25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

MNADA MPYA MAKONTENA YA MAKONDA WATANGAZWA

 

PATRICIA KIMELEMETA, DAR ES SALAAM


Mnada wa pili wa makontena 20 yenye samani zikiwamo   meza na viti, yaliyoingizwa nchini na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, utafanyika Septemba Mosi baada ya ule wa Agosti 25 kutofanikiwa kupata wanunuzi.

Makontena hayo ambayo yamekwama bandarini yanadaiwa kodi ya Sh bilioni 1.2.

Akizungumza na MTANZANIA  Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa (TRA), Richard Kayombo, alisema mamlaka hiyo imeazimia kufanya mnada wa pili Jumamosi.

“Tunatarajia kufanya mnada wa pili wa makontena 20 yaliyopo kwenye bandari kavu ya Dar es Salaam ifikapo Septemba mosi mwaka huu (Jumamosi),”alisema Kayombo.

Alisema mnada huo utaanza saa 2:00 asubuhi kwa kufuata taratibu zote za sheria kama mnada wa awali ulivyofanyika, hivyo wananchi wanapaswa kujitokeza kwa ajili ya kununua samani hizo kwa kufuata taratibu na sheria za minada.

Alisema TRA haiwezi kutangaza bei ya mnada huo kabla ya kufanyika kwa sababu ni siri, lakini wateja watakaofika watakuta bei ambayo imepangwa kwa mujibu wa sheria serikali iweze kupata mapato yake.

“Hatuwezi kupandisha au kushusha bei kwa sababu mnada huu unafanyika kwa mujibu wa sheria za minada, hivyo basi tunafanya siri lakini wateja watakapofika wataikuta na kununua,”alisema.

Aliwaomba wananchi kuondoa hofu kuhusu samani hizo na kuwataka kujitokeza waweze kununua samani hizo.

Baada ya mnada wa Agosti 25 kukwama kwa wateja kushindwa kufikia bei iliyotangazwa, Makonda alijitokeza na kusema mtu atakayenunua makontena hayo aliyosema yana samani za shule za Dar es Salaam, atalaaniwa na Mungu.

“Wananchi na vyombo vya habari wamejitolea na kuendelea kuhamasisha, huku walimu wakichanga kama sehemu ya kujikomboa, leo Mamlaka ya Mapato Tanzania wameamua kuuza samani za walimu kwa wamiliki wa kumbi za starehe walimu waendelee kugombania madawati na vyoo na wanafunzi.

“Mimi Paul Makonda nimefanya kwa sehemu yangu kilichobaki ni mwenye wazo atasimama siku moja kujitetea kwa sababu Mungu ndiye aliyewawezesha watu wakakubali kujitolea,” aliosema.

Aliongeza: “Nakuhakikishia atakayenunua hivi vifaa vya walimu amelaaniwa yeye na uzao wake na kamwe hatafanikiwa katika maisha yake. Nayasema haya nikiwa na uhakika kwa kuwa vya madhabahuni havichezewi.

“Hivi ni vifaa kwa ajili ya walimu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mungu hakunipa kwa ajili ya baa wala kumbi za starehe,” alisema Makonda.

Baada ya kauli hiyo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alimjibu Makonda   akisema makontena hayo yatapigwa mnada mteja atakapopatikana.

“Niliapa kutekeleza sheria za nchi na sheria za kodi. Katika usimamizi wa sheria hizi, kamishna zisimamie bila kuyumba. Piga mnada mara ya kwanza, ya pili na ya tatu kadri sheria inavyokuruhusu.

“Sheria inasema mzigo ulioagizwa kutoka nje hauna msamaha wa kodi. Hivyo, mchakato ulioanza kuutekeleza endeleeni nao,” alisema Dk Mpango akimuelekeza Kamishna wa Forodha, Ben Usaji.

Dk. Mpango alisema, “Niwaombe viongozi wenzangu serikalini tuchuje maneno. Nawaomba Watanzania, anayetaka kuja kununua samani hizi asiogope, aje kununua.

“Haipendezi kusikia eti mtu atakayenunua samani hizi atapata laana, tena ya Mungu. Kwa nini tunahusisha Mungu kwenye vitu vya namna hii? Nawaomba Watanzania anayetaka kuja kununua samani hizi aje, hakuna cha laana wala nini.

“Kamishna piga mnada mara ya kwanza, ya pili, ya tatu kadri sheria inavyokuruhusu. Hata mimi ningekuwa na hela ningekuja kununua tuone hiyo laana inatoka wapi”.

Kuhusu kauli ya Makonda kuwa samani hizo ni kwa ajili ya ofisi za walimu, Dk. Mpango alisema Serikali inathamini mchango wao na inafanya kila liwezekanalo kuhakikisha inaboresha mazingira yao ya kazi.

“Tuliapa kusimamia sheria. Sheria za kodi mimi ndiye mwenye dhamana hivyo niulizeni ni wajibu. Si sahihi hata kidogo kuingilia utaratibu ambao umebainishwa kisheria. Kamishna endelea kupiga mnada mpaka kieleweke,” alisema.

Waziri Mpango alisema sheria haitoi msamaha kwa samani kutoka nje na kila anayeziagiza anapaswa kufahamu hilo.

“Nimejizuia sana kujibizana kwenye mitandao, hii si hulka yangu lakini haya ndiyo maelekezo ya Serikali,” alisema Mpango.

Historia ya makontena

Suala  la makontena hayo lilianza baada ya tangazo la TRA lililochapishwa kwenye gazeti la Serikali la Daily News Mei 12, likiwataka wamiliki wa mali zilizokaa bandarini kwa zaidi ya siku 90 kujitokeza kuzilipia.

Tangazo hilo lilionyesha kuwa TRA inakusudia kufanya mnada wa wazi Juni kwa mizigo iliyokaa bandarini kwa muda mrefu bila kukombolewa, ikiwamo ya Paul Makonda.

Kwa mujibu wa tangazo hilo lililotolewa na Kaimu Kamishna wa Forodha na Ushuru wa TRA, Ben Asubisye, wamiliki walitakiwa kuitoa mizigo hiyo ndani ya siku 30 kuanzia siku ilipotangazwa.

Tangazo hilo lililokuwa na orodha ya makontena zaidi ya 800, jina la Paul Makonda lilijitokeza mara 20 akiwa mpokeaji wa makontena 20 yaliyopo katika bandari kavu ya DICD yakiwa na samani.

Ingawa hakukuwa na uthibitisho kuwa Makonda ndiye mwenye makontena hayo wakati huo, Februari 16 mkuu mkuu wa mkoa huyo alikaririwa katika mtandao wa gazeti la Serikali la HabariLeo akisema  alipokea makontena 20 yenye samani zitakazotumika katika ofisi za walimu zinazoendelea kujengwa.

Mzigo huo ulikuwa sehemu ya shehena ya makontena 36.

Samani hizo za ofisini zilizokuwa na thamani ya Sh bilioni mbili zilitolewa na Watanzania wanaoishi Marekani wanaojulikana kama Six Region Diaspora Council.

 

 

 

 

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles