27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

Mitazamo hasi ya jamii inawaumiza wauguzi hospitalini

 AVELINE KITOMARY 

UUGUZI ni taaluma ambayo inahitaji watu wenye moyo wa huruma. Hii ni kwa sababu kazi wanayokwenda kuifanya baada ya kuhitimu ni kubwa na inataka moyo wa ziada kuitekeleza. 

Miaka ya nyuma, taaluma hii ilionekana ni ya watu waliofeli masomo yao ya kidato cha nne, na hivyo hutafuta fani ambazo zinaweza kuwafanya wakapata kazi ya kujiongezea angalau kipato na kujikimu kimaisha. 

Ukichunguza kwa makini, utabaini kuwa wauguzi wengi ni wale ambao wamehitimu kidato cha nne na au darasa la saba. 

Hata hivyo, sasa hivi kiwango cha madaraja ya elimu kwa wauguzi imeongezeka, wapo ambao wana shahada ya kwanza hadi ya tatu (PHD). Kutokana na hali hiyo, weledi na ujuzi wa wauguzi umeongezeka mara dufu zaidi ambapo sasa wana nafasi kubwa ya kuhudumia jamii kulingana na mfumo wa maisha uliopo. 

Hadi sasa, Tanzania ina zaidi ya wauguzi 30,451 katika vituo vya umma na binafsi nchini, ambapo asilimia 80 ya huduma za afya katika vituo vya kutoa huduma za afya zinatolewa na wauguzi. 

Licha ya kwamba taaluma ya uuguzi inanafasi kubwa zaidi ya kutoa huduma wakati mwingine wauguzi wamekuwa wakinyooshewa vidole na jamii kwa mtazamo hasi. 

Dhana na taswira mbalimbali zilizojengeka katika jamii kuhusu wauguzi inasababishwa na wale wachache tu ambao wanakiuka maadili ya kazi yao. 

Ukiukwaji wa maadali ya kazi kwa baadhi ya wauguzi imewafanya jamii kila kukicha kutoa maneno yasiyofaa kuhusu taaluma hiyo. 

Licha ya kuwapo kwa mitazamo tofauti kwa jamii, ukweli ni kwamba wapo wauguzi wanaozingatia weledi na maadili ya kazi zao. Sophia Sanga, ni Ofisa Muuguzi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, kitengo cha afya na magonjwa ya akili. 

Kwa takribani miaka nane sasa amekuwa akifanya kazi ya kuwahudumia wagonjwa wakiwamo wenye magonjwa ya afya ya akili. 

Sanga anasema tangu utoto wake alikuwa akitamani siku moja kuwa muuguzi ili ahudumie wagonjwa kwa upendo. 

Hivi sasa malengo yake yametimia lakini bado kunachangamoto zinazomsibu katika taaluma hiyo. 

Licha ya kuwa mstari wa mbele katika kufata maadili ya taaluma ya uuguzi lakini mambo kadhaa kutoka kwa jamii yamekuwa yakiuumiza moyo wake. 

Anasema: “Nikiwa na miaka mitano kwenye kazi yangu nilikutana na changamoto ambayo sitakaa niisahau, ni baada ya jamii kuzungumzia uuguzi vibaya hicho kiliniumiza kwa sababu nilisikia kwa masikio yangu. 

“Siku hiyo nilienda msibani baada ya jirani yangu kufariki, nikakuta wanafamilia wamekaa lakini watu bado hawajakusanyika na walipokuwa wanazungumza walikuwa wanaelezea jinsi walivyokuwa wanaamini kuwa yule aliyefariki aliuawa na muuguzi. 

“Walikuwa wakielezea kwa lugha ya asili ya kwao ambayo naielewa, wakajaribu kukumbuka hata mgonjwa mwingine aliyekuwa amelala kitanda cha pili kuwa alichomwa sindano ya sumu na wauguzi akafa.” 

Kutokana na hali hiyo, anasema alishindwa kabisa kuvumilia maneno hayo akaamua kuondoka eneo la msiba. 

“Moyo wangu ulitaka kupasuka kwa maumivu, kwa sababu najua muuguzi hayupo kwaajili ya kazi hiyo na hawezi kufanya hicho kitu. Mbaya zaidi hao wauguzi nawafahamu na niliwahi kuwa na mgonjwa aliyehudumiwa na hao wauguzi,” anasema. 

Anasema mtazamo wa jamii kuwachukulia wauguzi kama wauaji inamtesa hasa ukizingatia yeye ni muuguzi anayefuata maadili ya taaluma yake. 

 “Binafsi ninatumia taaluma yangu vizuri ikiwamo mchakato wa kiuguzi katika kumhudumia mgonjwa kuhakikisha anakuwa salama na kufuata wajibu wangu. 

“Pia katika maadili tunajifunza kuthamini utu wa mgonjwa, kumhudumia mgonjwa kwa kumjali na kuamini kuwa yeye ni wa thamani anapokuja mikononi mwangu yuko salama zaidi,” anabainisha Sanga. 

Muuguzi huyo anataja changamoto nyingine kuwa ni kushindwa kuelewana na baadhi ya ndugu wa wagonjwa kutokana na sababu mbalimbali. 

“Kuna mazingira yasiyo salama kutokana na asili ya kazi, lakini pia upungufu wa vifaa tiba kwa kipindi cha nyuma ilikuwa ni shida, tunashukuru sasa hivi angalau hali imekuwa si mbaya. 

“Changamoto nyingine ni 

 kwamba wakati mwingine utakuta mimi niko sahihi na nimefika kwa wakati lakini daktari hajafika, sasa unakuta wagonjwa wanaona kama unawachelewesha kupata huduma,” anaeleza Sanga. 

Baadhi ya watu huamini kufanya kazi kwa muda mrefu na mazingira magumu husababisha wauguzi kuwa na tabia za kikatili. 

Kuhusu suala hilo Sanga anaamini kuwa mazingira magumu hayawezi kuchangia kuvunja maadili ya kazi. 

“Siamini kuwa kipato kidogo na mazingira ya kazi kuwa magumu inaweza kusababisha muuguzi kutoa lugha chafu kwa wagonjwa, nadhani hiyo ni tabia ya mtu. 

“Tunajitahidi kuelimishana katika vitengo vyetu na kliniki zetu, tunawaambia wagonjwa sisi ni nani na wanatakiwa kupata huduma nzuri kutoka kwetu. 

“Muuguzi ni mtu wa karibu zaidi na mgonjwa, anajua unavyopumua, jasho linavyomtoka, anajua iwapo mgonjwa ananjaa, hata akishindwa kula muuguzi ananawa mikono anamlisha. Kama wapo waliotofauti basi wanapaswa kubadilika kwa sababu sisi ndio tunapaswa kuwa marafiki wa wagonjwa,” anasema. 

Anatoa wito kwa wauguzi wanaoleta taswira mbaya kwa jamii kubadilika kwani taaluma hiyo ina misingi na maadili yanayopaswa kufuatwa. 

“Mfano, muuguzi anatakiwa kutunza siri za mgonjwa, kuheshimu utu wake, kumpenda na kumjali hivyo, turudi kwenye maadili yetu. 

 “Mimi hata akija mgonjwa mwenye tatizo la akili akinizidi umri namwamkia kwanza ndio nianze kumpa huduma kwa heshima na upendo,” anasema. 

Sanga anaiomba jamii nayo kuwa na mtazamo chanya kuhusu taaluma ya uuguzi kwani sio wote wanaokiuka maadili. 

“Kuna wimbo wa msanii mmoja hivi anamwambia mke wake nenda kapambane na wauguzi, sisi hatupambani na wagonjwa hivyo wasije na mtazamo huo,” anasema. Wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani, yaliyofanyika Mei 12, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema serikali itaendelea kutoa kipaumbele katika ajira za wauguzi kutokana na uhaba uliopo kwenye vituo vya afya. 

Anasema katika jitihada za Serikali huduma za wauguzi na wakunga, tayari imekamilisha muongozo wa kutoa huduma kwa kuzingatia utu, heshima na maadili. 

“Wauguzi wamekuwa wapambanaji wakubwa katika kutoa huduma kwa washukiwa wa ugonjwa unaosababishwa na virusi vya corona (Covid-19) hivyo, hongereni wauguzi wote nchini. 

“Tunatambua mchango wenu mkubwa katika kutumikia taifa, lakini pia tunataka mfuate maadili ya kazi yenu,” anasema Waziri Ummy. 

Anabainisha kuwa jumla ya waguzi 778 katika hospitali 15 za rufaa za mkoa wamepatiwa mafunzo muhimu ili kuwezesha mpango wa kutoa huduma rafiki kwa wananchi na kwa kujali utu wao. “Mafunzo haya yataendelea kutolewa katika ngazi zote za kutoa huduma na tayari tumetengeneza mfumo wa kupokea taarifa za malalamiko na kero kutoka kwenye vituo vya kutolea huduma,” anaeleza. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles