23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Mkapa awapa neno wanaotaka Magufuli aongoze mihula mitatu

YOHANA PAUL – MWANZA

RAIS wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, amesema ana hakika Rais Dk. John Magufuli hatataka kuongeza mhula wa tatu wa uongozi badala yake atafuata nyayo za watangulizi wake kwa kuhudumu mihula miwili.

Alitoa kauli hiyo jijini Mwanza juzi wakati wa hafla ya utambulisho wa kitabu chake cha ‘My Life, My Purpose’ kinachoelezea maisha yake.

Mkapa alisema kazi ya urais ina changamoto nyingi na ina majaribu tofauti kutoka ndani na nje ya nchi, hivyo linapokuja suala la kukaa madarakani kwa zaidi ya mihula miwili haoni sababu ya kufanya hivyo.

Alisema anaamini kuwa hata Dk. Magufuli hawezi kuongeza muda wa kukaa madarakani kwani licha ya ugumu wa kazi hiyo pia umekuwa kama utamaduni wa taifa.

“Kuna maneno nayasikia sikia watu wanasema eti Rais Magufuli anaweza kubadili Katiba na akabakia madarakani kwa zaidi ya mihula tuliyoizoea kwa maana ya mihula miwili ya kipindi cha miaka kumi, binafsi sidhani kama hilo lipo na hata simshauri kufanya hivyo.

“Labda niwakumbushe tu, kipindi nilipokuwa madarakani kuna wakati wazee wa Zanzibar walinifuata mara kadhaa wakiniomba wao kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi wabadilishe Katiba ili wapate fursa ya kumchagua kiongozi kwa mihula mitatu kwa maana ya miaka 15, suala ambalo naweka wazi kuwa lilitaka kutikisa kidogo muungano wetu.

“Pamoja na kuniomba sana sikuwa tayari kuunga mkono suala hilo, walifanya kila liwezekanalo kunishawishi lakini niligoma na mwisho walinielewa na kuendelea na utaratibu wa kawaida wa mihula miwili ya miaka mitano kila mmoja na hadi sasa wameendelea nao.

“Ninachoweza kusema ni kwamba utaratibu huu wa mihula miwili, sasa hata Watanzania weshauzoea na umegeuka kama utamaduni wa taifa.

“Pia naweza kusema pengine umechangia kwa kiasi kikubwa kulifanya taifa letu kuendelea kuwa na demokrasia ya mfano, hivyo ninaamini hata Rais hatabadilisha Katiba kwenye hilo.

“Ndiye aliyenifuata (Rais Magafuli) akaniambia mzee tukitegemea sana hawa wahisani kasi yetu ya ujenzi wa miundombinu itakuwa ndogo sana. Kwanini sisi wenyewe hatuwezi kuwathibitishia kwamba tuko tayari ‘ku-sacrifies’ kutumia mapato yetu wenyewe kujenga barabara zetu.

“Nikamkubalia tukaenda kwenye Baraza la Mawaziri tukaamua kila mwezi tutatenga kiasi fulani cha fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara. Ni kazi ya Magufuli.

“Mimi nimeshukuru wananchi wenzangu waliona anafaa huyu, na sasa anaongoza awamu ya tano, Mwenyezi Mungu ampe afya njema aweze kukamilisha na yeye mihula miwili, nina hakika hatataka wa tatu hata kidogo kwa sababu mmeona alivyobadilika katika miaka minne hii,” alisema Mkapa.

SERA YA UBINAFSISHAJI 

Akizungumzia sera yake ya ubinafsishaji wakati wa utawala wake, alisema ingawa amekuwa akilaumiwa namna uchumi wa taifa ulivyokuwa umefikia wakati huo, hakukuwa na namna nyingine ya kulijenga taifa tofauti na kufanya ubinafsishaji.

Alisema katika kipindi hicho nchi wahisani na wafadhili walikuwa wameanza kuikimbia Tanzania kutokana na hali ya uchumi isiyoridhisha na kuwa katika hatari ya kupoteza misaada kwa kiwango kikubwa.

Mkapa alisema ili kuwaaminisha wahisani kuwa uchumi wa Tanzania unajengwa kwa kushirikisha Serikali na taasisi binafsi, ilimbidi kufanya ubinafishishaji na jambo lililowezesha taifa kuaminika.

“Jambo lingine ambalo linasemwa ni kwamba ubinafsishwaji Baba wa Taifa hakuupenda, ni kweli lakini nieleze wazi kwamba hakukuwa na ‘altenative’, mashirika haya tuliyaanzisha ili yawe ya kiuchumi kupata faida na faida hiyo iletwe serikalini tuweze kupanua huduma za jamii na miundombinu ya nchi yetu.

“Mengi badala ya kuleta faida walikuwa wanaomba ruzuku kutoka Hazina, tusingaliweza kuvumilia, ilitubidi kutafuta namna ya kuhuisha biashara hizo, viwanda hivyo na hivyo ndivyo tulivyofanya.

“Pointi yangu ni kwamba nilitaka kudhihirisha maendeleo yanaweza kusukumwa na wote sekta binafsi pamoja na Serikali. Kuna mambo ambayo sekta binafsi haiwezi kuchukua gharama zake na hayo yatabebwa na Serikali, miundombinu na kadhalika.

“Lakini kwenye elimu kwa mfano hakuna sababu ya kuzuia sekta binafsi isianzishe shule, kwa hiyo tumemsikia Profesa hapa tulianzisha vyuo vyote hivi kwa sababu tulifikiri kwa ushirikiano huo ndiyo tunaweza kueneza elimu kwa watu wengi zaidi,” alisema Mkapa.

VIONGOZI VIJANA 

Kuhusu viongozi vijana, alisema ni lazima vijana wanapotaka kuwa viongozi wasikimbilie tu kujiingiza kwenye siasa, bali wajiandae kwa kiwango cha kutosha ili wanapochukua nafasi ya kuwatumikia wananchi wawe na uwezo wa kulisaidia taifa.

 “Ninachoweza kuwashauri ni kuwa kabla ya kuchukua maamuzi ya kutaka uongozi, vijana wanatakiwa wajaribu kujiimarisha, kujifunza na kujiandaa vya kutosha na wakati ukifika basi wawashirikishe wazee waliowatangulia. Kwa kufanya hivyo, natarajia kuona viongozi wenye hekima na busara na watakuwa na maamuzi yenye tija kwa taifa,” alisema Mkapa.

Aliwaasa vijana kujenga utamaduni wa kusoma vitabu na kuachana na kutumia muda mwingi kwenye mitandano kwani maarifa ya kweli yanapatikana kwenye vitabu na ndiyo maana viongozi wengi wa zamani si tu walikuwa na weledi, bali utamaduni wa kujisomea uliwaimarisha kiakili na kuwafanya wasiwe watu wa kuyumbishwa.

Mkapa alidai kuwa amekuwa akilaumiwa kuwa yeye ni jeuri na kwamba anajiona, hivyo aliwaasa watu kusoma kitabu chake waamue kama ni kweli yeye ni jeuri.

KUANDALIWA NA NYERERE 

Kuhusu kuandaliwa na Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere kuwa rais, alisema jambo hilo si kweli licha ya watu wengi kuamini kuwa alimpigia debe tangu kwenye mchakato wa kupitishwa na chama.

“Nilichokuwa na hakika nacho katika kufanya kampeni baada ya ‘nomination’, aliniunga mkono na wengine mnajua alifanya kampeni hapa Shinyanga mpaka Tabora,” alisema Mkapa.

Pia alieleza jinsi ambavyo Mwalimu alipinga uamuzi wa timu yake ya kampeni wa kutaka wakodi helkopita ili kufanya kampeni.

“Mwalimu alipinga akisema kuwa hata kama Mungu angetuma malaika wake wawatake watumie helkopita angempinga, kwa sababu kampeni zinahitaji watu waonane, hivyo wasingeweza kutumia usafiri huo,” alisema Mkapa.

SERIKALI YA KIZAZI KIPYA 

Alisema kuwa wakati anaunda Serikali yake bungeni kulikuwa na mawaziri wakuu wawili ambao walikuwa wamechaguliwa tena kuwa wabunge ambao aliwaita kwa heshima na kuzungumza nao na kuwaeleza kuwa watamsaidia wakiwa ‘back banch’ siyo katika Serikali yake.

Alisema kuwa lengo lake lilikuwa ni kuunda Serikali yenye kizazi kipya katika siasa, mmoja wao akiwa ni Rais wa sasa Dk. Magufuli, ambaye alikiri kuwa alifanya kazi kubwa ikiwamo kutekeleza ujenzi wa daraja la kuunganisha mikoa ya Kusini katika bonde la Mto Rufiji, maarufu Daraja la Mkapa.

Mkapa alisema hata pale ambapo Dk. Magufuli alipomfuata kumtaka daraja hilo lipewe jina lake alikataa, akiamini kuwa lilipaswa kuitwa jina la Magufuli, lakini alishangazwa wakati wa kulizindua alielezwa kuwa imekwishaamriwa litaitwa kwa jina lake. 

NYAYO ZA MKAPA 

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT), Balozi Profesa Costa Mahalu, alisema kama taifa lazima viongozi wafuate nyayo za Mkapa kwani ni muwazi, mkweli na msikivu jambo ambalo viongozi wengi wa Afrika wanakosa.

Alisema iwapo wataweza kufuata nyayo hizo, taifa linaweza kuepuka migongano ya mara kwa mara kati ya viongozi wa Serikali, vyama na wananchi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, alisema uamuzi wa Rais Mkapa kuandika kitabu ni jambo la kujivunia kwa kila mwenye maono mazuri na taifa, kwani ameyafanya mawazo yake yaweze kuishi milele na kuweza kutumiwa na watu wanaotaka kuingia kwenye uongozi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles