27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mkurugenzi wa Mashtaka amvaa Lema

Kulwa Mzee – Dar Salaam

MKURUGENZI wa Mashtaka nchini (DPP), Biswalo Mganga, amesema taarifa alizotoa Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema, kuhusu kuuawa kwa watu 13 ni za upotoshaji na hivyo watamchukulia hatua.

Alisema hivi karibuni Lema alikamatwa mkoani Singida kwa tuhuma za kutoa taarifa za uongo kwamba watu hao wameuawa bila Serikali kuchukua hatua.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Biswalo alisema; “sitajali mwanasiasa wa chama chochote, rangi, kabila au cheo, yeyoto anayefanya makosa atafunguliwa mashtaka, na kwa hili nitachukua hatua, hawawezi kuendelea na upotoshaji wa aina hiyo.

“Watanzania wana haki ya kutoa maoni, lakini wasitumie haki hiyo kwa masilahi yao binafsi, iwe wanasiasa au raia, kama mtu anadiriki kusema kuna watu 13 wameuliwa na mmoja kuchomwa moto, ana lengo la kuitishia amani.

“Katiba ya nchi inakupatia uhuru wa kujieleza, lakini hakuna uhuru usio na mipaka, tusikimbilie haki za binadamu.

“Hatuwezi kutumia kigezo cha haki za binadamu kuvunja umoja na amani ya nchi kwa sababu una haki ya kusema chochote,” alisema Biswalo.

Alisema Lema ameorodhesha kesi nane na kudai Jumanne Nderema alichinjwa na Serikali haijafanya lolote, tukio la Feb 5, mwaka huu eneo la Sasajila, Manyoni

DPP akifafanua matukio ya vifo aliyoyataja Lema, alisema Hamis Chadem (25) amekamatwa na sababu ya kifo cha Jumanne ni mwili kukutwa na majeraha na sehemu ya shingo imekatwa.

Alisema marehemu na mshtakiwa ni mtu na kaka yake, ambapo alikuwa akimtuhumu kufanya mapenzi na shemeji yake, hivyo alimvizia alipolala na kumkata na kesi namba 4 ya mwaka huu imefunguliwa Mahakama ya Wilaya ya Manyoni.

Pia alimtaja Issa Abdallah tukio lililotokea Januari 23 eneo la Sanjalanda, ambapo polisi wamefungua jalada kwa mshtakiwa Maria Robert (21).

Alisema marehemu hakuchinjwa na taarifa ya daktari inaonyesha ni mtoto wa kuzaliwa na mshtakiwa huyo, alikuwa na mgogoro na mumewe ambaye alikuwa hampatii matunzo hivyo alimnyonga mtoto wake mpaka kufa na akatoa taarifa za uongo Januari 27, amefunguliwa kesi ya mauaji namba 3 ya mwaka huu.

“Tukio la Novemba 21 mwaka jana, Mnyambelele Nyandu wa Itigi anadai amechinjwa, anarukia mambo ambayo hayawahusu, Myambelele Nyandu ni mshtakiwa kamuua mkewe Shoma Ngasa. Mshtakiwa ana wake wawili, mwengine ni Ana Makilrma, aliwapiga viboko wake zake na wakiwa ndani alimpiga mpaka kusababisha kifo chake, alifunguliwa kesi namba 22/2019.

“Tukio la Martin Motelewa, alichomwa moto. Washtakiwa Msem Hamidu (33) na Athanas Stephani maarufu Manyama walikamatwa, taarifa ya daktari na maelezo kwenye jalada ni kupigwa na kitu kizito usoni na kuchomwa moto, alikuwa amelala kwenye pagale, hakuna ushahidi wa kuwaunganisha watuhumiwa, hivyo walihojiwa na kuachiwa.

“Alex Jonas wa Manyoni mjini ni Katibu Mwenezi Wilaya Manyoni (Chadema), tukio la Februari 26 mwaka huu na sababu ya kifo ni kuvuja damu nyingi, alikuwa na majeraha upande wa uso na hadi sasa hakuna mshtakiwa aliyekamatwa na polisi wanaendelea na upelelezi. Aliuawa, lakini hakuchinjwa, alikatwa kwenye paji la uso,” alisema Biswalo.

Alisema Lema alidai pia Msechelela Leonard alichinjwa, lakini polisi wamefungua jalada na washtakiwa ni Rashidi Rashidi (34), Timothy Kindulu na Gervas maarufu Etoo.

Biswalo alisema marehemu alikuwa ni mtoto wa diwani wa CCM, alivuja damu kutokana na majeraha kichwani na michubuko tumboni, lakini hakuna maelezo kama alichinjwa.

“Kwanini watoe taarifa za uongo, kwamba Serikali na watu wake hawafanyi kitu chochote, tufanye siasa zenye ustaarabu, hakuna haki pasipo wajibu, kifungu 9 cha makosa ya jinai nawajibika kwenda kutoa taarifa polisi kueleza.

“Aje (Lema) aniambie ni lini alienda kutoa taarifa na kwamba hao watu anawafahamu, hatuwezi kuendelea kuwa na watu kueneza taarifa za uzushi na zenye kueneza chuki na kusababisha watu wakae kwa mihemuko kwamba hakuna amani.

“Baadhi ya watu wanasema wanachama wa upinzani wanaonewa wakati wanafanya mambo ya kipuuzi, usijifiche kwenye siasa, iwe CCM au chama chochote kwa kufanya watu waishi kwa hofu, haki za kikatiba zisije zikaathiri mambo ya watu wengine,” alisema Biswalo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles