Imechapishwa: Tue, Sep 12th, 2017

MLINZI SUMA JKT MBARONI SHAMBULIO LA MEJA JENERALI MRITABA

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linamshikilia askari wa Suma JKT aliyekuwa mlinzi nyumbani kwa Meja Jenerali Mstaafu Vincent Mritaba aliyejeruhiwa kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana.

Meja Jenerali Mritaba alishambuliwa kwa risasi mkononi, tumboni na kiunoni na watu wasiofahamika wakati akiingia nyumbani kwake Ununio, jijini Dar es Salaam jana mchana.

Akizungumza na Mtanzania Digital, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Lazaro Mambosasa leo Septemba 12, amesema, wanamshikilia mlinzi huyo kwa kuwa aliweka silaha yake chini na kwenda kufungua geti kitendo kilichompa nafasi mhalifu kutekeleza shambulio hilo na kufanikiwa kukimbia.

“Tunamshikilia mlinzi wa Suma JKT ambaye aliweka silaha chini kwenda kufungua geti huku akiacha mwanya kwa mhalifu kutekeleza tukio hilo na kufanikiwa kuondoka na kiasi cha Sh milioni tano na kumshambulia kwa risasi Meja Jenerali Mritaba,” amesema Kamanda Mambosasa.

Meja Jenerali Mritaba amelazwa katika Hospitali ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Lugalo, Jijini Dar es Salaam akiendelea na matibabu.

Weka maoni yako

XHTML: You can use these html tags: <a href="" title=""> <abbr title=""> <acronym title=""> <b> <blockquote cite=""> <cite> <code> <del datetime=""> <em> <i> <q cite=""> <s> <strike> <strong>

YOUTUBE

MLINZI SUMA JKT MBARONI SHAMBULIO LA MEJA JENERALI MRITABA