24.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

MKATABA EPA TUSIWEKE SAINI

  • Ni ukolonimamboleo mlango wa nyuma

Na Lilian Justice,Morogoro.

SERA ya Taifa ya uwezeshaji wa wananchi kiuchumi ulianza kabla ya uhuru  kutokana na sababu za kihistoria, wananchi hawakushiriki kikamilifu katika shughuli za uchumi, kwa kuwa walinyimwa fursa.

Hali hii ilikuwepo wakati wa ukoloni ambapo wananchi wengi waliwekewa vikwazo kushiriki katika uchumi ili watawalike kirahisi ambapo wananchi walilazimika kujishughulisha na uchumi wa sekta isiyo rasmi wakati sehemu kubwa ya sekta rasmi ilishikwa na watawala wa kikoloni na wageni.

Wakoloni walitumia mbinu mahsusi kuwaendeleza wazungu na wananchi wachache huku mbinu hizo ni pamoja na utoaji wa mikopo, utoaji wa elimu, ugawaji wa ardhi na utoaji wa leseni za biashara na baadhi ya mbinu hizo zinaweza kutumika hivi sasa kurekebisha hali hiyo na kuwawezesha wananchi kumiliki sehemu kubwa ya uchumi.

Hata hivyo baada ya Uhuru ulipopatikana mwaka wa 1961, Wananchi walipata madaraka ya kisiasa  ya bendera lakini sehemu kubwa ya uchumi bado ilibaki mikononi mwa wageni na baadhi  ndogo ya Watanzania viongozi. Hali hiyo  ilileta kero na ni mojawapo ya sababu muhimu ya kutangazwa kwa Azimio la Arusha, mwaka wa 1967 .

Azimio hilo lilikuwa  mkakati muhimu wa kuhakikisha kwamba wananchi kwa pamoja kupitia dola wanashika  na kumiliki njia kuu za uchumi.

Shughuli zote za uzalishaji na utoaji wa huduma ziliundiwa mashirika ya umma lakini hata hivyo  mashirika ya umma mengi  yaliendeshwa kwa hasara  kwa kukosa uaminifu, weledi  na ujuzi na  hivyo yaliendesha shughuli za kiuchumi kwa kutumia mtaji na ruzuku kutoka Serikalini, ikiwa ni kinyume na mategemeo ya mpango huo.

Katika kushiriki kikamilifu sasa  kwenye shughuli za uchumi, wananchi wanakabiliwa na vikwazo  sugu vifuatavyo ambavyo  ni upatikanaji wa mitaji, ukosefu wa ujuzi na uzoefu vikichochewa na upungufu katika elimu,  mafunzo, mila na desturi potofu na mtazamo  usio  sahihi wa maendeleo.

Ukosefu wa masoko ya uhakika au  uzalishaji  duni huleta  ugumu  wa uwezo wa kuingia katika masoko yenye ushindani.

Vilevile kuna ukosefu wa ushirikiano  baina ya watu  au katika  vikundi, ushirika hafifu na ukosefu wa sauti ya pamoja ya makundi mbalimbali ya wananchi katika kusimamia maslahi yao  ya Kiuchumi na  kuweza kukabili matatizo yanayowakwaza wasishiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi ndani ya sekta zao.

Uwezeshaji uchumi

Aidha, kuna vikwazo katika uchumi  vitokanavyo  na  udhaifu wa mfumo wa kodi, sheria, kanuni na leseni pamoja na huduma nyingine za Serikali kuunga uchumi huo.

Sera ya Uwezeshaji inalenga kuondoa vikwazo hivi ili kutoa nafasi nzuri zaidi kwa makundi mbalimbali kushiriki kikamilifu zaidi katika shughuli za uchumi.

Mtandao wa vikundi vya wakulima Tanzania (MVIWATA ) ambao ulisajiliwa rasmi mnamo mwaka  1995 ukiwa na lengo la kuhakikisha unawaunganisha wakulima ili kuweza kuwa na sauti moja katika kutetea maslahi  yao kama wazalishaji wakuu katika sekta ya uchumi.

Akizungumzia mtandao huo Mkurugenzi Mtendaji wa  MVIWATA Stephen Ruvuga anasema lengo la kuanzishwa mtandao huo ni kuwaunganisha wakulima wadogo nchini ambao ndio wazalishaji wakuu  na kuweza kupaza sauti  zao ili changamoto zao  serikali iweze kuzitafutia ufumbuzi ili kuleta maendeleo katika Taifa.

Ruvuga anasema kuwa bado wakulima wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ukosefu wa masoko ya uhakika wa  mazao yao, ushuru usio na tija  na mbegu feki ambazo humsababisha mkulima  hasara  na huku migogoro ya ardhi ikiwaathiri  kila kukicha .

Anasema licha wakulima kukumbwa na changamoto hizo kwa  hivi sasa wakulima wadogo nchini wanahofia endapo serikali itasaini makubaliano ya ubia wa kiuchumi ( EPA)  na Ulaya kwani hauna tija kwao na badala yake utazidi kumdidimiza zaidi.

Anaeleza kuwa  MVIWATA  umekuwa ukifuatilia  kwa karibu mchakato wa majadiliano kati ya serikali   na EU juu ya makubaliano  ya mashirikiano ya kiuchumi (EPA).

Janga la EPA

Ruvuga anaeleza kuwa tangu awali  Mviwata  imekuwa na mtazamo  kwamba misingi ya makubaliano hayo hayana maslahi kwa wazalishaji  wadogo  wa Tanzania   na uchumi kwa ujumla na hivyo kuishauri serikali  kuwa  kusaini makubaliano  hayo  ni kuweka rehani  maisha ya wakulima wa Tanzania hususani wakulima wadogo.

‘’Endapo Serikali itasaini makubaliano hayo ni kuuza maisha ya wakulima wadogo wa Tanzania ‘’anasema  Ruvuga.

Alikomelea kwa kusema  kuna athari  hasi nyingi.

‘’Kutakuwa na athari katika mfumo wa uzalishaji wa wakulima wadogo na maisha  yao kwa ujumla’’anasema Ruvuga.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa MVIWATA Veronica Sophu anasema kuwa  hofu kubwa ya wakulima   ni kuwa na uwezekano wa nchi kugeuzwa soko la bidhaa kutoka Ulaya  na hivyo kuwanufaisha  wazalishaji wa Ulaya  kuliko  wazawa.

Hata Rais wa awamu ya Tatu Benjamin Mkapa aliyaita masharti ya EPA kama ni ukoloni mambo leo na hayajabadilika kwa maana hayajali  hisia za watuwetu.

Sophu anabainisha hatari kwa serikali kupoteza mapato yake ya ushuru wa bidhaa zinazoingizwa kutokana na masharti ya makubaliano hayo.

“Endapo nchi itaingia makubaliano hayo (EPAs)  yataibana nchi kufanya biashara  ya mazao ya kilimo na mengineyo na mataifa mengine kupitia  mashirikiano mengine ya kibiashara hususani mashirikiano ya nchi za kusini kwa kusini(South-South Cooperation).

Naye Afisa Ushawishi na Utetezi  Thomas Laiser  anasema kuwa Mviwata  inampongeza  Rais Dk John Pombe Magufuli katika  kikao  cha 17 cha wakuu wa nchi za Afrika  Mashariki  kuacha kusaini makubaliano hayo  ya EPA ili  kujipa  muda wa kutafakari na kujiridhisha  iwapo kuna maslahi kwa mataifa ya Afrika Mashariki.

“Sisi kama Mviwata  tunaunga mkono  kwa asilimia mia moja msimamo huo  wa serikali  na kuiomba iufanye wa kudumu  kwa kuangalia  mazingira ya sasa na azma yake ya kujenga uchumi  wa viwanda,’’anasema Laiser

Aidha anaeleza kwa hivi sasa nchi bado inapitia kipindi cha kufungua  milango zaidi ya kiuchumi , kifedha  na kibiashara   hivyo haina budi kuangalia kwa kina  suala hili la makubaliano  ya kiuchumi .

Mhadhiri mstaafu kutoka Chuo kikuu cha Dar es Salaam  Prof Mwesiga Baregu anasema kuwa  mkataba wa EPA  sio wa kwanza nchi za Afrika  na zile za Ulaya kwani kumekuwepo na mikakati  mbalimbali hususan ule wa  mji wa Younde wa nchini Cameroon  ambao ulikuwa mwaka 1963-1975.

‘’Pia kulikuwa na mkataba wa Lome kati ya mwaka 1976-1979 na ule wa Cotoneu  wa mwaka 2000 ambao umekuja kuzaa EPA,’’anasema Prof Baregu.

Mikakati hiyo ilikuwa na vipengele  viwili  ambavyo ni kuongeza biashara kati ya nchi za Kiafrika , Caribbean  na Pasifik (ACP) ambapo nchi hizi zilikuwa makoloni  ya nchi za Ulaya.

Anasema  muda wote huo haikuleta  faida zozote  kwa wananchi  wa  ACP  na badala yake nchi hizo  zimebakia kuwa tegemezi.

Aidha anasema kuwa suala la EPA  sio  kitu  kigeni  bali kilichobadilika ni  nchi  za Ulaya badala ya  kuchukua  nchi za Afrika zote inataka mikataba  ya Kikanda  mfano  Afrika Mashariki  na Afrika   Magharibi . Mtindo  huu wa tuwa tugawe unafanywa makusudi ili kunyonya Afrika.

Anasema nchi zilizo  katika Kanda zinatakiwa kusaini   ambapo mvutano upo sehemu tatu ambazo ni wasaini au waache,  kusaini pamoja au kila mmoja asaini kivyake na pia kuendelea na mazungumzo  ili  kulinda  maslahi  binafsi  na  kusubiri mustakabali wa mbeleni wa kusaini ama kutokuusaini .

Prof Baregu anaeleza kuwa endapo Serikali  itasaini mkataba wa EPA  ni kujiwekea kitanzi  kutokana na sababu mbalimbali .

Sababu hizo ni  katika nchi za Afrika  Mashariki  mkataba  huo unataka soko huria  ili kubadili bidhaa  zinazotoka nje  ziingie  nchini bila ya kutozwa kodi  na nchi  pia ipeleke Ulaya   bila ya kutozwa kodi.

“Katika nchi  za Afrika Mashiriki,  Kenya  ni muathirika mkubwa  inapambana na kutozwa kodi kwa uchumi wake kwani uko juu  ambapo  hutegemea zao la maua kuuza  barani  Ulaya na kulipishwa kodi hivyo endapo nchi nyingine zitajiunga hawatalipa kodi, ’’anasema Prof Baregu.

Pia anasema kuwa endapo  mkataba  utasainiwa  bidhaa zote za viwanda  zilizotengenezwa nje zitaingizwa bila ya kulipilia kodi. Eneo hiloAfrika Mashariki  halina ubavu.

Hasara yazidi faida

Baregu anaeleza kuwa  endapo nchi ya Tanzania  ikijiunga  itapoteza   dola za Kimarekani Mil. 940 kwa mwaka kwenye kodi ya Mapato.

‘’Nchi nyingine  kupata  athari endapo zitasaini mkataba huo ni Uganda  ambapo italazimu  kupoteza Dola Mil. 597, Rwanda Dola Mil 241 na Burundi Dola Mil. 242 kwa mwaka,’’anasema Prof Baregu.

“Kutokana na changamoto hiyo  nchi zenye lengo la  viwanda  haiwezi  kufikia lengo kutokana na kupoteza mapato mengi ya kodi,’’anasema  Prof Baregu, na kuongezea kuwa “kutokana na changamoto hiyo watakaoathirika ni wakulima wadogo, wavuvi, wafugaji wa kuku nk.

Anabainisha kuwa  kwa upande wa Kampuni za Ulaya  kwa asilimia 90  watatuzidi  kwenye ushindani   huku nchi za kiafrika wakishinda ama kupata faida ni kwa asilimia  10% pekee.

Pia anaeleza kuwa viwanda vitakavyoathirika  ni mafuta na gesi, mafuta  ya kula, viuatilifu , mbolea , madawa  na bidhaa zinazotumika kutengeneza vitu.

‘’Kwa sababu hiyo basi hakuna sababu yoyote  ya kiuchumi, kisiasa , wala kijamii ambayo  italeta hasara endapo hautosainiwa mkataba huo wa EPA,’’anafafanua  Baregu na kuhitimisha.

Anaeleza  kuwa nchi za Afrika Mashariki  tangu mwaka 2011  waliamua  kupitia vikao vyake vya bunge la Afrika  Mashariki, Baraza  la mawaziri, wakuu wa  nchi (summit)  kuwa na mpango thabiti wa viwanda  kwa  pamoja katika Afrika Mashariki.

Anasema kuwa sera hiyo imetoka kama mchakato lakini utekelezaji wake haujaweza kufanyika  hivyo haiwezekani kuanzisha programu nyingine.

Hata hivyo Prof Baregu anasema kuwa  endapo serikali  ya Tanzania inataka kuwa nchi ya viwanda  inapaswa  kutekeleza  maazimio waliyojiwekea kama serikali   ya mwaka 2012-2032  ambao ni mkakati wa pamoja  wa viwanda Afrika  Mashariki   uweze kutekelezwa kwanza ili kuweza  kutambua  kama EPA itaweza kuwa na manufaa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Ni wakati sasa umefika kwa serikali kuwa makini katika  kusaini mkataba huo na kuamua kusimama yenyewe na kuepuka vitisho vya kukosa misaada kutoka nchi za Ulaya  na  hivyo ni vyema viongozi walioko madarakani  kutokubali  kusaini mkataba huo kutokana na visingizio fulani  na badala yake wawe waangalie athari zitakazowapata wananchi endapo serikali itajiingiza katika kuusaini mkataba huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles