27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

MMILIKI LUCK VINCENT KUSOMEWA MASHTAKA YA AWALI

Na JANETH MUSHI-ARUSHA


MAHAKAMA ya Wilaya ya Arumeru, Mkoa wa Arusha, inatarajia kuwasomea hoja za awali watuhumiwa wawili, akiwamo mmiliki wa Shule ya Lucky Vincent ya jijini Arusha, Innocent Mushi.

Watuhumiwa hao wanakabiliwa na makosa ya usalama barabarani, ikiwamo kusafirisha watoto bila kuwa na vibali muhimu.

Mushi na Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule hiyo, Longino Nkana, walifunguliwa kesi namba 78 ya mwaka huu, katika Mahakama ya Wilaya ya Arumeru, wakikabiliwa na makosa ya usalama barabarani.

Mbele ya Hakimu Mkazi, Jasmine Abdul, Wakili wa Serikali, Fortunatus Mhalila, aliieleza mahakama hiyo kuwa, upelelezi umekamilika, hivyo wanaomba kupangiwa tarehe nyingine ya kuwasomea hoja za awali za kesi hiyo. Kutokana na kauli hiyo, Hakimu Abdul aliahirisha shauri hilo hadi Agosti 28, mwaka huu.

Awali, wakisomewa mashtaka yao Mei 12, mwaka huu, mtuhumiwa wa kwanza ambaye ni Mushi, alidaiwa kukabiliwa na makosa manne, wakati Nkana akituhumiwa kwa kosa moja.

Wakili wa Serikali, Rose Sule, alidai Mushi akiwa Mkurugenzi wa Shule ya Lucky Vincent, aliruhusu kuendeshwa gari la abiria bila ya kuwa na leseni ya usafirishaji.

Alidai kuwa, Mei 6, mwaka huu, katika eneo la Kwamrombo, wilayani Arusha, mtuhumiwa huyo alifanya shughuli ya usafirishaji wa abiria akiwa na gari aina ya Mitsubishi Rossa, lenye namba T 871 BYS.

Alilitaja kosa la pili kuwa ni mtuhumiwa huyo kuruhusu kuendeshwa kwa gari bila kuwa na bima, Mei 6, mwaka huu.

“Kosa la tatu ni kushindwa kuingia mkataba na mwajiriwa wake, ambapo Mei 6, mwaka huu, ukiwa mmiliki wa gari hilo, ulishindwa kuingia mkataba wa ajira na dereva wako, Dismas Gasper, ambaye kwa sasa ni marehemu.

“Mtuhumiwa unakabiliwa na kosa la nne ambalo ni la kubeba abiria waliozidi 13, ambapo Mei 6, mwaka huu, ukiwa mkurugenzi, ofisa msafirishaji na mmiliki wa Lucky Vincent, ulibeba na kusafirisha abiria zaidi ya 13, kinyume cha sheria,” alidai wakili huyo.

Kwa upande wa mtuhumiwa Nkana, Wakili Sule, alidai aliandaa safari iliyozidi abiria 13, huku akijua ni kinyume cha sheria.

Miezi michache iliyopita, wanafunzi wa Shule  ya Msingi Luck Vincent ya Arusha, walipata ajali ya basi na wenzao 32 kufariki pamoja na dereva na mwalimu wao mmoja.

Pamoja na vifo hivyo, wanafunzi watatu walionusurika, walisafirishwa kwenda Marekani ambako hadi sasa wanaendelea na matibabu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles