27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Mlinzi wa Dk. Slaa atoboa siri

NA WAANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
TUHUMA za mauaji ya Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, zimeendelea kutikisa pembe za nchi huku mlinzi wake binafsi, Khalid Kagenzi, akitoboa siri za mkasa huo.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Mabere Marando, kudai mlinzi huyo alikuwa akitumiwa na vyombo vya usalama kwa lengo la kumuua Dk. Slaa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kagenzi alisema hausiki na mpango huo ila kuna watu ndani ya Chadema wamekuwa wakimtuhumu bila kutoa uthibitisho wa madai hayo.
Akiwa amefuatana na mtoto wake wa kiume katika Ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo, alisema taarifa iliyotolewa Machi 8, mwaka huu kwa waandishi aliiandika yeye kwa kushinikizwa baada ya kupigwa na kuteswa, huku akitishiwa kuuawa na walinzi wenzake wa Chadema.
Alisema Machi 7, mwaka huu aliitwa katika ofisi ya Makao Makuu Chadema ambako aliingizwa katika chumba kilichokuwa na watu watano aliowatambua kwa majina ambao ni Boniface Jacob ambaye ni Diwani wa Ubungo, Hemedi Sambura, Benson Mramba, na watu wengine wawili aliowataja kwa majina moja moja ya Jumanne na Mamba.
Kagenzi alisema baada ya kuingizwa ndani ya chumba hicho, aliona begi lililokuwa limehifadhiwa bisibisi, kisu, bikari na ‘plies’ ambazo walizitumia kumpiga na kumtesa.
“Ndani ya chumba hicho waliniweka kwenye kona na sikuwa na wasiwasi na kuniamuru ‘weka vitu vyako hapo’, nikawajibu hawana sheria ya kuniambia hivyo kama kuna tatizo waniambie.
“Beni alinyanyuka na kunipiga teke la ubavuni, tena teke la nguvu, sijakaa sawa akanipiga teke jingine na kunibamiza na mbao alizokuwa amezifunga mikononi, nikaanguka chini.
“Walichukua mkanda na wakanifunga mikono nyuma na miguu wakaanza kunipiga kwa mkanda wa jeshi na mbao, nikawauliza ‘mbona mnanipiga, mnataka kuniua kosa langu ni lipi’, akajibu wewe si unashirikiana na Philip Mangula (Makamu Mwenyekiti wa CCM) na wanausalama, ndipo wakanivua nguo zote wakaanza kunipiga nikiwa uchi wa mnyama na kunidhalilisha.
“Ndipo waliponiuliza ulipewa chupa ya sumu kumuua Dk. Slaa, nililia sana… nikawauliza kwanini hamjaniambia, wakanilazimisha kuandika maelezo kuwa ninashirikiana na Mangula na watu wa usalama, nikakataa.
“Walinipiga hadi saa moja usiku, nilipoona kipigo kimenizidi nilikubali kuwa ninashirikiana na Mangula ili nisije nikapoteza uhai wangu nikaacha familia yangu na watoto wangu, walitoka nje nikapata mwanya wa kuchukua simu na kumpigia mtu mmoja kumweleza kuwa ninakufa huku, nikaizima nikairudisha ilipokuwa.
“Askari walifika katika eneo hilo wakazunguka zunguka, lakini hawakutambua kuwa kuna mtu ndani hivyo waliondoka,” alisema Kagenzi.
Kutokana na kipigo hicho, alisema alikubali kuandika maelezo ambayo walinzi hao wa Chadema walitaka.
“Niliwambia nimeshaandika kile mlichokitaka waniache niondoke, lakini waliendelea kunipiga na ilipofika saa nne usiku walisema Dk. Slaa amesema niachwe na nipelekwe katika hoteli, ndipo wakanipeleka katika Hoteli ya Valley View iliyopo Sinza kwa kutumia gari lenye namba za usajili T 384 BKL aina ya Benz.
“Walinichukua na kuanza safari ya kwenda hotelini na walichukua vyumba vitatu vyenye namba A1, A2 na A3, mimi waliniingiza chumba A1 na wao walitumia chumba namba A2 na A3.
Alidai walipokuwa hotelini hapo walimtaka kuandika kile watakachomwambia na alipokataa walitoa fuko lenye silaha wakamtisha kwamba asipoandika wanaendelea na kazi yao.
“Pia waliniamuru nitaje nilipoficha chupa ya sumu ambayo nimeiandaa kuitumia kumuua Dk. Slaa tuhuma ambazo si za kweli,” alisema Kagenzi.
Pamoja na hali hiyo, alisema watu hao walilazimika kwenda hadi nyumbani kwake ambako walimkuta mkewe na kupekua kila kona ya nyumba kwa lengo la kutafuta chupa yenye sumu.
“Nilikubali kuandika walichokuwa wakiniambia na karatasi hiyo ndiyo iliyotumika kutoa taarifa kwa waandishi wa habari kwamba nimekiri kupanga njama za kumuua Dk. Slaa nikishirikiana na CCM pamoja na maofisa wa Usalama wa Taifa,” alisema
Mlinzi huyo binafsi wa Dk. Slaa alisema pamoja na kutakiwa kufanya hivyo alitakiwa kueleza uhusiano wake na Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa, Philip Mangula huku wakidai alimtumia fedha.
“Sioni sababu kuwa na namba ya mtu au kutumiwa fedha, kutumiwa fedha si kosa kwa sababu hata Dk. Slaa ana namba za viongozi wa CCM na wanawasiliana.
“Mimi unaweza kunikuta na namba ya Mangula au mtu wa CCM, lakini kwani ni kosa? Kuwa na namba ya mtu au kutumiwa fedha na mtu si kosa.
“Ukimkuta Dk. Slaa au kiongozi wa chama yeyote si wana namba zao? Mfano Mbowe au Dk. Slaa si wanawasiliana na watu wa CCM, kwani ni kosa? Sina kosa, nimefanya kazi na huyu mzee kwa muda,” alisema Kagenzi.

ALINDWA
Akiwa ndani ya ukumbi wa Maelezo, muda wote nje walikuwapo baadhi ya watu ambao walikuwa wakiranda na baada ya kumaliza mkutano na waandishi watu hao walikuwa wakimfuta kwa nyuma.

WALINZI WENGINE MBARONI
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, linawashikilia watu wawili ambao ni makada wa Chadema, Benson Mramba na Hemed Sabura kwa tuhuma za kumshambulia, kumpiga, kumjeruhi Kagenzi.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Camillus Wambura, alithibitisha kukamatwa kwa watu hao na kwamba wanashikiliwa tangu jana saa nne asubuhi katika Kituo cha Polisi Oysterbay.
“Ni kweli tunawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kumshambulia, kumpiga na kumjeruhi Khalid Kagenzi ambaye ni mlinzi wa kujitegemea wa Dk. Slaa.
“Watuhumiwa hawa tayari tumeshawafungulia jalada la mashtaka na tunaendelea kuwashikilia kwa ajili ya mahojiano zaidi,” alisema Kamanda Wambura.

PROFESA ABDALLAH SAFARI
Alipoulizwa hatua ambazo chama kimechukua kuhusu suala hilo, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari, alisema hakuwa na taarifa za walinzi wake kushikiliwa na polisi, na kama wamevunja sheria wapelekwe mahakamani.
“Sina taarifa za kukamatwa kwa vijana wetu wa ulinzi, nina taarifa za Kagenzi peke yake, hata hivyo kama polisi wanadhani sheria imevunjwa basi wapelekwe mahakamani na sisi tutaweka wanasheria wa kuwatetea,” alisema Profesa Safari.

CCM WAIBUKA
Kwa upande wao Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimewataka wananchi kupuuza tuhuma za uzushi unaotolewa na Chadema wa kukihusisha chama hicho na mikakati ya kumdhuru Dk. Slaa.
Kauli hiyo ilitolewa jana mjini Dodoma na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, ambaye alisema tukio hilo ni mwendelezo wa tuhuma za uongo ambazo hutolewa na chama hicho mara kwa mara.
Alisema hatua hiyo inatokana na Chadema kukosa ajenda za maana mbele ya umma jambo ambalo sasa wanaibuka na kuokoteza hoja za kipuuzi.
“Kimsingi tuhuma hizi ni za kipuuzi, lakini uongo huu usipojibiwa unaweza kugeuzwa kuwa ajenda na Chadema kutokana na kukosa ajenda nyingine za maana.
“Hakuna asiyejua kuwa Chadema kwa sasa inapumulia mashine, hivyo maneno na matendo yao kwa sasa lazima ya lenge kujaribu kujinasua na balaa la kufa kwa chama chao.
“Eti CCM ipange kumdhuru Dk. Slaa ili ipate nini kwa kudhurika kwake? Kwa umri wake, afya yake na kadhalika, kwanini CCM ipange kumdhuru mzee huyu? Huu ni mwendelezo wa tabia yake ya kuzusha mambo ya uongo kila anapoona anachuja kisiasa,” alisema Nape.
Alisema mtu aliyetumika kuufikisha uongo huo kwa umma, naye ana historia ya kuzusha mambo na kusema hata asiyoyaamini.
Nape alisema Marando aliwahi kuitisha kikao na waandishi wa habari na kudai Katibu NEC wa Itikadi na Uenezi alifaidika na fedha za EPA, lakini alipobanwa na mteja wake aliyekuwa akimtetea mahakamani kwa kesi hiyo hiyo ya EPA akakanusha matamshi yake kwa maandishi na kudai kuwa lilikuwa shindikizo la chama.
“Mzee huyo ni mnafiki, hebu tujiulize ni lini Marando aliacha rasmi kazi yake ya awali ya ukachero mpaka aaminike leo kufanya kazi afanyayo, nani alimtumia kujaribu kusambaratisha chama cha NCCR-Mageuzi miaka ya mwanzo ya mfumo wa vyama vingi nchini? Hivi ni kweli Marando ni wa kuaminiwa leo?” alihoji Nape.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles