27.5 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

MIKATABA YA TBC YAMTIA MATATANI TIDO MHANDO

Na MANENO SELANYIKA -DAR ES SALAAM

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, kwa kibali maalumu imempandisha kizimbani na kumsomea mashtaka matano ya uhujumu uchumi aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Tido Mhando, anayedaiwa kulisababishia hasara shirika hilo zaidi ya shilingi milioni 800.

Tido  ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Azam Media Limited, akiwakilishwa na Wakili Dk. Ramadhan Maleta, alisomewa mashtaka hayo na mawakili wa Takukuru, Leonard Swai, akishirikiana na Pendo Temu pamoja na Aneth Mwavika mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa.

Katika shauri hilo namba 7/2018, Swai alidai kuwa Tido anakabiliwa na makosa matano ya uhujumu uchumi kwa kuisababishia hasara TBC.

Katika kosa la kwanza mshtakiwa anakabiliwa na matumizi mabaya ya madaraka.

Inadaiwa mahakamani hapo kuwa Juni 16, 2008, Tido akiwa Dubai kama mtumishi wa TBC, alitumia madaraka yake vibaya kwa kusaini mikataba ya uendeshaji wa vipindi kati ya TBC na Channel 2 Group Corporation (BVI) bila kutangaza zabuni na hivyo kuinufaisha channel hiyo.

Si hilo tu, inadaiwa Juni 20, 2008 akiwa huko huko Dubai kama Mkurugenzi Mkuu wa TBC, alitumia madaraka yake vibaya kwa kusaini mikataba ya kiutendaji kati ya TBC na Channel 2 Group bila kutangaza zabuni.

Agosti 11, 2008 na Septemba 2008, akiwa Dubai pia kama mwajiriwa wa TBC, inadaiwa kwa makusudi alisaini mikataba ya kununua, kusambaza na kusimika vifaa vya kurushia matangazo kati ya TBC na Channel 2 Group bila kutangaza zabuni ya manunuzi na kuisababishia channel hiyo kupata faida.

Wakili Swai alidai Novemba 16, 2008 akiwa Dubai kwa mara nyingine kwa makusudi alisaini mikataba ya uendeshaji wa miundombinu ya DTT kati ya TBC na Channel 2 Group bila kutangaza zabuni.

Alisema kitendo hicho kinakiuka kifungu cha 31 cha sheria ya manunuzi namba 21 ya mwaka 2004 na hivyo kuifanya chaneli hiyo ipate faida.

Katika kosa la tano inadaiwa aliisababishia mamlaka hasara ya Sh 887,112,219.19.

Pasipo kufafanua kwa kina hasara hiyo, ilielezwa mbele ya mahakama, Tido kwa mamlaka yake alisababisha hasara hiyo kati ya Juni 16 na Novemba 16, 2008  akiwa Falme za Kiarabu, kama mwajiriwa wa TBC kwa cheo cha Mkurugenzi Mkuu.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, mshtakiwa aliyakana na Wakili Swai   alieleza kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.

Wakili wa utetezi, Ramadhan Maleta, aliiomba mahakama hiyo impatie dhamana Tido.

Kwa sababu mahakama hiyo ilipewa kibali maalumu na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) cha kusikiliza kesi hiyo, Hakimu Nongwa alikubali ombi hilo la dhamana na alimtaka mshtakiwa atoe ama fedha taslimu shilingi milioni 444 au mali isiyohamishika yenye thamani ya fedha hiyo.

Pia alimtaka awe na wadhamini wawili ambapo kila mmoja asaini bondi ya shilingi milioni 500, pia hatakiwi kutoka nje ya nchi bila kibali cha mahakama.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 23, mwaka huu itakapotajwa na mshtakiwa alikamilisha masharti ya dhamana na kuachiwa.

HUYU NDIYE TIDO

Tido ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Azam Media Limited, ana uzoefu wa zaidi ya miaka 40 kwenye tasnia ya utangazaji na uandishi wa habari, amejulikana na kuheshimika katika tasnia hiyo ukanda wa Afrika Mashariki na ulimwenguni kote.

Alianza kazi yake ya utangazaji kama DJ na Radio Tanzania, baadaye akawa mtangazaji wa michezo maarufu na habari nyingine.

Tido pia ameripoti katika mashirika makubwa ya habari ikiwa ni pamoja na Deutsche Welle (DW), Sauti ya Amerika (VOA) na Shirika la Utangazaji la Kenya, ambalo lilijulikana wakati huo kama Sauti ya Kenya.

Alikuwa Mkuu wa Idara ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kati ya 1999 hadi 2006 na baada ya hapo alirudi Tanzania kwa wito wa Serikali ya Awamu ya Nne ili kuja kuliendeleza Shirika la Utangazaji nchini (TBC).

Akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa TBC kati ya mwaka 2006 na 2010, Mhando alifanya maboresho makubwa ya mfumo wa utendaji na kubadili programu mbalimbali kiasi cha kituo hicho kuanza kuonekana kuwa tishio hasa kwa washindani wake.

Wakati wa uongozi wa Tido, TBC mbali na kurusha taarifa za kampeni katika njia iliyoonekana kuwa si ya upendeleo hata kwa chama tawala, pia ilifanikiwa katika urushaji wa moja kwa moja wa matangazo ya mechi za mpira wa miguu na matukio makubwa ya kisiasa na kijamii, bunge na kufanya kituo hicho kuwa na uwezo wa kupambana na vituo vingine vya watu binafsi na pia kuaminiwa na wananchi.

Hata hivyo, baada ya miaka minne Serikali iliamua kuachana naye baada ya mkataba wake kuisha, hata hivyo mwanahabari huyo alieleza katika moja ya gazeti (si hili) kuwa uamuzi huo ulikuwa na utata.

Alisema kwa mujibu wa taratibu mfanyakazi anayemaliza mkataba wake anatakiwa kujulishwa suala hilo miezi sita kabla, jambo ambalo kwake halikufanyika.

Habari za Tido kuondoka TBC zilianza kuvuma wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, wakati iliposemekana kuwa alikuwa akipigana vijembe vya chini chini na vigogo wa CCM kutokana na vyombo hivyo vya umma kutangaza habari bila ya upendeleo.

Baadhi ya mambo yaliyoibua hisia kuwa mtendaji huyo wa shirika la umma angeondolewa ni msimamo wake wa kuendelea kurusha hewani kipindi cha “Jimbo kwa Jimbo” ambacho kilikutanisha wagombea ubunge wa vyama mbalimbali vya siasa kwenye mdahalo kuhusu maendeleo ya eneo lao.

Kipindi hicho kilichorushwa kwa wakati mmoja na vituo vya televisheni na redio kilianza kwa kushirikisha wagombea wote wa ubunge kwenye jimbo, lakini Katibu Mkuu wa CCM kwa wakati huo, Yusuf Makamba, akaandika waraka wa kuzuia wagombea wa CCM kushiriki kwenye mdahalo huo akidai kuwa chama hicho tawala kina njia zake za kufanya kampeni, hata hivyo TBC iliendelea kurusha vipindi hivyo.

Baada ya kuondoka TBC kabla ya kwenda Azam alipo hadi sasa, Tido alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communication Ltd (MCL) mwaka 2012 na kudumu miaka miwili na nusu.

HISTORIA YAKE BBC

Alijiunga na BBC idhaa ya Kiswahili Nairobi kama mwandishi wa habari. Ukuwaji wake ndani ya shirika ulimpelekea kuhamishiwa jijini London mwaka 1991 ambako aliteuliwa kuwa Mwafrika wa kwanza kuongoza Idara ya Idhaa ya Kiswahili BBC.

Alifikia kiwango cha juu cha heshima kutoka kwa waandishi wa habari katika nchi za Afrika zinazozungumza lugha ya Kiswahili kwa kina na ubora wa kazi yake ulionekana alipokuwa akiripoti kwa kina matukio muhimu nchini Ethiopia, Kenya, Somalia, Tanzania na Uganda.

Tido ni mmoja wa waandishi wa habari wachache wa Afrika Mashariki kufanya  mahojiano na marais wa sasa na wa zamani wa Afrika ya Mashariki na Kati.

Miongoni mwao ni pamoja na Rais wa DR Congo, Joseph Kabila, Mwai Kibaki kabla ya kuwa Rais wa Kenya na mtangulizi wake, Daniel Arap Moi, Rais wa Rwanda, Paster Bizimungu na Paul Kagame, marais wa Uganda, Idi Amin na Yoweri Museveni na Rais wa Zanzibar,  Salmin Amour na Amani Karume.

Mwaka wa 1990, Tido alikuwa mwandishi wa habari wa kwanza kuripoti taarifa ya kupotea na hatimaye kifo cha Waziri wa Mambo wa Nje wa Kenya, Dk. Robert Ouko na Januari 2001, alikuwa mwandishi wa habari wa mwisho kufanya mahojiano na Rais Laurent Kabila wa DR Congo. Majadiliano yao ya muda mrefu na ya wazi yalifanyika wiki moja kabla ya mauaji yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles