31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Mjue Nduda mwenye sura mbili

Na Sosthenes Nyoni-Dar es Salaam


UTAKUWA sahihi kabisa kama ukisema ni mtu mwenye bahati nzuri, lakini pia hautakosea kama utasema ana bahati mbaya.

Ninayemzungumzia hapa ni kipa mkongwe nchini, Said Mohamed, ambaye pia ni  maarufu miongoni mwa wadau wa soka kwa jina la Nduda.

Kipa huyu ambaye kwa sasa anaidakia timu ya Simba, maisha yake ya soka yamejikita katika sura mbili, moja ikiwa ni shujaa na nyingine mnyonge.

Ushujaa wake unatokana na mara kadhaa kupata kuwa kipa bora wa mashindano na kumjengea heshima miongoni mwa wadau wa soka, lakini ile ya unyonge inatokana na kusajiliwa kwa kishindo na timu tofauti tofauti na mwisho wa siku huishia kusugua benchi.

Haya yamekuwa maisha ya kawaida kabisa  kwa Nduda.

Umaarufu wake ulipoanzia

Nduda alianza kujenga jina lake miongoni mwa wadau wa mchezo wa soka hapa nchini akiwa na kikosi cha timu ya Majimaji yenye maskani yake mjini Songea.

Akiidakiwa Majimaji, kipa huyu alikuwa nguzo  muhimu katika timu hiyo kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuokoa michomo ya washambuliaji wa timu pinzani.

Lakini alitambulika hasa kutokana na kuwa kikwazo kwa timu kongwe nchini za Simba na Yanga zilipokuwa zikikutana na Majimaji.

Na hili ndilo lililoishawishi Yanga kubisha hodi katika klabu ya Majimaji na kueleza bayana nia yake ya kumsajili na hatimaye kufanikiwa kumpeleka Jangwani.

Kila mwana Yanga kwa wakati ule alifurahia ujio wa Nduda katika klabu yao, akiamini kwamba atalifanya lango lao kuwa gumu zaidi, hatua ambayo itawasaidia kupata matokeo mazuri dhidi ya wapinzani wao katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

Lakini tofauti na matarajio, Nduda aligeuka mtalii ndani ya Klabu ya Yanga kutokana na kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara, hivyo mara nyingi kujikuta akiwa benchi.

Kikwazo kikubwa kwa kipa huyo baada ya kusajiliwa Yanga kilikuwa makipa wengine aliokutana nao katika kikosi hicho, nao ni Yaw Berko na Juma Kaseja.

Berko na Kaseja walifanya nafasi ya Nduda kupenya hadi kusimama kwenye milingoti mitatu ya Yanga kuwa migumu kweli kweli.

Hakika kutokana na ushindani huu alioukuta pale Yanga, maisha ya Nduda yaligeuka na kuwa magumu.

Nduda alijikuta katika hali ngumu zaidi baada ya Yanga kulazwa mabao 5-0 na Simba katika mchezo wa Ligi Kuu msimu wa 2011-2012, huku mabao matatu kati ya matano akifunga yeye.

Ilivyokuwa siku hiyo; Yanga iliingia uwanjani kuikabili Simba, huku langoni mwake akiwa Berko ambaye hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika aliruhusu mabao mawili.

Kipindi cha pili, Berko aligoma kuingia uwanjani kwa madai kwamba alipata majeraha, hatua iliyompa fursa Nduda kuchukua nafasi yake.

Nduda alidaka dakika 45 zote za kipindi cha pili na kuruhusu wavu wake kutikiswa mara tatu.

Baada ya kujitafakari kwa kina hali yake ndani ya Yanga, Nduda aliomba kuondoka kwa mkopo, kwakua mkataba wake na miaka hiyo ya Jangwani ulikuwa bado  haujamalizika.

Kitu kizuri ni kwamba uongozi wa Yanga ulikubaliana na ombi lake na kumtoa kwa mkopo katika klabu ya Mtibwa Sugar ya mkoani Morogoro.

Baada ya kutua Mtibwa, Nduda aligeuka na kuwa lulu, kwani uwezo wake ulimfanya aaminiwe na kupewa heshima ya kuwa kipa namba moja.

Mafanikio aliyoyapata akiwa na Mtibwa ni pamoja na kuiwezesha timu hiyo kutwaa ubingwa wa Kombe la Mapinduzi, michuano inayofanyika kila mwaka visiwani Zanzibar.

Mbali ya kuiwezesha Mtibwa kutwaa taji la Mapinduzi, yeye binafsi aliibuka kipa bora wa michuano. Hili lilimjengea heshima kubwa katika soka la Tanzania.

Kiwango cha Nduda kilimshawishi aliyekuwa kocha wa timu ya Taifa, Taifa Stars, Salum Mayanga, kumjumuisha katika kikosi  kilichoshiriki michuano ya Baraza la Vyama vya Soka kwa Nchi za Kusini mwa Afrika (Cosafa), iliyofanyika nchini Afrika Kusini mwaka 2017.

Katika michuano hiyo, Taifa Stars ilikamata nafasi ya tatu, huku Nduda akiibuka kipa bora wa mashindano.

Kilichowashangaza wadau wengi wa soka ni hatua ya kipa huyu kunyakua tuzo hiyo, licha ya kucheza mchezo mmoja pekee wa mashindano hayo.

Mambo yalizidi kumnyookea Nduda, kwani baada ya kurejea nchini Simba  haikuchelewa ikamsajili kwa mkataba wa miaka miwili.

Ni katika kipindi hicho hicho, Simba ilimsajili  Aishi Manula  kutoka Azam FC.

Baada ya kusajiliwa Simba, Nduda hakuweza kukaa langoni kwa kipindi kirefu kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya goti, hatua iliyoifanya klabu hiyo kumpeleka Afrika Kusini kwa ajili ya matibabu.

Huko Afrika Kusini alifanyiwa upasuaji na kutakiwa kupumzika kiasi cha kutosha, kabla ya kurejea uwanjani.

Baada ya kuwa nje ya uwanja kwa kipindi kirefu, Nduda alirejea kikosini, lakini akakutana na changamoto ya ushindani kati yake na Manula, kabla ya klabu hiyo kumsajili kipa mwingine mzoefu, Deogratias Munishi ‘Dida’.

Uwapo wa Manula na Munishi umezidi kuyafanya majaliwa ya Nduda kuwa magumu zaidi, kwani tangu  Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu ilipoanza hajaidakia Simba mchezo wowote.

Zipo fununu kwamba kuna uwezekano klabu ya Simba ikamtoa kwa mkopo kipa huyo wakati huu wa usajili wa usajili wa dirisha dogo. Huyu ndiye Nduda, ambaye maisha yake ya soka yana sura mbili, moja ikiwa ya ushujaa na nyingine unyonge.

 

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles