23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Mnyika kusuka upya mipango Chadema

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAM

KATIBU Mkuu mpya wa Chama cha Demokrasi na Maendeleo (Chadema), John Manyika, amesema kuwa kwa sasa anajiandaa kuingia ofisini ambapo ataweka wazi mikakati yote ya chama hicho kuelekea mwaka 2020.

Kauli hiyo ya Mnyika, imekuja baada ya MTANZANIA Jumapili kumtafuta kutaka ufafanuzi wake kuhusu mikakati yake ikiwamo namna alivyojipanga kama mtendaji mkuu wa chama na matarajio yake kwa siku za usoni.

Desemba 20, 2019,  Mwenyekiti wa Chadema, Mbowe alitangaza kumteua Mnyika kuwa Katibu Mkuu mpya pamoja na manaibu wake wawili na Mjumbe wa Kamati Kuu mmoja.

Kutokana na hali hiyo alisema kuwa kwa sasa bado  hajaripoti ofisini ila amewataka Watanzania hasa wapenda demokrasia kujipanga na Chadema sasa inakuja kuwa mkombozi wao.

“Kwa sasa bado sijaripoti ofisini ila kwa ufupi ninachoweza kukuambia kwa sasa ni kwamba tumejipanga na tuweka wazi mikakati yetu ikiwamo kuzungumza na vyombo vya habari. Chadema ipo vizuri sana kuliko ilivyokuwa juzi na jana,” alisema Mnyika kwa kifupi.

Katika kusuka safu mpya ya uongozi Mbowe pia alikiomba kikao cha Baraza Kuu la chama hicho kuridhia uteuzi wa Salum Mwalimu  kuwa Naibu Katibu Mkuu Zanzibar na aliyekuwa Mkurugenzi wa Oganaizesheni, Mafunzo na Usimamizi wa Kanda wa chama hicho, Benson Kigaila, kuwa Naibu Katibu Mkuu Bara.

Baraza Kuu la Chadema pia lilipokea na kuridhia jina la Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho baada ya kuteuliwa na kutangazwa na Mbowe.

Hata hivyo katika kauli yale aliyoitoa wiki katika Mkutano Mkuu wa sita wa Uchaguzi uliofanyika Mlima City jijini Dar es Salaam, Mnyika alisema kuwa akifikiria miaka 15 ya utumishi ndani ya Chadema na kazi kubwa iliyopo mbele, kama ingekuwa ni mapenzi yake, angeomba kikombe cha uongozi wa juu kimuepuke kwa sasa.

Alisema anafananisha kipindi hiki na simulizi za dini katika Biblia Takatifu, wakati wa mateso ya Yesu, alipokuwa bustanini kule Getsemane ambapo anatamani kuwa baada ya miaka 15 ya kubeba msalaba kama Simon Mkirene, angetamani kikombe hicho kimuepuke.

“Baada ya miaka 15 ya kutafuta ukombozi na mabadiliko katika Taifa letu, Mshimiwa mwenyekiti natamani kama vile kikombe hiki kiniepuke, kila mtu ana matamanio yake lakini kwa imani zote, tunaamini katika katika kila jambo mapenzi ya Mungu yatimizwe,” alisema.

Akisimulia namna alivyojiunga Chadema, Mnyika alisema alianza utumishi kama Mkurugenzi wa Vijana wa chama akiwa na miaka 24, akiwa Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo aliingia kwenye chama baada ya Mbowe, wakati huo Mwenyekiti  wa Vijana chini ya Edwin Mtei, walimualika kwenye kongamano la kujadili sera za vijana na uanzishwaji wa Baraza la Taifa la Vijana wakati huo akiwa kwenye taasisi zingine si za kisiasa zinazohusika na masuala ya vijana.

“Mimi nilikuwa mwanafunzi chuo kikuu lakini nilikuwa kwenye taasisi kadhaa za vijana zisizo za kiserikali, nikaitwa na Mtei wakati huo na ninaamini ilikuwa ni kwa mapendekezo ya Mbowe, kwenda kutoa maoni kwenye kongamano lililoandaliwa na Chadema, kuhusu mapitio ya Sera za Chadema lililofanyika Landmark Hotel, Ubungo.

“Nilikwenda kutoa maoni nikiwa si mwanachama wa Chadema na kati ya maoni niliyoyatoa kwenye kongamano lile ni kwamba ili Chadema iweze kuvutia vijana na akina mama ni vyema (wakati huo haikuwa na mabaraza ya chama kikatiba, hakukuwa na vyombo vya makundi haya mawili) basi kuanzishwe mabaraza ya chama, baraza la vijana na baraza la akina mama.

“Waliokuwepo kwenye kongamano lile walifurahia ule ujumbe lakini Mbowe baadaye aliniambia, wewe umetoa maoni kama mtu asiye mwanachama, sasa maoni haya uliyoyatoa nani atasimamia kuyatekeleza, kwa nini usitoke huko uliko ukajiunga na Chadema ili uongoze utekeleaji wa maoni uliyoyatoa? Kwa hiyo nikajiunga na Chadema na kuchaguliwa kuwa Mkurugenzi wa Vijana,” alisema.

Alisema hapo ndipo ilipoanza safari ndefu ya kisiasa ambapo alikuwa Mkurugenzi wa Vijana, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi na Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na wakati mwingine alitumikia nafasi hizo zote kwa pamoja. 

Alisema mwaka 2014 Mwenyekiti na Katibu Mkuu wakati huo waliona ni vyema apewe jukumu kubwa la kuwa naibu Katibu Mkuu wa chama.

Alisema katika kipindi chake cha utumishi tangu 2004 akiwa Mkurugeni wa Vijana mara nyingi sana alikuwa akikaimu ukatibu mkuu kumsaidia Katibu Mkuu akiwa hayupo.

Alisema wamekuwa wakifanya kazi katika makao makuu ya chama kutekelea maagizo ya Kamati Kuu na ya viongozi wakuu wa chama na kwamba anashukuru ameweza kuendesha makao makuu salama na kufikia hatua hii ilipofikia pamoja na kupitia mashambulizi magumu.

Alisema wameifanya kazi hiyo kwa gharama kubwa kidogo kwa kuwa walijiwekea utaratibu kuwa ukishika nafasi ya utendaji katika makao makuu ya chama kama ni mbunge hupati posho yoyote, hivyo tangu aliposhika ubunge mwaka 2010, amefanya kazi kwa miaka tisa kwa kutumia mshahara wa ubunge pekee.

KAULI YA MSEKWA

Akizungumzia uteuzi wa Mnyika, Makamu Mwenyekiti Mstaafu Pius Msekwa, alipongeza hatua ya Chadema kukamilisha mchakato wake wa ndani huku akihoji namba demokrasi ainavyotekelezwa ndani.

Akizungumza na gazeti moja la kila siku (Si MTANZANIA Jumapili) licha ya Mbowe kushinda tena kwenye nafasi ya uenyekiti lakini ushindi wake hauakisi demokrasi halisi ambayo wamekuwa wakiinadi.

“Ninawapongeza kwa kumaliza mchakato mkutano na kuwapata viongozi mbalimbali lakini suala la Mwenyekiti wao kuendelea kushikilia tena kijiti cha nafasi hiyo si zuri kwa demokrasi halisi ambayo inataka watu kubadilishana vijiti vya uongozi.

“Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere kupitia Katiba ya nchi alipendekeza kuwapo na ukomo wa uongozi wa nafasi za juu, kwa kubadilishana madaraka kiongozi mmoja hadi mwingine, suala ambalo lingekuwa na maana kubwa kama lingefanyika Chadema kwa kuwa linajenga demokrasia ya kweli,” alisema 

Msekwa ambaye pia alikuwa kuwa Spika wa Bunge, alisema kuwa hata kwa upande wa CCM, wapo baadhi ya wabunge wamekaa katika nafasi hizo kipindi kirefu hadi wanapoamua kuacha wenyewe, jambo alilodai si zuri na kushauri liangaliwe upya ili kuepusha wabunge hao kugeuka miungu watu katika majimbo,” alisema Msekwa

MNYIKA NI NANI

Mnyika ambaye alikua mwanaharakati wa kutetea haki za wanafunzi na watu mbalimbali na pia akiwa mtangazaji wa Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD), alishawishiwa na Mbowe kujiunga na Chadema ili kuungana na wanamabadiliko wengine, baada ya kuona uwezo wa Mnyika katika kujenga hoja, umakini, weledi na akili. 

Uwezo mkubwa wa Mnyika ambao aliuonesha katika ukumbi wa Nkrumah Chuo kikuu cha Dar es Salaam (ingawa yeye alikua akisoma masomo ya jioni), ambapo alisimama na kupinga Sera ya Uchangiaji wa Masomo Elimu ya Juu na kusababisha wanafunzi kuanza mgomo chuoni hapo. 

Mnyika akiwa Morogoro, aliombwa kutuliza hali hiyo na alipofika chuoni, aliita wanafunzi na kuwaambia mambo kadhaa ili kupima ujasiri wao. 

Alimuomba rafiki yake kurusha jiwe katikati ya kusanyiko Mabibo Hostel, baada ya kurushwa jiwe hilo, wanafunzi walitawanyika kukimbia ndipo Mnyika aliposema “Ninyi ni waoga. Hamuwezi kupambana. Nawataka muache mgomo endeleeni na masomo”.

Mnyika alikuwa mfuasi wa Chadema mpaka pale alipojiunga na chama hicho mwaka na kufanikiwa kuteuliwa kuwa mgombea ubunge kijana ambaye alichuana na Waziri wa Kilimo wa wakati huo Charles Keenja, katika Jimbo la Ubungo ambapo alijikuta akibwagwa akiwa mshindi wa tatu.

Hakukana tamaa, Mwaka 2010 Mnyika alishinda ubunge katika Jimbo la Ubungo ambapo alikuwa akishindana na Hawa Ngh’umbi (CCM) na ilipofika mwaka 2015 jimbo hilo liligawanywa na kuhamia jimbo la Kibamba ambalo analiongoza hadi sasa baada ya kumshinda aliyekuwa Waziri wa Habari wa wakati huo, Dk. Fenella Mukangara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles