MNH YATUMIA MIL 600 KWA MWEZI KUHUDUMIA WASIOJIWEZA

0
570

VERONICA ROMWALD NA FRANK KAGUMISA (SAUT),DAR ES SALAAMHospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), inatumia kati ya Sh. milioni 450 hadi Sh. milioni 600 kila mwezi kugharamia wagonjwa wanaoshindwa kulipia matibabu yao.

Hayo yalielezwa Dar es Salaam jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Profesa Lawrence Museru alipokuwa akimkabidhi msaada wa baiskeli ya matairi matatu, Said Mtonga ambaye amekatwa miguu yote miwili kutokana na maradhi yanayomsumbua.

“Jukumu letu ni kutibu lakini inapobidi huwa tunaenda zaidi ya hapo na kutoa msaada ‘rehabilitation’, kwa mgonjwa kama huyu, ili anapotoka hapa aweze kwenda kuendelea na majukumu yake, ajenge uchumi wa nchi na wake pia.

“Hivyo, hospitali imegharamia matibabu yake yote kwa kuwa hakuwa na uwezo wa kulipia na kwa mwezi huwa tunatumia kiasi cha kati ya Sh. milioni 450 hadi Sh. milioni 600,” alisema.

Ofisa Ustawi wa Jamii Muhimbili, Wodi ya Kibasila, John Mwakyusa alisema matibabu ya Said yamegharimu Sh. 935,000 tangu alipofika hospitalini hapo Mei, mwaka huu. .

“Alikukuja miguu yake ikiwa imevimba na ina vidonda, alichunguzwa na kuonekana haikuwa saratani, madaktari wakamfanyia upasuaji kukata mguu wake mmoja lakini baadae mguu uliobaki nao ulionyesha tatizo, nao ukakatwa.

“Ndugu zake hawakuwahi kujitokeza, tukawatafuta lakini tulipowapata walitueleza hawakuwa na uwezo wa kumsaidia, hata marafiki zake pia hawakuja,” alisema.

Alisema waliendelea kumtibia hadi alipopona kabisa wakaona ni vema kumtafutia baiskeli ili aweze kutembelea.

“Tunamshuruku mkurugenzi alitupatia Sh. 500,000 tukaenda SIDO kutafuta Sh. 80,000 tukampa mtaji,” alisema.

Mkuu wa Idara ya Ustawi wa Jamii Muhimbili, Emmanuel Mwasota alisema ugonjwa uliokuwa ukimsumbua Said kitaalam unaitwa Septic Wound with Gangrene.

Akizungumza na MTANZANIA, Said aliushukuru uongozi wa MNH kwa kumpatia baiskeli hiyo ambayo itamuwzesha kujitafutia riziki.

“Mimi ni fundi viatu, kabla sijaugua nilikuwa najipatia riziki kwa kazi hiyo kwa ajili ya maisha yangu,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here