30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Mikoa kinara kwa ukatili wa watoto yatajwa

ANDREW MSECHU – Dar es Salaam

RIPOTI ya haki za binadamu iliyotolewa Dar es Salaam jana, inaonyesha mikoa 19 inaongoza kwa ukatili dhidi ya watoto, huku ukatili wa kingono ukiwa juu zaidi.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotolewa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), mikoa hiyo ni Tabora, Njombe, Geita, Songwe, Simiyu, Pwani, Ruvuma, Kilimanjaro, Katavi, Mara, Dodoma, Kagera, Mwanza, Iringa, Morogoro, Singida, Tanga, Rukwa na Dar es Salaam.

Ripoti hiyo imeonyesha kuongezeka kwa ukatili huo, huku maeneo mengine vifo na mauaji yanayotokana na imani za kishirikina na ajali za barabarani vikipungua.

Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga, alisema wamebaini kuendelea kushamiri ukatili dhidi ya watoto, hasa wa kingono unaohusisha ubakaji na ulawiti.

“Katika matukio haya, kanda inayoongoza kwa matukio ya ukatili dhidi ya watoto ni Kanda ya Ziwa (asilimia 38), ikifuatiwa na Kanda ya Juu Kusini (asilimia 32), Kanda ya Pwani ya Kaskazini (asilimia 9) Kanda ya Kati (asilimia 7), Kanda ya Magharibi (asilimia 5),” alisema.

Alisema kupitia ripoti hiyo iliyoandaliwa kwa kutumia ripoti za mashirika, taarifa kutoka vitengo vya LHRC, vyombo vya habari na zinazopatikana kupitia mfumo wa shirika wa ufuatiliaji haki za binadamu, wamebaini asilimia 66 ya matukio ya ukatili dhidi ya watoto ni ukatili wa kingono na asilimia 44 ni ukatili wa kimwili.

Akitoa ufafanuzi kuhusu matukio ya kunyanyaswa kwa watoto, Mtafiti wa LHRC, Fundikira Wazambi, alisema ukatili wa watoto umeendelea kuwa changamoto kubwa, hasa ubakaji na ukatiki wa kingono.

Alisema katika asilimia 66 iliyorekodiwa katika ukatili wa kingono, karibu asilimia 90 ni ubakaji, na ilibainika watuhumiwa wakuu ni watu wa karibu wa watoto, ikiwemo wazazi, ndugu, jamaa, majirani na walimu.

Wazambi alisema katika Kanda ya Ziwa ambayo ndiyo inayoongoza kwa asilimia 38 ya matukio yote, maeneo yaliyoripotiwa ni katika mikoa ya Geita, Shinyanga, Mara, Simiyu na Kagera.

Alisema kwa Mkoa wa Mwanza, ulawiti wa watoto unaofanywa na watoto wenzao umeonekana kuwa changamoto katika kata 17, zikiwemo Igofo, Igoma na Nyegezi.

“Ukatili wa kimwili dhidi ya watoto pia unazidi kushamiri, ikiwemo watoto kupewa adhabu za kikatili, kumwagiwa maji ya moto na kuunguzwa sehemu za miili yao kwa makosa madogo kama kupika mboga bila ruhusa ya wazazi,” alisema Wazambi.

Alisema kutokana na vitendo hivyo, mimba za utotoni pia zimeonekana kushamiri.

Wazambi alisema kati ya Januari hadi Juni, matukio mengi ya mimba yameripotiwa Tanzania Bara, hasa mikoa ya Mara, Mwanza, Kagera na Lindi.

UKATILI DHIDI YA WANAWAKE

Henga alisema suala jingine ni kuongezeka ukatili dhidi ya wanawake, hasa ukatili wa kimwili unaotokana na mauaji yanayosababishwa na wivu wa mapenzi, pia ukatili wa kingono kama ilivyotokea kwa mtindo wa ‘teleza’ mkoani Kigoma.

Alisema matukio ya ukatili dhidi ya wanawake yameripotiwa katika mikoa ya Dodoma, Kagera, Kigoma, Morogoro, Dar es Salaam, Mbeya, Shinyanga na Manyara.

Henga alisema ripoti hiyo pia imebaini kuwa mauaji yanayotokana na imani za kishirikina na kujichukulia sheria mkononi yamepungua kidogo ikilinganishwa na miaka iliyopita, japo bado ni mengi.

HAKI NYINGINE

Henga alisema ripoti hiyo imebaini kuwepo kwa changamoto katika mazingira ya elimu, hasa upungufu wa vyoo/matundu ya vyoo shuleni.

Alitolea mfano mkoani Geita, ambako zaidi ya wanafunzi 4,000 wa shule za msingi Ihunamilo na Mwaloni wanalazimika kutumia vyoo vya majirani kutokana na ukosefu wa matundu ya vyoo kwenye shule hizo.

Alisema suala jingine ni marekebisho ya sheria ya asasi za kiraia ambayo yameathiri uhuru wao wa kujumuika kwa kuingilia uhuru wa utendaji wa kazi zao, pia kutoa mamlaka makubwa kwa msajili wa asasi za kiraia ikiwemo kuzifuta.

Henga alisema wanaamini mchakato wa kuteua makanimsha wa Tume ya Haki za Binadamu umeanza, hivyo wanaisihi Serikali kuukamilisha ili kusimamia masuala ya haki za binadamu na utawala bora nchini.

“Hatua hiyo ni muhimu kwa kuwa haki ya watu kuishi imeendelea kukiukwa kutokana na mauaji yanayohusishwa na imani za kishirikina, mauaji ya kikatili ya watoto mkoani Njombe, mauaji yanayodaiwa kufanywa na maofisa wa vyombo vya dola, adhabu ya kifo na ajali za barabarani zinazochangiwa na uzembe,” alisema Henga.

Alisema kwa sasa zaidi ya wafungwa 430 waliopo magerezani wanasubiri utekelezaji wa adhabu ya kifo, japokuwa Tanzania haijatekeleza adhabu hiyo tangu mwaka 1994.

“Katika kipindi cha miezi sita ya kwanza, LHRC imekusanya adhabu saba za vifo, ambazo ni mbili zaidi ya zile ilizokusanya katika kipindi kama hicho mwaka 2018,” alisema.

NINI KIFANYIKE

Akizungumzia kuhusu mapendekezo muhimu, Wazambi alisema ni vyema Serikali ihakikishe watoto ambao wamekuwa wahanga wakuu wa ukatili wanapata ulinzi zaidi na kuwa salama ili wafurahie haki zao kama binadamu.

Alisema ni vyema pia kwa Serikali kufikiria kuondoa utaratibu wa adhabu ya kifo ambayo inakiuka haki za binadamu na haijatekelezwa kwa zaidi ya miaka 20 sasa.

“Pia, ni vyema Serikali kupitia Wizara ya Sheria na Katiba ianzishe mchakato wa kufanyia marekebisho sheria zinazokandamiza haki za binadamu, ili kukuza na kulinda haki hizo.

“Sheria hizi ni pamoja na Sheria ya Huduma za Habari, Sheria ya Takwimu na Kanuni za Maudhui ya Mitandaoni,” alisema.     

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles