24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Mkwasa amlilia Keshi

Stephen-Keshi*TFF watuma salamu za rambirambi NFF

NA BADI MCHOMOLO, DAR ES SALAAM

KOCHA wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Boniface Mkwasa, amedai kuguswa na kifo cha aliyekuwa kocha wa timu ya Taifa ya Nigeria (Super Eagles), Stephen Keshi, ambaye amefariki jana mjini Benin nchini Nigeria.

Mkwasa amedai kwamba alikuwa anajifunza mengi kutoka kwa kocha huyo ambaye alifanya makubwa kwa taifa lake tangu akiwa mchezaji hadi nafasi ya ukocha.

“Kifo cha Keshi kimemgusa kila mmoja mwana familia ya soka hasa kwa upande wa barani Afrika, alikuwa kocha wa mfano kwa makocha wengi Afrika kwa kuwa aliweza kutwaa ubingwa wa Kombe la Mataifa Afrika akiwa kama mchezaji.

“Hata hivyo, wakati anaifundisha timu hiyo mwaka 2013 aliipatia ubingwa huo kwa mara ya pili, hivyo ni historia kubwa ambayo ameiacha katika historia ya soka nchini humo.

“Kwa upande wangu nikiwa kama kocha mzawa wa Taifa Stars nilikuwa najifunza mengi kupitia yeye, hasa kwa kujipa moyo wa kuisaidia timu yangu ya Taifa nikiwa kama mzawa, pengo hili ninaamini haliwezi kuzibwa na yeyote.

“Ninaungana na familia ya wanasoka wote Afrika kwa ujumla katika kipindi hiki kigumu kwa kumpoteza kiongozi huyo bora katika soka,” alisema Mkwasa.

Kwa upande wa Frederick Mwakalebela, alisema: “Keshi ni kocha ambaye ameleta utamaduni wa nchi mbalimbali kuwaamini makocha wazalendo na kuwapa timu za Taifa, tutamkumbuka kwa misimamo yake na mafanikio aliyowapatia Wanigeria,” alisema Mwakalebela.

Keshi amepoteza maisha ghafla huku akiwa na umri wa miaka 54, kwa mujibu wa wanafamilia na marafiki zake wa karibu, Keshi hakuonesha dalili zozote za kuumwa, ila inadaiwa kwamba kocha huyo amepoteza maisha kutokana na msongo wa mawazo kwa kumpoteza mke wake ambaye alifariki mwaka jana kutokana na kusumbuliwa na saratani.

Keshi amekuwa kocha pekee mzawa kutwaa taji la Mataifa ya Afrika akiwa kama mchezaji na baadaye akiwa kocha, mbali na kuifundisha Super Eagles, aliwahi kuifundisha Togo na Mali.

Alianza kuichezea timu ya Taifa akiwa na umri wa miaka 20 kuanzia mwaka 1982 hadi 1994, akiwa nahodha wa timu hiyo ambapo alikuwa anacheza nafasi ya ulinzi.

Taifa Stars inatarajia kukutana na Super Eagles kwenye michuano ya kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika, mchezo huo unatarajiwa kupigwa Septemba 2 mwaka huu nchini Nigeria, huku wenyeji hao wakiwa chini ya kocha wao, Daniel Amokach.

Hata hivyo, Stars itacheza na Nigeria kwa kukamilisha ratiba yake kwa kuwa tayari ndoto za kufuzu zimeyeyuka huku kundi hilo likiongozwa na Misri, ambao tayari wana pointi 10 wakifuatiwa na Nigeria wenye pointi 2, huku Tanzania ikiwa na pointi 1.

Shirikisho la soka nchini Tanzania (TFF), linaungana na wanasoka wote katika kuomboleza kifo cha nyota huyo wa zamani wa Nigeria, Keshi ambapo Rais Jamal Malinzi ametuma salamu za rambirambi kwa Rais wa Shirikisho la Soka Nigeria (NFF), Amaju Pinnick, familia ya marehemu Keshi pamoja na ndugu, jamaa, marafiki walioguswa na msiba wa gwiji huyo.

Katika rambirambi ambazo zimefika pia katika Ofisi za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Rais Malinzi amesema kuwa japokuwa Keshi ametangulia mbele za haki, mchango wake kwenye mpira wa miguu hautasahaulika kwani atabaki kuwa alama ya maendeleo ya mchezo wa soka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles