27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Misimamo ya baadhi ya wasomi wetu tahayuri kwa Taifa

YAPO masuala mengine unaweza kujikuta unacheka, lakini kiukweli yanatia dhuli kwa wananchi juu ya wasomi wetu (baadhi yao). Huwa sioni aibu kupongeza pale wasomi wetu wanapofanya vema, lakini pia huwa najisIkia deni kubwa la kusema pale ninapoona wasomi wetu wanahangaika na masuala madogo ambayo ni dhilifu kati ya mambo jadidi kwa maslahi mapana ya Taifa.

Taifa lolote lile duniani, pamoja na makundi mengine, huhitaji sana majagina kwenye kada anuai za kitaaluma. Na ndiyo maana niliwahi kuandika kwenye makala yangu ya ‘Nafasi ya Mwananchi kwenye matabaka matano ya mfumo wa utawala’ ya Novemba Mosi, 2017 iliyochapishwa na gazeti hili hili.

Kwenye Makala hiyo, nilieleza tabaka la tatu ambalo ni ‘The Elite Class’, ambalo sifa kuu, nikimnukuu nguli wa masuala ya utawala Chuo Kikuu cha Deakin, Mashariki ya Kati, Profesa Sally Totman, ni matakwa ya kuwaridhisha wengine (complaisance), kwa maana ya wananchi wa kawaida. Kwa tafsiri nyepesi, wasomi hawa huaminika kwa misimamo yao yenye manufaa mapana kwa taifa lao na aghalabu misimamo yao huwa madhubuti kiasi kwamba huwa ni ngumu kuibadilisha.

Tanzania ni nchi mwanachama wa Jumuiya ya Madola (nitaeleza kwa nini nimesema hili) tangu mwaka 1964. Na nchi hii inayo wasomi wakubwa; wapo waliolisaidia taifa hili kwa nafasi ya usomi wao na wapo ambao hawakulisaidia taifa, ila kujisaidia wao. Kati ya wasomi wengi waliolisaidia taifa hili ni Baba wa Taifa mwenyewe, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa nafasi yake kama Waziri mkuu wa kwanza, Rais na kama Baba wa Taifa la Tanzania.

Ninachojaribu kujiuliza hadi hii leo, vipi Mwalimu Nyerere angekuwa na msimamo legevu na badilifu kulingana na matakwa ya njaa zake kwa wakati ule, Tanzania ingekuwa ni ya namna gani? Kwa maana hii, wasomi ni dafiria ya taifa; tegemeo la wananchi wake. Wasomi wakiwa na misimamo inayoendeshwa kwa njaa zao, unafiki na ghiliba kwa matakwa ya kukidhi njaa zao ama itikadi zao, basi taifa hilo huyumba na wakati mwingine hata kuambulia tahayuri kwa fasiki zao kiitikadi.

Hunisikitisha kuona wasomi ambao leo wanaweza kuwaaminisha hivi na mkawa nao pamoja, lakini kesho wakawaambia lile kwa sababu aidha wamevutwa kusogea tabaka la pili (tabaka la wateule ambao sifa zao kubwa huwa ni ‘complicit’, yaani njama) na mabosi wao kwa vitisho vya kuachishwa kazi ama hatari ya maisha yao. Na punde wasogezwapo kwenye tabaka hili, niliwahi kusema, hulazimika kuacha misimamo yao na kufuata misimamo mipya ya kumfurahisha ‘mteuzi’ na wao, kama malipo, kukidhi haja ya njaa zao na usalama wao. Hapa utaona wanabadilika. Wanakuwa si wale tuliowazoea wakiwa tabaka la tatu, ‘The Ellite Class’. Taratibu wanaanza kubadilisha namna yao ya kuchanganua mambo kwa maslahi ya Taifa.

Mwaka wa tatu toka awamu hii iwepo madarakani, tumeshuhudia chaguzi endelevu; wanasiasa lukuki wakihama chama ‘A’ kwenda chama kile kwa madai ya kuunga mkono juhudi za awamu ya tano (ndiyo sababu yao kubwa) ambazo wamekuwa wakizipigania kule walikokuwa. Wengi wa wanaohama vyama ni wasomi wakubwa kabisa ndani ya nchi. Kabla hawajahama, walituaminisha baadhi ya mambo; wakihama wanaanza kuyapangua na kutuaminisha mengine.

Nimesoma makala ya aliyewahi kuwa kiongozi wa ngazi ya juu ndani ya Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro ya Septemba 16, 2018, ‘Tutumie 2020-2025 kujenga mifumo imara’ iliyochapishwa na gazeti la Mwananchi, hakika naona wasomi wetu wa sasa ni aina ya wasomi ambao hawaaminiki tena. Ndani ya makala ile, kwa mfano, Mtatiro alisema kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano inafanya vyema kwenye mapambano dhidi ya ufisadi, rushwa, nidhamu kazini na dawa za kulevya. Lakini kuna sehemu alisema kuwa, ‘ukiwauliza Watanzania kuwa wanataka nini, watasema wanataka maendeleo kwa vitendo na amani. Na anatuaminisha kuwa, kwa sasa yapo maendeleo kwa vitendo (akitolea mifano ya ujenzi wa stieglers  gorge, ufufuaji wa shirika la ndege, ujenzi wa bomba la mafuta la Tanga-Hoima na elimu bure) na ipo amani.

Kabla ya makala hii ya Mtatiro, msomi na mtafiti mkubwa, alikuwa ni mpigania haki, huku akituambia kuwa Tanzania inahitaji ‘utawala wa sheria’. Kwa mfano, ukiangalia hoja zake kwenye mitandao ya kijamii, utakubaliana na mimi. Julai 4, 2018, Mtatiro aliwahi kupost kipande cha video kilichomuonesha Jaji Mstaafu, Barnabas Samatta, aliyeshauri, akiwa kwenye mazungumzo ya mashauriano Ikulu, akisema, ‘utawala wa sheria lazima uambatane na haki’. Julai 7, Mtatiro alituma kipande kingine kikimuonesha Waziri wa Mambo ya ndani akimfukuza na kumzuia kuingia ukumbini, Kamishna wa Jeshi la Magereza. Hii ilikuwa ni ishara kubwa kwamba, Mtatiro aliubeza uongozi wa awamu ya tano kwa kuwa na aina ile ya mawaziri. Haya ni baadhi ya maandiko ambayo Watanzania walimwamini Mtatiro kuwa, ‘haki kwanza, maendeleo baadaye’ na naamini alijua kuwa, amani (ambayo leo hii anataka tumwamini kuwa ipo) ni tunda la haki.

Baada ya kuona kuwa matakwa yake, ambayo mimi naamini ni yake binafsi, hayajakidhiwa na usomi wake, Mtatiro ameamua kubadilisha na sasa anaamini (na ndiyo msimamo wake mpya) kuwa, maendeleo kwanza, haki baadaye. Amesahau kuwa, wakati anaandika na kuonesha msimamo wake mpya, tupo kwenye chaguzi ambazo zinaendeshwa kwa ‘sintofahamu’ ya sheria zilizomo kwenye Katiba. Tunafanya chaguzi mara nyingi huku matukio kibao ya wanachama wa baadhi ya vyama wakishambuliwa.

Email: [email protected]

Itaendelea wiki ijayo….

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles