25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mke wa Kisena wa mwendokasi naye kortini

PATRICIA KIMELEMETA-DAR ES SALAAM

MKE wa mfanyabiashara maarufu na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka Mkoa wa Dar es Salaam (Udart), Robert Kisena, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka saba yakiwamo ya uhujumu uchumi na utakatishaji wa fedha zaidi ya Sh bilioni 2.4.

Frolencia Mashauri  ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Mafuta na Gesi ya Zenon Limited inayomilikiwa na mumewe, alikamatwa juzi jijini Dar es Salaam na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na kufikishwa mahakamani hapo jana.

Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka uliwakilishwa na mawakili Ester Martin na Fatuma Waziri huku upande wa utetezi ukiwakilishwa na Wakili Semi Malimi.

Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Augustine Rwizile, Wakili wa Serikali, Ester Martin alidai kuwa, mshtakiwa huyo akiwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Mafuta na Gesi ya Zenon Limited anadaiwa kutenda makosa hayo katika vipindi tofauti vya kuanzia mwaka 2011 hadi 2018, Mkoa wa Dar es Salaam.

Katika shtaka la kwanza, kati ya 2011 hadi 2018 katika maeneo ya Mkoa wa Dar es Salaam, anadaiwa kuratibu shughuli za kihalifu  kinyume na sheria za nchi.

Alidai kuwa, shtaka la pili linalomkabili mshtakiwa huyo ni pamoja na kudaiwa kujenga kituo cha mafuta cha Petroleum Filling Station, katika eneo la Jangwani, Ilala, jijini Dar es Salaam bila ya kuwa na kibali kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura).


Alidai kuwa, kitendo hicho alikifanya kati ya Januari 2015 hadi Desemba 31,2017, jambo ambalo ni kinyume na sheria.


Alida kuwa kati ya Januari, 2015 hadi Desemba 2017, akiwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Zenon Limited na wenzake, wanadaiwa kufanya biashara ya kuuza mafuta katika eneo lisiloruhusiwa la Jangwani Manispaa ya Ilala, Jijini Dar es Salaam kinyume na sheria ya mafuta.

Alidai kuwa kati ya Januari 25, 2015 hadi Desemba 31,2016, mshtakiwa huyo akiwa Mkurugenzi anadaiwa kuiibia Kampuni ya usafiri ya Mabasi Yaendayo Kazi Mkoa wa Dar es Salaam (Udart),  mafuta yenye thamani ya Sh bilioni 1.2.

Alidai kuwa kati ya Mei 25,,2015 hadi Desemba 31,2016, kwa lengo la kuhalalisha na kuficha uhalifu alilinganisha mafuta yenye thamani ya Sh bilioni 1.2  kwa kuuza, wakati akijua kuwa mafuta hayo ni zao la uhalifu.

Anadaiwa kuwa, kati ya Mei, 25,2015 hadi Desemba 31,2016, alimiliki kiasi cha Sh bilioni 1.2, ambacho kimetokana na fedha za zao la kosa la wizi.

Alidai kuwa, katika kipindi hicho alisababisha Kampuni ya Udart kupata hasara ya zaidi ya Sh bilioni 2.4 .

Wakili Ester alidai kuwa, upelelezi wa kesi huyo bado unaendelea na kuiomba mahakama kupanga tarehe nyingine kuwa ajili ya kutajwa.

Hata hivyo, Hakimu Rwizile alisema kuwa mshtakiwa huyo haruhusiwi kujibu lolote katika mahakama hiyo kwa sababu mashtaka yanayomkabili hayana dhamana na mahakama hiyo haina mamlaka kisheria ya kuisikiliza ambapo kesi hiyo aliiahirisha hadi  Aprili 23, mwaka huu itakapokuja kwa ajili ya kutajwa.

Awali, kabla ya kupandishwa kizimbani, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ilisema kuwa, mke wa Kisena, Frolencia, alihusika kuuza mafuta hewa kwenye Kampuni ya Usafiri wa Mabasi yaendayo Haraka Mkoa wa Dar es Salaam (Udart).

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwao, Dar es Salaam Jana, Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Takukuru, , Kassim Ephraem alisema licha ya kusajiliwa kisheria kwa ajili ya kuagiza mafuta nje ya nchi, lakini kampuni hiyo haijawahi kuagiza mafuta hayo hata mara moja, badala yake wamekua wakinunua mafuta ya rejareja kutoka kampuni za ndani za kuuza mafuta.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles