31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Mlango upi umemfungulia mwenzako katika maisha yako?

KILA ambaye yuko katika mahusiano anaishi katika dunia yake. Anawaza kinyake na kutafakari mambo katika namna yake. Ila wale walio katika mahusiano huwa wana dunia mbili.

Ni ama wenzao wawafungulie mlango wa dunia ya furaha, amani na raha au wawafungulie mlango wa mateso, dhiki na karaha. Mwenzako katika mahusiano yenu amekufungulia mlango gani?

Kila mtu akiwa nje ya mahusiano hutamani kuwa katika mahusiano ya raha na amani. Hata siku moja, hakuna mtu akiingia katika uhusiano akatarajia kuteseka.

Na njia nzuri ya kumfungulia mwenzako mlango wa furaha ni wewe kuacha ubinafsi, kumsoma mwenzako na kumwelewa na kufahamu kuwa furaha na amani yako inaanzia kwa kwake.

Dunia ya mtu ambaye hayuko katika mahusiano huenda ikawa na upweke lakini katu haiwezi kuwa na mateso. Hivyo mwenzako anapokuja kwako, shida yake kuu ni wewe kumfanya asiwe mpweke lakini pia apate furaha na amani ambayo hakuwa anaipata kipindi akiwa mwenyewe.

 Mwenzako anahitaji kuona thamani yake ambayo hakuwa anaiona alipokuwa mwenyewe. Anataka kuonja uzuri wa dunia ambayo mwanzo hakuwa akiishi.

Ukifanikiwa kumfanya mwenzako akafurahia dunia ambayo umempeleka siyo tu atakuwa na furaha na amani ila pia atakuona tumaini na mshirika wa kweli katika maisha yake.

 Wapo wanawake walio tayari siyo tu kubadili dini na kuhama nchi zao ila pia hata kutengwa na dunia nzima ila siyo kuachana na wanaume walionao. Hali hiyo haitokei kwa sababu ya uchawi ama ulimbukeni wa wanawake hao.

 Ila hutokea kwa sababu wamepelekwa katika dunia waliyokuwa hawapo ila walikuwa wakiitamani na kuiota miaka mingi.

 Kwani wanaume wangapi huitwa wamerogwa kisa wako radhi kuwalinda na kuwatetea wanawake wao kwa kila hali na kwa kila mbinu? Usiamini kuhusu habari za kurogwa ila tafakari juu ya dunia ambayo wenzao wamewapeleka.

Kama umemtoa mwenzako katika dunia yake ya utulivu, upweke ila isiyokua na maumivu na karaha na ukampeleka dunia ya karaha na mateso, abadani hawezi kujiona kabahatika kuwa na wewe.

Daima hawezi kujipanga katika kulinda na kutetea penzi lake kwako. Ni nani anapenda kuwa na zimwi limmalizalo furaha katika maisha yake?

 Mwenzako atapima thamani yako kutokana na aina ya mlango wa dunia unayomfungulia. Kama ukimfanya kuumia na kulia, atakuona mshenzi usiyefaa kuenziwa. Ila kama utamfanya adeke, afurahi basi atakulinda na kukutunza kwa nguvu na maarifa yake yote.

Aina ya maisha unayompa mwenzako ndiyo yanayotengeneza mtazamo wake kwako na kujenga mfumo wenu wa mahusiano. Kuwa makini.

 Thamini ujio wa mwenzako katika maisha yako kwa kumpa yote anayostahili na kujenga taswira njema katika akili yake.

 Tambua  mapenzi bora utakayompa sio tu yatamfanya kuwa na furaha na amani ila pia yatamsukuma kuwa mtu mwema na bora katika familia yako.

Kumbuka, watoto wenu watakuwa wamoja, wenye furaha na amani kutokana na ninyi kuwa katika mapenzi ya amani na raha.

 Tafiti zinaonesha watoto waliozaliwa na wazazi wasio na furaha katika mahusiano yao mbali na wao kukosa furaha ila pia hata ubunifu wao kiakili huwa mdogo.

Watoto wa aina hii hata wakiwa watu wazima, hujikuta na wao wakishindwa kujenga mahusiano ya amani kwa sababu walikosa mfano bora toka kwa wazazi wao toka awali.

 Maisha ya watoto ya baadaye hujengwa kutokana na mambo na matukio wanayokutana nayo wakiwa wangali wadogo. Kama katika umri mdogo hawaoni thamani ya upendoana kupendana kutoka kwa wazazi wao, hata wao wakiwa wakubwa watashika uelekeo huo wa maisha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles