha bodi ndicho kilichokuwa na uamuzi juu ya shughuli za kampuni ikiwamo masuala ya kukopa. Januari 25, 2012 wajumbe walikaa na kukubaliana kukopa. Mnyika akiwa mwenyekiti aliidhinisha kwa kutia saini yake Mei 11, 2012 ndipo kampuni ikakopeshwa,” kilieleza.

Nyaraka nyingine kutoka benki hiyo ambazo MTANZANIA imeziona zinaonyesha awali  kampuni hiyo  ilikuwa ikirejesha vizuri deni hilo,  tangu Agosti 31, 2012 hadi   Februari 28, 2014.

Nyaraka hizo zinaoneysha kuanzia Machi 31, 2014  kampuni ilishindwa kurejesha fedha zozote hadi kufikia  Julai 31, mwaka huu ambao ndiyo ulikuwa mwisho wa kurejesha mkopo huo.

Kwa mujibu wa chanzo chetu, wadhamini hao walikuwa wakifuatilia maendeleo ya kampuni hiyo kwa mmoja ya wakurugenzi (jina tunalo) na walikuwa wakijibiwa kuwa kampuni inaendelea vizuri.

“Miezi sita baada ya kuzungumza na Mkurugenzi huyo, benki ilituma wawakilishi wake kwa wadhamini na wakakabidhiwa barua ya kuwajulisha kuwa deni halijalipwa na nyumba zao zitapigwa mnada kulifidia,” kilieleza.

Chanzo hicho kilieleza kuwa kutokana na hali hiyo, mmoja wa wadhamini hao amekwisha kufanya juhudi za kukutana na viongozi wa ngazi za juu wa Chadema, chama ambacho anatokea Mbunge huyo  kutafuta ufumbuzi wa suala hilo.

“Alishawahi kumfuata Dk. Willbrod Slaa (alipokuwa Katibu Mkuu wa Chadema), Freeman Mbowe (mwenyekiti) na hivi karibuni ameenda kuomba kuonana na Edward Lowassa (Mjumbe wa Kamati Kuu) na iwapo hatafanikiwa yeye na mwenzake wamepanga kuchukua hatua nyingine ambazo hawajaziweka wazi,” alisema.

MTANZANIA ilipomtafuta Mnyika kwa   simu kuzungumzia suala hilo    simu yake  iliita bila kupokewa na alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi alijibu baadhi ya maswali kama ifuatavyo;

MTANZANIA: Habari mheshimiwa, naitwa… kuna taarifa kuwa nyumba za wadhamini wako zinapigwa mnada kwa sababu umeshindwa kurejesha mkopo wa zaidi ya Sh milioni 200, nini kauli yako juu ya tuhuma hizi?

Mnyika: Hakuna mtu yeyote aliyeweka nyumba kunidhamini waulize wakuambie ukweli.

MTANZANIA: Kuna nyaraka ambazo tunazo moja ikiwamo ya makubaliano ya bodi ya wakurugenzi ambayo wewe ulisaini ukiwa mwenyekiti na ilionyesha wadhamini sita zikiwamo nyumba mbili zilizopo Bunju na Mmbweni.

Mnyika: Iliyokopa ni kampuni si mimi na niliondoka kwenye hiyo kampuni tangu mwaka 2013 bila kupokea fedha yoyote binafsi… hivyo ni vizuri ukawatafuta wenye hiyo kampuni kuwauliza na waulize pia hao wadhamini walinufaika vipi na hiyo mikopo na nani aliwafuata waweke hati zao.

MTANZANIA: Mheshimiwa wewe ulikuwa nani kwenye hiyo kampuni, wajibu wako ulikuwa upi na uliondoka vipi na nani ni wamiliki wa hiyo kampuni?

Mnyika hakulijibu swali hili na alipoombwa kupigiwa hakujibu.  Vilevile,  alipopigiwa simu yake iliita bila kupokelewa hadi gazeti hili linakwenda mtamboni jana usiku.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles