24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mjamzito alivyojitoboa tumbo na kutoa mtoto

Na MWANDISHI WETU

-RUKWA

MGANGA Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Dk. Boniface Kasululu, ameeleza chanzo cha tukio la mwanamke Joyce Kalinda (32), anayedaiwa kujichana tumbo na kitu chenye ncha kali na kutoa mtoto.

Hatua hiyo ilitokana na hoja iliyotolewa bungeni na Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy (CCM), kudai kuwa mwanamke huyo amejichana tumbo kwa wembe kutokana na kukosa huduma kwa wakati huku akitaka hatua za Serikali katika suala hili.

Joyce ambaye alikuwa mjamzito, alijichana tumboni na kumtoa mtoto akiwa hai, akapelekwa katika Kituo cha Afya Kirando, na baadaye kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Rukwa kwa uangalizi wa karibu.

Katika taarifa yake, Dk. Kasululu alisema baada ya tukio hilo timu ya wataalamu wa afya iliyoundwa kufuatilia tukio hilo, ilibaini kuwa Mei 30, mwaka huu saa 9:30 usiku, Joyce akiwa na ndugu zake wawili (wifi na shangazi yake), walipokewa katika Kituo cha Afya Kirando kilichopo katika Kata ya Kirando, Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi kwa ajili ya kujifungua.

Alisema Joyce, alipokewa na kufanyiwa uchunguzi wa awali, ambapo ilibainika alikuwa na ujauzito unaokadiriwa kuwa na miezi tisa, akiwa na dalili za uchungu katika hali ya kawaida ya kiafya.

“Baada ya uchunguzi wa awali kukamilika, alipelekwa katika wodi ya wazazi wanaosubiri kujifungua kwa ajili ya kupumzika, huku watoa huduma wakiendelea kutoa huduma kwa wagonjwa wengine.

“Katika ujauzito huu, alikuwa akihudhuria kliniki ya afya ya mama na mtoto katika Kituo cha Afya Kirando ambako alifanikiwa kufanya mahudhurio matatu na hudhurio la mwisho likiwa ni Mei 8, mwaka huu.

“Mnamo saa 10:30 alfajiri wakati watoa huduma wakifuatilia kujua maendeleo yake ndipo walipobaini kuwa Joyce hakuwepo ndani ya wodi na hivyo kuanza kumtafuta katika maeneo mbalimbali na kutoa taarifa kwa mlinzi na uongozi wa kituo hicho cha afya.

“Wakati juhudi za kumtafuta zikiendelea, majira ya saa 12:30 asubuhi, Joyce aliletwa kituoni akiwa amebebwa kwenye godoro na watu watatu (mmojawapo akiwa ni mwenyekiti wa Kijiji cha Kamwanda) huku akivuja damu nyingi.

“Watoa huduma walimpokea mgonjwa na kumuona akiwa ametapakaa damu, mtoto akiwa nje ya tumbo.

“Baada ya kumchunguza,  Joyce alibainika kuwa na jeraha lililosababishwa na kitu chenye ncha kali tumboni huku sehemu ya utumbo, mfuko wa uzazi, kondo la nyuma na mtoto vikiwa nje na yeye mwenyewe akiwa hajitambui. 

“Baada ya hapo timu ya kituo cha afya ikiongozwa na Mganga Mfawidhi, Dk. Gideon Msaki iliendelea na huduma za upasuaji wa dharura kwa ajili ya kuokoa maisha ya Joyce.

“Baada ya huduma za upasuaji wa dharura kufanyika, timu ya ufuatiliaji iliendelea na ufuatiliaji zaidi wa tukio hili na kubaini kuwa Joyce alipotoka kituo cha afya alirudi nyumbani kwake anakoishi yeye, mtoto wake wa kiume aitwaye Linus Sindani anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 12 au 13 na mume wake ambaye siku ya tukio hakuwepo nyumbani.

“Mara baada ya kurudi nyumbani, Joyce alimwagiza mwanaye (Linus) kwenda kumwita shangazi yake ambaye anaishi maeneo ya jirani na nyumbani kwao. 

“Waliporudi wakiwa na shangazi ndipo walipomkuta Joyce akiwa ameloa damu na hivyo kutoa taarifa kwa majirani na mwenyekiti wa kijiji kwa ajili ya msaada zaidi,” alisema Dk. Kasululu.

Kutokana na hali hiyo, alisema timu ya ufuatiliaji imejiridhisha kuwa huduma za dharura za upasuaji wa kuokoa maisha ya Joyce zimefanyika kwa mafanikio makubwa katika Kituo cha Afya Kirando na kwamba mama na mtoto ambao kwa sasa wamehamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa kwa uangalizi zaidi wanaendelea vizuri.

“Tunatoa pongezi kubwa kwa watumishi wa Kituo cha Afya Kirando kwa juhudi kubwa walizofanya kuokoa maisha ya Joyce Kalinda. Tukio hili limeripotiwa katika Jeshi la Polisi kwa ajili ya kuendelea na uchunguzi zaidi,” alisema Dk. Kasululu.

KAULI YA MBUNGE

Akizungumzia tukio hilo, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Keissy, alisema baada ya kuzungumza na mwanamke huyo, alimweleza kuwa aliamua kuchukua uamuzi huo baada ya madaktari kumwambia asubiri.

“Joyce mwenyewe anasema alihisi kuna kiumbe alimjia akaondoka naye mpaka nyumbani kwake na akaona yeye mwenyewe akichukua wembe akijichana tumbo akapoteza fahamu, alipozinduka akasikia sauti ya mtoto,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles