23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Mkakati mzito Zanzibar 2015

mtanzania
mtanzania

NA MWANDISHI WETU, PEMBA

CHAMA cha Wananchi (CUF) kipo hatarini kupoteza nguvu yake visiwani Zanzibar, kutokana na kile kinachodaiwa kuwa ni mkakati hasi unaosukwa dhidi ya chama hicho kuelekea mwaka 2015, MTANZANIA linaripoti.

Mkakati huo wenye harufu ya kutaka kuua upinzani visiwani humo, unaratibiwa na kusimamiwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

Unadaiwa kutaka kupunguza majimbo matatu ya uchaguzi kisiwani Pemba kutoka 18 ya sasa hadi 15 na kuongeza mengine nane kisiwani Unguja kutoka 32 hadi 40.

Kufanikiwa kwa mpango huo, Zanzibar itakuwa na jumla ya majimbo ya uchaguzi 55, tofauti na 50 yaliyopo hivi sasa.

Baadhi ya wajumbe wa tume hiyo, wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti, Abdulhakim Ameir Issa, jana walikutana na baadhi ya wawakilishi na wabunge wa Wilaya ya Mkoani kisiwani hapa.

Taarifa kutoka ndani ya kikao hicho ambazo MTANZANIA imezipata, zinaeleza kuwa lengo la mkakati huo ni kukifanya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kiweze kupata theluthi mbili katika Baraza la Wawakilishi ili kupitisha mipango ya serikali, tofauti na sasa.

Siasa za Zanzibar zinashikwa na vyama viwili vikubwa, ambapo CUF, imekamata ngome ya Pemba na CCM imejikita Unguja.

Majimbo yanayotarajiwa kufutwa ni Mkanyageni ambalo mbunge wake ni Mohamed Habib Mnyaa, Mgogoni, ambalo mwakilishi wake ni Waziri wa Sheria na Katiba Zanzibar, Abubakar Khamis Bakary na mbunge ni Kombo Khamis Kombo.

Jimbo jingine ni Mtambwe ambalo mbunge wake ni Dk. Said Suleiman Said wote kutoka CUF.

Mtambwe ndiko anakotoka Katibu Mkuu wa CUF ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad.

Inadaiwa kuwa baada ya kufutwa, Mkanyageni litakuwa sehemu ya majimbo mawili tofauti ambayo ni Mtambile na Mkoani.

Akizungumza na MTANZANIA jana baada ya kikao hicho kumalizika, Mnyaa alisikitishwa na mkakati huo na kueleza kuwa hizo ni njama chafu zinazolenga kupunguza nguvu ya chama chake visiwani humo.

Mnyaa ambaye ni mjumbe wa Baraza Kuu na mwenyekiti wa wabunge wa CUF, alisema chama chake kina nyaraka za CCM kwenda ZEC zinazotoa maelekezo kwa tume hiyo kutekeleza mkakati huo.

“Tunazo nyaraka hizo za siri, ni mkakati uliosukwa na CCM, watu wa ZEC ni watekelezaji, hii tume haiko huru, siku zote tunasema, kwa sababu katika makamishna saba wa tume, watano wanatoka CCM na wawili CUF.

“Mkakati huu ni msukumo kutoka CCM, hili siyo siri, ushahidi mimi ninao, wao wana mapandikizi katika chama chetu na sisi tunao watu wetu kule, ndiyo maana taarifa hii si siri tena.

“Wanataka kupunguza majimbo Pemba kutoka 18 hadi 15 halafu Unguja wanaongeza kutoka majimbo 32 hadi 40, ni mkakati wa kutaka kuibeba CCM katika uchaguzi ujao 2015,” alisema.

Mnyaa alisema kwa muda mrefu tofauti ya majimbo kati ya Unguja na Pemba imekuwa ikiongezeka, lakini bado nguvu ya CUF inazidi kushamiri licha ya mikakati ya kumega ngome yake.

Kwa mujibu wa Mnyaa, mkakati huo ukifanikiwa utafanya kuwapo na tofauti ya majimbo 25 kati ya Unguja na Pemba, ambapo mwaka 1963 kulikuwa na tofauti na ya majimbo matatu tu Unguja 17 na Pemba 14, jumla 31.

“Mwaka 1995 Zanzibar ilikuwa na majimbo 50 Unguja 29 na Pemba 21 tofauti ya majimbo 8. Mwaka 2000 Unguja ikawa na majimbo 32 na Pemba 18 tofauti ya majimbo 14. Kwa mkakati huu sasa 2015 kutakuwa na tofauti ya majimbo 25, hii si sawa,” alisema.

Kwa mujibu wa viongozi wa ZEC, majimbo hayo yanafutwa kutokana na kwamba idadi ya watu haikidhi matakwa ya kisheria, kwani ni wachache.

“Wao wanasema idadi ya wananchi wa Jimbo la Mkanyageni ni 17,000 na kisheria inatakiwa jimbo liwe na wastani wa watu 20,000. Mimi nasema hizi takwimu zao ni za kupika, si za kweli.

“Kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012, watu wa Mkanyageni ni 20,614, hizo za kwao wamezitoa wapi? Si hivyo tu, kila mwaka idadi ya wananchi Wilaya ya Mkoani inaongezeka na takwimu zipo.

“Suala hili lina athari kubwa kwa wananchi endapo majimbo haya yatafutwa, unapoongeza majimbo au wilaya maana yake serikali inasogeza karibu huduma kwa wananchi.

“Jimbo moja linapata Sh. milioni 24 kutoka katika Mfuko wa Jimbo wakati kupitia mwakilishi jimbo linapata milioni 15. Maana yake ni kwamba majimbo matatu kwa fedha za mbunge ni milioni 72, za mwakilishi ni milioni 45.

“Hivyo ukifuta majimbo haya matatu tafsiri yake ni kwamba unakata mgawo wa Sh. milioni 117 Pemba, wananchi wa Pemba watakosa huduma zilizokuwa zipatikane kwa fedha hizi,” alisema.

Makamu Mwenyekiti wa ZEC, Abdulhakim Ameir Issa, alipohojiwa alikanusha mpango wa tume yake kutaka kufuta na kuongeza majimbo visiwani humo.

“Taarifa hizi sio sahihi, tupo Pemba kwa ajili ya kupokea maoni tu juu ya uchunguzi wa idadi ya watu, majina na kuhakiki mipaka ya majimbo,” alisema kwa kifupi.

Mwandishi alipotaka ufafanuzi mipaka ya majimbo ya sasa ina kasoro gani hadi ihakikiwe upya alijibu: “Ndiyo tunawasikiliza wananchi. Kuna wadi zilizoingiliana, ni kubwa sana, nyingine mipaka yake inaleta ugumu kiutendaji. Hivyo wananchi wanapendekeza namna ya kuondoa matatizo hayo.

“Kazi hii ilianza kwa vyama vya siasa na taasisi za serikali. Sasa hivi tupo wilayani tunazungumza na wabunge, wawakilishi, madiwani, asasi za kiraia pamoja na wa kila wilaya.”

Kutokana na mvutano huo, MTANZANIA ilimtafuta Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Vuai Ali Vuai kutaka kuzungumzia suala hilo, lakini jitihada hizo hazikufanikiwa kutokana na kiongozi huyo kutopokea simu.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles