33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mkwasa arudi na kifurushi cha visingizio

tanzania-2NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

KOCHA Mkuu wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Charles Boniface Mkwasa, amerudi na kifurushi cha visingizio, akifichua sababu zilizoiua timu hiyo na kupokea kipigo cha fedheha cha mabao 7-0 dhidi ya Algeria ‘The Desert Foxes’.

Stars ilipokea kipigo hicho kwenye mchezo wa raundi ya pili ya kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2018 nchini Urusi, kilichoifanya kutolewa kwa jumla ya mabao 9-2 kufuatia sare ya 2-2 ya mechi ya awali.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mkwasa alisema mbali na uwezo mkubwa wa wapinzani wao, amedai Algeria ilitumia mbinu nyingi chafu nje ya uwanja zilizowaathiri wachezaji wake kisaikolojia.

Alisema mbinu ya kwanza iliyowaondoa mchezoni wachezaji wake, ni namna waamuzi walivyokuwa wakali kwa upande wao huku wakiwapendelea kwa kila kitu Algeria.

“Waamuzi walituvuruga, walikuwa wakiwakaripia wachezaji wetu na kuanza kutoa kadi zisizo na msingi, kwani hadi dakika ya 40, tulikuwa tumeshapata kadi nne za njano na kadi nyekundu, hivyo tukawa tunacheza kwa tahadhari, lakini kibaya zaidi waamuzi wale walikuwa wakizungumza lugha moja ya Kifaransa na wachezaji wa Algeria huku wakicheka,” alisema.

Mkwasa aliendelea kusema kuwa, pia wapinzani wao walidiriki kuumwagia uwanja maji kupitiliza, jambo ambalo liliwafanya wachezaji kuteleza mara kwa mara na kuzaa bao la kwanza la sekunde 45.

“Algeria ilimwagia uwanja maji wakati sisi tukitaka kuanza kupasha misuli kabla ya kuanza mchezo, tulipokwenda vyumbani kuvaa wakamwaga maji tena, wao walijiandaa kwa kuvaa viatu maalumu vya kuzuia utelezi.

“Matokeo yake tukafungwa bao hilo mapema baada ya Kapombe (Shomari) kuteleza wakati akiokoa pasi na Brahimi akafunga, vilevile walimwagia tena maji wakati mpira ulipoenda mapumziko na kuna baadhi ya maeneo mengine walimwagia maji wakati mpira unaendelea,” alisema.

Kocha huyo wa zamani wa Yanga, alisema wapinzani wao walienda mbali zaidi kwa kutoupiga vizuri wimbo wa Taifa wa Tanzania baada ya kutosikika vizuri, huku  mashabiki wa Algeria wakizomea wakati ulipokuwa ukipigwa.

“Pia wenyeji wetu waliwakataa wakalimani wetu wa kututafsiria mambo mbalimbali na kuwaweka wa kwao, jambo hilo lilionyesha kuwa kuna mipango waliandaa ya kutuficha vitu…Vilevile winga wao Yacine Brahimi, aliyeukosa mchezo wa kwanza alituweka kwenye wakati mgumu sana, alikuwa hazuiliki, aliweza kuwachukua watu hadi watatu na kupita,” alisema.

Katika hatua nyingine, Mkwasa aliwaomba radhi Watanzania wote kwa kipigo hicho, huku akiwataka wasikate tamaa na waendelee kuiunga mkono timu hiyo.

“Tumepoteza na imetuuma sana, hatukutarajia yale, kwa niaba ya benchi la ufundi na wachezaji kwa ujumla, tunawaomba radhi Watanzania wote, kuwa haya matokeo yaliyotokea hatukuyapenda, tunaomba watusamehe sana, naamini tumejifunza na haya mambo yatatupa uzoefu huko tunapoelekea, timu bado tunaijenga, kikubwa waendelee kuiunga mkono,” alisema.

Naye Nahodha Msaidizi wa Stars, John Bocco, aliwashukuru Watanzania kwa namna walivyojitolea kuisapoti timu hiyo, tokea kwenye mechi mbili za awali dhidi ya Malawi na zilizopita za Algeria, huku akiwataka waendelee kuwaunga mkono katika mechi zinazokuja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles