27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Mkurugenzi Mkuu afichua ‘wajanja’ walivyotaka kukwamisha Bandari

Mwandishi Wetu -Dar es Salaam

MKURUGENZI wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Deusdedit Kakoko, ameeleza namna baadhi ya watu walivyohujumu mamlaka hiyo na kufanya baadhi ya wateja kukimbia, hatua iliyowalazimu kufanya kampeni kubwa ya kuwarudisha na kupandisha mapato.

Akizungumza Dar es Salaam mwishoni mwa juma, Kakoko alisema baadhi ya hujuma hizo zilikuwa zikifanywa ndani na nyingine nje ya Bandari.

Alisema hujuma hizo zilisababisha shehena, hasa ya magari kushuka kwa kiasi kikubwa. Baadhi ya watu wakiwamo wa hapa nchini  walianza kuagiza magari kupitia bandari za nchi jirani.

Akitoa takwimu, alisema mwaka 2014/15 magari yaliyoingia kupitia Bandari ya Dar es Salaam yalikuwa 163,772, mwaka 2015/16 magari 127,335 mwaka 2016/17 magari 93,471 na mwaka 2018/19 magari 159,939.

“Shehena ya magari iliporomoka sana kwa sababu ya uhuni uliokuwa unafanyika hapa, mtu analeta gari lake linaingizwa kwenye mnada, kuna mama mmoja nilimkuta Lubumbashi (Congo) analia.

“Aliagiza gari lake akaja anataka kulipa akakataliwa, akawa anazungushwa tu ili achelewe baadaye awekewe gharama kubwa kwa sababu ya gari kukaa muda mrefu bandarini, ashindwe kulipa halafu lipigwe mnada, nikaja hapa nikakuta gari lake limeshaingizwa kwenye mnada nikalichomoa, akalipa alichotakiwa akaondoka na gari lake.

“Tulienda sehemu nyingine tukakuta mtu anakwambia alikuwa na gari lake katoa bandarini analisafirisha (kwenda nje ya nchi), bampa likachomoka akalichukua akaliingiza kwenye gari, wale watu wa mpakani wakamkamata eti ili athibitishe kama bampa ni la gari hilo, alipokamatwa alikaa wiki nzima,” alisema.

Alisema kutokana na mambo kama hayo, timu ya Bandari akiwemo yeye mwenyewe, walilazimika kutembea maeneo kadhaa kuchunguza changamoto na kuanza kuzitatua.

“Kwa kampeni tuliyofanya, tunaamini kwa miaka mitatu shehena ya magari itakuwa imefika 600,000,” alisema Kakoko.

Alisema pia kwa baadhi ya mawakala, wamekuwa wakisababisha baadhi ya wateja kuikimbia bandari kwa kuwawekea gharama ya juu pale wanapoagiza mizigo yao.

Kakoko alisema hata baadhi ya Watanzania walikuwa wakipitisha magari yao nchi jirani, lakini baada ya kampeni hiyo hali imebadilika na hivi karibuni, nchi hiyo ilitangaza kuwa mizigo ya Tanzania iliyokuwa ikipita huko imeshuka kwa kiasi kikubwa.

Pamoja na hayo, alisema kwa ujumla mwaka 2014/15 hadi 2018/19, shehena imekuwa ikipanda na kushuka ingawa kwa ujumla iliongezeka kwa wastani wa asilimia 2.1 kwa mwaka.

Kakoko alisema mwaka 2018/19 shehena iliyohudumiwa na bandari za TPA ilikuwa tani za uzito 17,166,079 ikilinganishwa na tani 16,197,818 zilizohudumiwa mwaka 2017/18 ikiwa ni ongezeko la tani za uzito 968,261 sawa na asilimia 6.0.

“Hiki ni kiwango cha juu kabisa kwa upande wa tani zilizowahi kufikiwa na kwa ongezeko kati ya mwaka na mwaka katika historia ya TPA,” alisema.

 Akizungumzia shehena ya kontena, alisema katika kipindi cha miaka mitano, shehena iliyohudumiwa katika Bandari ya Dar es Salaam imekuwa ikiongezeka kwa wastani wa asilimia 2.4 kwa mwaka.

“Shehena ya makasha TEUs 705,061 ilihudumiwa mwaka 2018/19 ikilinganishwa na shehena ya makasha TEUs 653,054 iliyohudumiwa mwaka 2017/18 ikiwa ni ongezeko la makasha TEUs 52,007 sawa na asilimia 8.0.

“Shehena ya kontena iliyohudumiwa katika Kitengo cha TICTS pekee katika kipindi hicho imekuwa ikiongezeka kwa wastani wa asilimia 6.8 kwa mwaka, wakati shehena ya makasha iliyohudumiwa katika Kitengo cha General Cargo katika kipindi hicho imekuwa ikipungua kwa wastani wa asilimia 10.0 kwa mwaka.

“Katika kipindi cha mwaka 2018/19 shehena ya makasha iliyohudumiwa kupitia Kitengo cha TICTS ilikuwa kontena TEUs 584,157 ikilinganishwa na makasha TEUs 535,525 yaliyohudumiwa mwaka 2017/18 ikiwa ni ongezeko la makasha TEUs 48,632 sawa na asilimia 9.1.

“Wakati shehena ya makasha iliyohudumiwa na mamlaka katika Kitengo cha General Cargo ilikuwa makasha TEUs 120,904 ikilinganishwa na makasha TEUs 117,529 yaliyohudumiwa mwaka 2017/18 ikiwa ni ongezeko la makasha TEUs 3,375 sawa na asilimia 2.9,” alisema.

Kakoko alisema kuanzia 2014/15 hadi 2018/19, shehena ya nchi jirani kupitia Bandari ya Dar es Salaam ilikuwa ikiongezeka kwa wastani wa asilimia 4.3 kwa mwaka.

 “Shehena iliongezeka kutoka tani milioni 4.694 mwaka 2014/15 hadi tani milioni 5.545 mwaka 2018/19, ikilinganishwa na tani milioni 5.244 zilizohudumiwa mwaka 2017/18, ni ongezeko la tani 300,641 sawa na asilimia 5.7,” alisema.

MAPATO YAMEONGEZEKA

Kakoko alisema pamoja na changamoto zote, mapato ya mamlaka hiyo yamekuwa yakiongezeka kila mwaka, ambapo kwa sasa yameongezeka kwa wastani wa asilimia 7.6 kwa mwaka.

Alisema kwa mwaka 2018/19 TPA ilipata ziada ya Sh bilioni 464.369 kutokana na mapato ya Sh bilioni 944.740.00 zilizokusanywa.

Akizungumzia kuhusu bandari bubu na mchakato wa kuziboresha ili ziweze kuchangia mapato ya Serikali, Kakoko alisema nchi nzima zipo 437 ambapo mamlaka hiyo imejipanga kurasimisha bandari 120.

 “Nyingine zote zitafungwa, lakini hizi 120 tutazirasimisha,” alisema.

Kakoko pia alisema katika mpango wa kuhakikisha mizigo inayopita kwenye bandari nchini inafika tani milioni 20 mwaka 2020 na tani milioni 25 mwaka 2025, wanajenga reli ya kisasa (SGR) kuingia bandarini.

Lakini pia alisema wanafanya mchakato wa kuiunganisha nchi ya Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) ambayo Bandari inaitegemea kwenye soko lake.

Alisema kwa sasa DRC inachukua asilimia 35 ya soko lake ikifuatiwa na Zambia asilimia 30, Rwanda 19, Burundi 7, Malawi 6, Uganda 3 na Comoro asilimia 1.

Kakoko alisema baada ya kuchukua hatua nyingi za kuboresha Bandari ya Dar es Salaam, ikiwa ni pamoja na kuifanyia matengenezo makubwa kwa kutekeleza miradi mbalimbali, lakini pia kuboresha mifumo ya usalama na na masoko, anaamini kutakuwa na ongezeko kubwa la biashara ndani ya nje ya nchi hadi kufikia kupakua tani milioni 18 mwaka 2020.

BANDARI YA BAGAMOYO

Kuhusu mpango wa mradi wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo, alisema bado Serikali ipo kwenye mchakato na kwamba mazungumzo yanaendelea na mwekezaji wa China ili akubali kwanza kubadili masharti 11 ambayo hayatekelezeki.

Kakoko alisema wamewaandikia barua wawekezaji hao wa China Merchant Holdings International ambaye ni mwendeshaji mkubwa kuliko wote wa bandari ya China, watafakari ili wapunguze masharti hayo.

Alisema Kituo cha Uwekezaji (TIC) kinatoa vivutio vingi kwa wawekezaji, lakini masharti ya mwekezaji wa bandari hiyo hayatekelezeki, hivyo kwa sasa wanaendelea na mazungumzo naye na ikishindikana wataangalia namna nyingine ya kutekeleza mradi huo.

“Wale walikuja na masharti, kwa mfano walitaka ardhi iwe yao kwa miaka 99, pia wakipata hasara wafidiwe, walikuwa wana masharti 11 ambayo hayawezekani.

“Kwa hiyo bado tunawasubiri, ikishindikana tutajenga wenyewe ama tutafute mwekezaji mwingine, hiyo yote ni kama ikishindikana, lakini kwa sasa bado mazungumzo yanaendelea,” alisema.

Kakoko alipinga kile alichokiita dhana kwamba kumekuwepo na mkakati wa kuiondoa bandari hiyo kwenye ramani akisema kuwa Bandari ya Dar es Salaam ni mzee na ile ya Bagamoyo ni mtoto, hivyo mzee lazima awe na mtoto na nafasi hizo haziwezi kuchukuliwa na yeyote.

Alisisitiza kuwa ujenzi wa bandari hiyo ya Bagamoyo kwenye eneo la kilomita 75 (maili 47) kaskazini mwa Dar es Salaam utatekelezwa, lakini si kwa masharti hayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles