30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

MKOPO WA SH TRILIONI 3.3 ZA KUJENGA RELI YA SGR KUTOLEWA

 

 

NA BENNY MWAIPAJA, DAR ES SALAAM


Benki ya Standard Chartered Group imekubali kuipatia Tanzania mkopo nafuu wa dola za Marekani bilioni 1.46 (Sh trilioni 3.3) zitakazotumika kujenga kipande cha reli ya kisasa (SGR) kati ya Morogoro na Dodoma.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, baada ya kukutana na   Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Bill Winters,   Dar es Salaam jana.

Dk. Mpango aliishukuru benki hiyo kwa kukubali kugharamia ujenzi wa reli hiyo.

“Tunajenga reli hiyo ya kisasa kutoka Dar es Salaam – Morogoro hadi Makutupora (Dodoma) ambazo ni awamu mbili.

“Pia tutajenga reli hiyo kuelekea Isaka mpaka Mwanza na baadaye Rusumo ambako wenzetu wa   Rwanda tutasaidiana, wao watajenga reli hiyo kutoka Rusumo hadi Kigali,” aliongeza Dk. Mpango.

Waziri alimweleza Winters vipaumbele vikubwa vya nchi ikiwamo kuboresha Shirika la Ndege Tanzania  (ATCL) na ujenzi wa mradi mkubwa wa kufua umeme wa mto Rufiji (Stiegler’s Gorge).

“Tunaimarisha shirika letu la ndege ili kuimarisha sekta ya utalii kwa sababu tuna vivutio vingi na haipendezi wageni wanaokuja nchini wanafikia nchi jirani.

“Sasa ifike wakati tuwe na uwezo wa kuwasafirisha moja kwa moja kuja nchini kwetu,” alisema Dk. Mpango.

Alisema Tanzania ni ya pili duniani kwa kuwa na vivutio vingi vya utalii ikitanguliwa na Brazil lakini inapokea watalii wasiozidi milioni mbili kwa mwaka jambo ambalo linahitaji kufanyiwa kazi kwa haraka  sekta hiyo ichangie uchumi wa nchi kwa kiasi kikubwa kupitia fedha za kigeni.

Alisema katika kulifufua shirika hilo la ndege, tayari Serikali imenunua ndege nne ikiwamo ndege kubwa aina ya Boeing 787- 8 Dreamliner na ndege nyingine tatu zitawasili nchini Juni mwakani.

Alivitaja vipaumbele vingine kuwa ni kuboresha huduma za jamii kama vile elimu, afya, maji na kuendeleza ujuzi kwa wananchi  waweze kufanyakazi kwenye viwanda na kuwawezesha wananchi katika uchumi kwa ujumla kwa kuwa maendeleo yanahusu watu.

Naye Winters, aliipongeza Tanzania kwa kupiga hatua katika uchumi na kwamba benki yake itatoa mkopo huo.

Aliahidi atakuwa balozi wa kuelezea mafanikio ya  uchumi ya Tanzania kwa wadau wengine.

Vilevile aliahidi kuzishawishi taasisi nyingine za fedha duniani kuangalia uwezekano wa kuunga mkono jitihada hizo ambazo mwisho wake wanufaika watakuwa Watanzania kwa ujumla.

“Tuna imani kubwa na uwezo wa Tanzania pamoja na fursa nyingi za uchumi ilizonazo na  kwamba miradi mingi ya kipaumbele iliyoainishwa itafikiwa.

“Tunalo jukumu kama benki kutoa fedha na kuiweka miradi hiyo pia sokoni  iweze kupata fedha,” alisema Winters.

Winters alifuatana  na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo nchini Kenya na nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki, Lamin Manjang na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo nchini Tanzania, Sanjay Rughani.

 

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles