24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Mkataba wa Lugumi, polisi kitendawili

aeshyPatricia Kimelemeta na Jonas Mushi

AGIZO la Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) la kulitaka Jeshi la Polisi kuwasilisha mkataba wa Kampuni ya Lugumi Enterprises Ltd, limegeuka kitendawili baada ya watendaji wa jeshi hilo kushindwa kufanya hivyo.

Kampuni ya Lugumi inadaiwa kupewa tenda na Jeshi la Polisi kwa ajili ya kufunga mashine za kuchukua alama za vidole katika vituo 108 nchi nzima kwa gharama ya Sh bilioni 37.

Lakini hadi sasa mashine hizo zimefungwa katika vituo 14 pekee na kampuni hiyo kulipwa Sh bilioni 34 ambazo ni sawa na asilimia 99 ya fedha za makubaliano ya mkataba.

Kutokana na hali hiyo, Kamati ya PAC ambayo ilibaini kuwapo viashiria vya ufisadi katika tenda hiyo, iliwaagiza watendaji wa jeshi hilo kuwasilisha taarifa za mkataba huo pamoja na vielelezo vyake ili wajumbe waweze kuupitia pamoja na kutoa maagizo.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Aeshi Hilaly, alisema kamati yake iliwataka watendaji wa polisi kuwasilisha mkataba wa kampuni hiyo ili wajumbe waweze kupitia na kutoa maagizo.

Alisema hadi jana watendaji wa jeshi hilo waliwasilisha taarifa ya mali tu, bila ya mkataba huo jambo ambalo ni kinyume na maagizo ya kamati.

“Hadi leo (jana) sasa tisa alasiri, hatujapata mkataba wowote unaohusiana na Kampuni ya Lugumi na Jeshi la Polisi,” alisema Aeshi.

Alisema kamati hiyo inawasiliana na Katibu wa Bunge, Dk.Thomas Kashilila ili waweze kupata taarifa kama mkataba huo umewasilishwa ofisini kwake au laa.

Aeshi alisema kanuni za Bunge zinawataka watendaji wanaopewa maagizo ya kuwasilisha taarifa kwenye kamati, kuwasilisha taarifa hizo ofisi za Katibu wa Bunge.

“Kanuni za Bunge zinawataka watendaji kuwasilisha taarifa zinazohitajika kwenye kamati kwa Katibu wa Bunge, ambaye akizipata anawasiliana na katibu wa kamati husika, lakini ninavyoongea na nyinyi hapa, hatujapewa taarifa yoyote kuhusu Lugumi,” alisema.

Aeshi alisema kamati hiyo ilitoa maagizo hayo wiki iliyopita baada ya wajumbe kuona kuna utata katika mkataba wa kampuni hiyo na jeshi hilo.

Alisema walielekeleza nyaraka yoyote inayohusu kampuni hiyo na jeshi hilo inapaswa  kuwasilishwa kwenye kamati yake.

“Kama jeshi hilo halitawasilisha taarifa hiyo, kamati itaiagiza Serikali kuwachukulia hatua watendaji walioshindwa kutimiza wajibu wao.

“Hakuna cha kufichaficha hapa, ndiyo maana wajumbe wametaka mkataba huu kuwasilishwa, ikiwa Jeshi la Polisi litakaidi, tutaiandikia barua Serikali kuwachukulia hatua za kinidhamu watendaji waliokaidi agizo,” alisema Aeshi.

Alisema kutokana na hali hiyo, wajumbe wa kamati hiyo watasubiri taarifa hizo hadi leo ili ziweze kuwasilishwa, na ikiwa hazitawasilishwa watatoa tamko.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles