25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Mjadala kura ya maoni yawaibua Raila, Ruto

NA ISIJI DOMINIC

KUNA kila dalili Wakenya wakapiga kura ya maoni kubadilisha Katiba ambayo imebakisha miaka miwili kutimiza miaka 10 tangu kupitishwa. Endapo zoezi hilo litafanyika, hii itakuwa mara ya tatu Katiba inabadilishwa.

Mara ya kwanza Katiba kubadilishwa ilikuwa 1969 ikiwa ni miaka sita tangu Kenya kupata uhuru na 2010, Wakenya wakabadilisha tena Katiba lakini baada ya kushuhudia machafuko ya kisiasa kufuatia Uchaguzi Mkuu wa 2007.

Kinara wa upinzani kupitia Muungano wa NASA ambaye pia ni kiongozi wa chama cha ODM, Raila Odinga, amekuwa katika mstari wa mbele kushinikiza kura ya maoni kufanyika huku Naibu Rais William Ruto kabla ya hivi karibuni kubadili mawazo alikuwa anapinga Katiba kubadilishwa.

Rais Uhuru Kenyatta naye hajaweka wazi yupo upande gani na badala yake amewataka viongozi kuacha kupiga siasa akisisitiza huu ni muda wa kuwatumikia wananchi ikiwamo kutekeleza ajenda nne kuu.

Hivi karibuni akiwa katika Kaunti ya Migori kumnadi mgombea wa ODM, Ochillo Ayacko anayewania  kiti cha useneta kwenye uchaguzi mdogo kufuatia kifo cha Ben Oluoch Okello, Raila alisema mabadiliko yanayotarajiwa baada ya kura ya maoni itakuwa ya manufaa kwa Wakenya.

Raila ambaye ni Waziri Mkuu wa zamani alikutana na Rais Uhuru Machi 9, mwaka huu na kwa pamoja wakakubaliana kufanya kazi. Wawili hao waliunda kamati ya watu 14 watakaochukua maoni ya wananchi yenye nia ya kuboresha maisha ya Mkenya wa kawaida.

Wajumbe wa kamati hiyo ni Agnes Kavindu, Senata Amos Wako, Profesa Adams Oloo, Florence Omose, Saeed Mwanguni, James Matundura na Meja Mstaafu John Seii.

Wengine ni Askofu Lawi Imathiu, Maison Leshomo, Senata Yusuf Haji, Morompi ole Ronkai, Bishop Peter Njenga, Rose Moseu na Askofu Mkuu Zecheus Okoth huku makatibu ni Balozi Martin Kimani na Paul Mwangi.

Ni takribani miezi saba tangu kamati hii iundwe na bado hawajatoa mapendekezo lakini Raila amedokeza kura ya maoni ni moja ya vitu vilivyokubaliwa na kinachosubiriwa ni mwitikio wa Wakenya.

Maswali ya kujiuliza, kwanini Raila anataka kura ya maoni kubadilisha Katiba? Kwanini Ruto ambaye sasa amelegeza msimamo wake alikuwa anapinga vikali Katiba kubadilishwa? Je, wote katika maamuzi yao wanaangalia maslahi ya Wakenya?

Awali Ruto na kundi lake walidai kufanyika kwa kura ya maoni kutahitajika kutumika fedha nyingi wakati Raila na kundi lake wanadai Katiba ya sasa ni mzigo kwa wananchi. Hata hivyo wanaopinga kufanyika kura ya maoni wanashikilia msimamo wao kwamba wenzao wanaoutaka ni kwa ajili ya manufaa yao ya kujipatia vyeo serikalini.

Tayari aliyekuwa mgombea urais katika uchaguzi mkuu uliopita Ekuru Aukot kupitia chama chake cha Thirdway Alliance ameshaanza mchakato wa kukusanya kura milioni moja kushinikiza kura ya maoni.

Akitumia kampeni aliyoipachika jina ‘Punguza Mzigo’, Aukot anakusudia kumpunguzia mwananchi kodi kubwa anayotozwa katika kuhakikisha idadi ya wabunge inapunguzwa kutoka ilivyo sasa ya 416 hadi 194.

“Lengo letu ni kuifanya (kura ya maoni) kabla ya 2022. Tunakusanya saini za Wakenya ambao wameonesha kuchoka ili mwakani twende kwenye kura za maoni,” alisema baada ya hivi karibuni kufanya mkutano na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), Wafula Chebukati.

Viongozi wa dini nao pia hawajaachwa nyuma katika kupaza sauti kuwepo kwa kura ya maoni itakayopelekea kubadilishwa kwa Katiba iliyopitishwa Agosti 27, 2010 baada ya Kenya kugubikw na machafuko ya siasa kufuatia uchaguzi mkuu wa 2007.

Tayari viongozi wa dini na baadhi ya wabunge wameshawasilisha maombi katika Bunge la Taifa wakishinikiza Katiba kubadilishwa. Miongoni mwa mapendekezo yaliyowasilishwa na Mbunge wa West Mugirango Vincent Mogaka na mwenzake wa Ndia George Kariuki wanataka idadi ya mawaziri ipunguzwe kutoka 22 ilivyo sasa hadi 12 na kaunti zipunguzwe kutoka 47 hadi 12.

Naye mbunge wa Tiaty, William Kamket, anapendekeza nafasi ya waziri mkuu mwenye mamlaka na kiongozi wa serikali, kufutwa kwa nafasi ya naibu rais na kubuni nafasi ya manaibu wawili wa waziri mkuu. Aidha mapendekezo ya Kamket ambaye alichaguliwa kupitia tiketi ya KANU anataka rais anayechaguliwa kukaa madarakani kwa miaka saba tu – tofauti na mihula miwili ya miaka mitano – na jukumu lake liwe kusimamia sherehe za kitaifa.

Mbunge mwingine aliyewasilisha mapendekezo yake ni Caleb Kositany wa Soy anayetaka nafasi za seneta, wabunge wa kuteuliwa na wajumbe wa baraza la kaunti kufutwa akidai ni chanzo ya ongezeko la matumizi ya serikali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles