23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

MIZOZO, MAPIGANO YATATIZA UKUAJI WA KILIMO AFRIKA

UMOJA wa Mataifa (UN) umezitaka nchi za Afrika kukabili  mizozo na mabadiliko ya tabia nchi ili kushinda vita dhidi ya baa la njaa, ukisema ni suala lililo ndani ya uwezo wa Bara hili kulitatua.

Kwenye mkutano wa siku mbili wa Umoja wa Afrika (AU), uliomalizika mapema wiki hii mjini Addis Ababa Ethiopia, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alitoa mwito kwa Bara la Afrika kuimarisha amani kama njia muhimu ya kustawisha kilimo.

Pembezoni mwa mkutano wa 30 wa AU, viongozi na wadau wa kilimo na chakula pamoja na maafisa wa UN walikutana kujadili jinsi ya kuondoa njaa barani Afrika.

Mkutano wao unafanyika miaka mitano baada ya Umoja wa Afrika kutoa azimio la kukomesha njaa barani humu ifikapo mwaka 2025.

Ingawaje, huku ikisalia miaka minane tu kabla ya kufanikisha azimio hilo la mwaka 2013, Afrika bado inaendelea kukabiliwa na uhaba wa chakula kutokana mabadiliko ya hali ya hewa, mizozo ya kisiasa na umaskini.

“Kilimo na uzalishaji wa mifugo barani Afrika unakabiliwa na hatari, hasa kutokana na mapigano na mabadiliko ya tabianchi, ukosefu wa chakula na umaskini zinahusiana kwa karibu,” Guterres anasema na kuongeza:

“Ni muhimu kuangazia kwamba wengi wa watu wanaokosa chakula barani Afrika wako katika nchi zinazokumbwa na migogoro.

“Kuwa na kilimo shirikishi na endelevu ni muhimu katika kufikia malengo mawili ya kwanza ya maendeleo endelevu ya kuangamiza njaa na umaskini, pia kusongesha mbele malengo mengine.”

Kujitolea kikamilifu kwa serikali za Afrika na Umoja wa Afrika kunahitajika ili kuendeleza amani, haki za kibinadamu maendeleo endelevu kama njia mojawapo ya kupambana na njaa.

Takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) zinaonyesha kuwa katika kanda ya Afrika Mashariki pekee nchi za Sudan Kusini, Kenya, Ethiopia na Somalia watu milioni 28 wanahitaji misaada ya chakula.

Kulingana na takwimu hizo za mwaka 2017, zaidi ya watoto milioni moja wanakabiliwa na utapiamlo hali inayotia hofu.

FAO inaripoti kwamba watu wanaokosa chakula cha kutosha duniani waliongezeka kwa asilimia 30 kati ya mwaka 1990 na 2016, hali ikiwa mbaya zaidi katika kanda ya Sahel na pembe ya Afrika.

Lakini hata hivyo nchi za Afrika zimeendelea kuongeza uwekezaji kwenye kilimo na hivyo kupunguza idadi ya watu wasio na chakula.

Kwa mfano nchini Ethiopia Serikali imeongeza bajeti yake kwa wizara ya kilimo na kuboresha sera za sekta hiyo ili kuongeza uzalishaji.

Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mpango wa Kina wa Maendeleo ya Kilimo barani Afrika (CAADP) anasema: “Kwa wastani kilimo na sekta husika, vimekuwa na ukuaji wa asilimia 10 kwa mwaka kwa kipindi cha miaka 15 iliyopita. Tumekuwa tukitenga zaidi ya asilimia 10 ya bajeti ya taifa kwa sekta ya kilimo.

“Hayo ni zaidi ya malengo yaliyowekwa na mpango wa kina wa maendeleo ya kilimo barani Afrika (CAADP), pia tulianzisha mpango wa kufanya kilimo biashara ambao umesaidia kuendesha kilimo cha kisasa kwa njia ya mashine.”

Nchi nyingi barani Afrika hutegemea kilimo kama njia kuu ya kuendeleza uchumi. Lakini kutokana na changamoto zinazoathiri uzalishaji endelevu kama kupungua kwa mvua na ukosefu wa mtaji wa kutosha sekta hiyo bado haijakua kikamilifu.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kilimo na Chakula Duniani (FAO), Jose Graziano da Silva anasema hatua mpya za shirika hilo zitasaidia Afrika kupiga hatua za kuelekea kujitosheleza na chakula.

“Uwekezaji katika sekta ya kilimo unasalia kuwa njia bora zaidi ya kuwezesha familia kuwa na mapato pamoja na lishe bora barani Afrika. Naridhika kusema kwamba tunaingia awamu mpya yenye matumaini ya kuwa na hatua kuwa na hatua bora sekta ya kilimo mwaka huu wa 2018,” anasema.

Umoja wa mataifa unapendekeza kuwa serikali za Afrika zitenge angalau asilimia 10 ya bajeti yake ya taifa kwa sekta ya kilimo.

Malengo muhimu ya Umoja huo ni kuwa na dunia yenye chakula cha kutosha ifikapo mwaka 2030.

Hilo limekuja huku kukiwapo mwito wa mataifa ya Afrika kutumia mbinu za kisasa za kilimo kutokana na umuhimu wa sekta hiyo kwa maendeleo ya bara hili.

Mkutano wa 24 wa jukwaa la ushirikiano kati ya Ujerumani na Afrika kuhusu kilimo cha biashara umefanyika mjini Berlin, Ujerumani mapema wiki iliyopita, ambapo Naibu Waziri Mkuu wa Uganda Jenerali Mstaafu Moses Ali alihimiza matumizi ya teknolojia.

Jenerali Ali anasema ili kuwapo kwa ustawi wa kilimo Afrika ni sharti wakulima waanze kutumia mbinu za kisasa na teknolojia katika shughuli zao za ukulima.

Anasema Afrika ina utajiri wa kutosha wa rasilimali za kilimo kwa hiyo inahitaji washirika wazuri tu watakaosaidia katika masuala ya kupenyeza teknolojia katika kilimo barani humo kwa kuwa ndiyo uti wa mgongo wa idadi kubwa ya nchi za Afrika.

Amezungumzia pia suala la ubora wa bidhaa kutoka Afrika akisema nchi nyingi za Afrika hazina teknolojia ya kutathmini ubora wa bidhaa za kilimo au hata kama ipo basi si ya kisasa.

“Teknolojia inaweza kusaidia, kwanza kuwapunguzia wakulima mzigo wa kutumia jembe, mtu anatumia jembe kwa kulimia chakula cha familia yake, na wengine hata kwa kuuzia nchi nzima. Hilo hata haliwezekani.

Katika ulimwenguni wa sasa, kilimo kinafanywa kwa mbinu za kisayansi, ambazo nafikiri iwapo hata sisi tutazifuata, tutakuwa kama wao, au hata kuwapita baadhi yao,” anasema Jenerali Ali katika mahojiano mjini Berlin.

Waziri wa Kilimo wa Ujerumani Dk. Herman Onko Aeikens anasema Ujerumani iko tayari kuisaidia Afrika kwa kuwa mustakabali wa bara hilo unategemea maendeleo katika kilimo.

Dk. Herman ameonya Afrika ni sharti ichukue jukumu kama bara na kwamba Ujerumani italiunga mkono katika masuala kadhaa kama ufadhili na teknolojia, akisema ustawi na ufanisi wa kilimo unawategemea Waafrika wenyewe.

Waziri huyo pia ameelezea matumaini ya Afrika kupiga hatua katika kukabiliana na ufisadi pamoja na migogoro ambayo imeathiri sekta ya kilimo pia.

Amezungumzia hatua ya viongozi wa nchi mbalimbali Afrika kupitia Umoja wa Afrika, kujitolea katika kukabiliana na ufisadi katika nchi zao akisema hiyo ni hatua itakayosaidia siyo kilimo tu bali hata uchumi wa Afrika.

Mwisho

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles