24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

MINGO: KAMERA NI AJIRA TOSHA

Na MWANDISHI WETU


KILA kitu ni fursa katika maisha kama anavyoeleza mpiga picha na msanifu wa kazi za matangazo ya wasanii mbalimbali nchini, Said Mingo maarufu kwa jina la Mingo Classic.

Mingo kwa sasa ni mpiga picha wa msanii Malaika lakini pia anamiliki studio ya upigaji picha iliyopo Tabata, jijini Dar es Salaam, inayofanya kazi kubwa ya upigaji picha za wasanii na watu mashuhuri nchini.

Kazi ya upigaji picha anayofanya imemletea mafanikio makubwa katika maisha yake na sasa yupo mbioni kwenda kuweka makazi yake nchini Marekani, baada ya kutakiwa na kampuni ya Urban Studios ambayo inafanya kazi na msanii Malaika.

“Baada ya kuona picha nilizompiga Malaika, uongozi wa kampuni hiyo na nyingine ya vidonge kwa wasanii ya Vocal zone, zimetaka kufanya kazi na mimi hivyo wakati wowote tukifikia makubaliano nitakwenda kuishi Marekani kwa ajili ya kufanya nao kazi na nitakuwa mpiga picha wa kwanza Afrika Mashariki kuchukuliwa na kampuni hizo kubwa za nje,” anasema Mingo.

Akutana na Shilole

Safari ya mafanikio ya Mingo haikuwa rahisi, ilianza kwa msanii wa Bongo Fleva, Zuwena Mohamed (Shilole) ambaye alimkuta mtaani alipokuwa akijishughulisha na upigaji picha za harusi, ndipo akamtaka awe anampiga picha yeye katika kila maonyesho yake kwa malipo ya shilingi 30,000.

“Shilole alinichukua mtaani nilikuwa na ‘shoot’ video kabla ya kuwa mpiga picha, akaninunulia kamera na kompyuta mpakato (laptop) kipindi hicho sikuwa naweza kupiga picha vizuri, lakini alinivumilia nikawa naendelea na kazi hiyo na alikuwa akinilipa Sh 30,000 kwa kila shoo yake, lakini pia alinikutanisha na wasanii wengi maarufu.

“Kipindi hicho Shilole alinivumilia sana hadi alipokutana na aliyekuwa mpenzi wake, Nuh Mziwanda, mimi nilikuwa mpiga picha wao huku nikiendelea kujifunza upigaji picha vizuri, lakini pia Shilole namheshimu kwa kuwa ndiye msanii wa kwanza kunipandisha ndege kwa mara ya kwanza nilikwenda naye kwenye shoo yake iliyofanyika Mwanza,” anaeleza Mingo.

Kama ilivyo kawaida ya tamaa baada ya Mingo kuanza kujua kupiga picha vyema, walijitokeza wasanii Elias Barnaba na Dully Sykes wakimtaka awe mpiga picha wao huku wakiahidi kumlipa 50,000/-.

Akutana na Dully Sykes

“Dully alinitangazia dau la Sh 50,000 na Shilole alikuwa akinilipa Sh 30,000, nikaona bora niende kwa Dully lakini nilikuwa nikitumia kamera na ‘laptop’ ya Shilole na hakuwa akijua kama nimeacha kazi kwake baada ya kujua akawa akinitafuta kila kona,’’ anaeleza Mingo.

Mingo anasema kilichomsaidia kumkwepa Shilole mara kwa mara kulitokana na rafiki yake ambaye ni mwongozaji video za wasanii, Hanscana kwa kuwa muda mwingi walikuwa kwenye shughuli zao pamoja, hivyo akawa akimweleza kwamba Shilole anakuja naye anaondoka eneo la tukio.

“Dully alinisaidia kujua mikoa karibia yote ya Tanzania na alikuwa akiniongezea malipo kutoka Sh 50,000 akanilipa 70,000/- hadi ikafika100,000/- kwa kila anapofanya shoo moja.

“Namashukuru Dully kwani ndiye aliyenifundisha namna ya kuweka akiba ya fedha hadi nikafanikiwa kununua kamera yangu na nikarudisha kamera na laptop ya Shilole,” anaeleza Mingo.

Akutana na Ney wa Mitego

Mingo anasema licha ya Dully kumlipa kiasi hicho cha fedha na kumtembeza mikoa mingi, lakini alikuwa na tamaa ya kujuana na wasanii wengine maarufu akiwamo mwana hip hop, Emmanuel Elibariki (Ney wa Mitego), ambaye alikuwa akisikia umaarufu na sifa za mpiga picha huyo wakakubaliana kufanya kazi pamoja.

“Nilipokutana na Ney aliniuliza kama nafanya kazi na Dully, nilimkana Dully, akaniuliza kama nalipwa kiasi gani na Dully nikamweleza Sh100,000,  akaniambia atanilipa 150,000/- nikaanza kazi kwake nikaachana na Dully bila kumwambia,” anaeleza Mingo.

Mingo anasema kilichokuwa kikimfurahisha zaidi kwa Ney ni kukutanishwa na wasanii wenye majina makubwa, akiwemo Nassib Abdul (Diamond Platnumz) jambo ambalo kwake aliona ni kukua kwa kazi yake ya upigaji picha iliyokuwa ikihitaji kujulikana zaidi.

“Nimefanya kazi na Ney kwa miaka mitatu, nilikuwa nikiishi kwake kama mdogo wake, mwanzo alikuwa akinilipa vizuri lakini baadaye akaingiza undugu wa kujuana sana akawa anajisahau ananiona kama mdogo wake asiyestahili kulipwa na si ndugu yake wakati aliniambia mwenyewe niishi kwake ili iwe nafuu kama inatokea kazi ya kufanya ya ghafla.

“Alipoanza kutokunilipa akinichukulia kama mdogo wake, nikamtaka anunue kamera ya 7D ambayo ilikuwa ikiuzwa milioni 2.5 kwa mtu badala ya milioni nne dukani ili tuendane na ushindani wa wapiga picha wengine, hakununua zaidi ya kutoa ahadi zisizotekelezeka, nikamuazima mama fedha nikaongeza na nilizokuwa nikijiwekeza nikanunua kamera nikawa na kamera mbili,” anasema.

Mingo anasema anachoshukuru kwa Ney alifahamiana na wapigapicha wengine akiwemo Kasampaida wa Ayo tv, Kiface wa Diamond na pia alisafiri nchi mbalimbali ikiwamo Rwanda, Burundi na Kenya, lakini aliondoka kwa Ney na kwenda kuanza maisha yake mapya akiwa hana kitanda wala godoro.

Safari ya Fiesta

Alipotoka kwa Ney alipanga Tabata akawa akiishi bila kitanda wala godoro alikuwa na lap top na kamera tu, lakini akiwa katika maisha hayo Baraka Da Prince na Linah walimwita ili akawapige picha kwenye Fiesta.

Akutana na B12

Lakini alipokuwa Fiesta, mtangazaji wa Redio Clouds, B12, akawa akitumia picha zake kwa wingi kwenye matukio yake wakawa wakimlipa kiasi fulani na baada ya tamasha hilo kuisha wakamchukua kwa ajili ya kuwa mpigapicha wa kipindi cha XXL, wakawa wakimlipa 250,000/- pamoja na kumtangaza redioni.

“Nilipata kazi mpya nikaifanya kwa muda mfupi, kwani kuna siku Shilole alinipigia kwamba ana safari mikoani akiwa na aliyekuwa mpenzi wake Nuh Mziwanda na walinitangazia dau kubwa nikaondoka sikumuaga B12, nikaenda Mwanza niliporudi nikaamua kuanzisha studio yangu ya Mingo Studios ili nijisimamie mwenyewe.

Afungua studio

“Lakini kwa kuwa nilikuwa bado sijapata kiasi cha fedha za kutosha kufungua studio, nilitafuta sherehe za harusi nikapata mbili ambazo niliingiza shilingi milioni 3 nikaagiza taa maalumu za studio kutoka Dubai kwa milioni mbili nikapata, lakini fedha iliyobaki haikutosha kulipia pango la ofisi nikarudi kwa mama akanilipia miezi sita nikaanza kazi,” anaendelea kueleza Mingo.

Anasema kazi yake ya kwanza ilikuwa ni kupiga picha za harusi kwa gharama ya 500,000/- baada ya kupata fedha hizo alinunua vifaa vingine vinavyotakiwa kwenye studio yake kisha akatafuta warembo akawapiga picha za Modo akasambaza kwenye magroup mbalimbali ya wasanii.

“Nilipopiga picha zile kiufundi na kutumia taa vizuri wasanii wengi walioziona walivutiwa kupiga picha kwangu na wakaja akiwemo TID, Q Chif, Lulu Diva, Mr. Blue, Chege, Malaika na wengine wengi,” anaeleza.

Anasema kipindi hicho msanii Malaika ndiyo alikuwa amerudi kutoka Marekani alivutiwa na picha za Mingo, akamtafuta wakakubaliana kufanyakazi kama mpiga picha wake hadi hivi sasa amepata dili mbalimbali nje ya nchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles