23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

MKUCHIKA AHIMIZA UZALENDO KWA VIONGOZI, WATUMISHI

Na MWANDISHI WETU – Dar es Salaam            |               


VIONGOZI na watumishi nchini wamekumbushwa kutanguliza mbele moyo wa uzalendo na masilahi mapana ya taifa katika utekelezaji wa majukumu yao ili kupeleka mbele maendeleo ya nchi na kuimarisha usalama wa taifa.

Kauli hiyo ilitolewa jana Dar es Salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika, wakati akifunga kozi fupi ya tano kwa viongozi iliyofanyika Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC).

Mkuchika alisema ni matumaini kuwa washiriki waliohudhuria kozi hiyo, utendaji wao wa kazi utabadilika kwa kuwa na tija kwa sababu wamepatiwa mbinu zote zinazohusu namna ya kufikiri kimkakati, kufanya tathmini katika mambo mbalimbali ili kufikia uamuzi.

“Sasa mnatambua dhana ya usalama wa taifa vema na kwa mapana zaidi, si kulinda mipaka na mali za wanajamii tu, bali pia inahusisha kutunza mazingira, kuwa na chakula cha kutosha, kupiga vita rushwa na madawa ya kulevya na mengine mengi ambayo ninyi mnayafahamu zaidi,”  alisema Mkuchika.

Aliongeza kuwa usalama wa watu ni muhimu kuliko jambo jingine lolote, hivyo akasisitiza masuala ya usalama yawe ni sehemu ya kuzingatia katika utendaji wa kila siku na hasa pale uamuzi unaogusa masilahi ya nchi na jamii unapotolewa.

Alisema Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais Dk. John Magufuli imedhamiria kwa dhati kuipeleka nchi katika uchumi wa viwanda, lakini suala la rushwa limekuwa kikwazo kikubwa kufikia lengo hilo, hivyo ni jukumu la viongozi wote kutoa majawabu ya namna gani malengo yatafikiwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa NDC, Luteni Jenerali Paul Massao, aliishukuru Serikali kwa kuhakikisha viongozi na watumishi wengine wanahudhuria kozi hiyo muhimu kwa masilahi ya taifa.

Wahitimu 24 walikabidhiwa vyeti, baadhi yao wakiwa ni naibu mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa, viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama na viongozi waandamizi wa taasisi za Serikali.

Mtaala wa kozi hiyo ulilenga katika masuala yanayohusu masilahi, uzalendo na dhana nzima ya usalama wa taifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles