27.5 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Mikasa askari aliyehatarisha maisha yake kuzima moto matanki ya mafuta

FARAJA MASINDE-DAR ES SALAAM

AWALI alikuwa akifahamika kama askari wa kawaida tu katika kikosi cha Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Wilaya ya Kigamboni, zaidi akiwa anasimamia nidhamu. Lakini, kitendo cha dakika tano tu kimeweza kubadilisha kabisa historia yake.

Katika hili wapo wanaomuita shujaa, jasiri, mzalendo na majina mengine kama hayo.

Huyu siyo mwingine ni Station Sagent, Willison Mwageni, ambaye umaarufu wake ulianza katikati ya juma lililopita baada kujitolea kwa kuweka maisha yake rehani baada ya kuingia kwenye eneo la matenki ya mafuta ya kampuni ya Lake Oil, huku moto mkubwa ukiwaka.

Eneo aliloingia linaelezwa kuwa la hatari kutokana na moto huo kuwa mkali huku ukielekea kwenye matanki yenye mafuta na mitungi ya gesi ambapo inadaiwa endapo moto ungefika hapo, madhara yangekuwa kwenye eneo kubwa la Dar es Salaam na si Kigamboni pekee.

Askari huyo aliingia eneo hilo ili kufunga koki ambayo ilikuwa inasukuma mafuta hayo ya petroli na diseli, jambo ambalo lilikuwa likiongeza hatari kwa moto huo kuwa na madhara zaidi na pengine usizimike, kama ukifikia matanki hayo na mitungi ya gesi.

Baada ya Mwageni kuonyesha ujasiri huo uliopunguza madhara ya moto huo, alipandishwa cheo ambapo mwenyewe anasema “cheo hiki ni mwanga wa kutoka majukumu ya chini kwenda ya juu, japo hakuna utofauti mkubwa sana na kile cha awali, lakini sasa kuna kitu kimeongezeka ikiwa ni pamoja na nembo ya bibi na bwana, ambapo Mungu akipenda nitakuwa Mkaguzi Msaidizi siku za usoni.”

Ushiriki wake siku ya tukio

Mwageni anasema siku ya tukio Januari 8, mwaka huu, aliingia kazini kama ilivyo ada saa 1:30 asubuhi na kutoka saa 9:30 alasiri. Lakini ratiba ilibadilika mara baada ya kufika nyumbani kwake.

“Awali nilikuwa Mkuu wa Kambi ya Wilaya ya Kigamboni, jukumu langu kubwa lilikiwa ni kusimamia nidhamu jambo ambalo nimelifanikisha kwa kiwango cha juu hadi kufikia kupachikwa jina la ‘Chuma’. 

“Siku ya tukio nilikuwa natoka ofisini na saa tatu usiku nilikuwa nimefika nyumbani kwangu, nikiwa nimechoka kwa kuwa nilikuwa nimetoka kwa mwalimu wangu wa Sheria. “Lakini kitendo tu cha kufika nyumbani Pugu Bangulo, nikawa nimepigiwa simu na askari mwenzangu ambaye ni mkubwa kwangu (kwa sasa nimempita).

Station Sagent, Willison Mwageni akipandishwa cheo

“Aliniambia: ‘Mkuu wa kambi, Lake Oil tanki kule zimeshika moto’, mke wangu (Agatha Shitundu) akashtuka akaniambia wewe vipi, nikamwambia mama mimi naondoka, wakati huo nilikuwa nimekula chipsi peke yake kwa mwalimu wangu.

“Nilimwambia mke wangu mimi naondoka lakini nitarudi na kama sitarudi Mungu mwenyewe atakuwa amemua,” anasema Mwageni.

Safari ikaanza

Anasema safari ilianza huku akimuacha mkewe mwenye ujamzito asijue la kufanya na kuendesha pikipiki yake lakini alipofika sehemu aliitelekeza na ufunguo wake.

“Niliopofika njiani kuna kijana wangu nilikutana naye akiwa na abiria nikawaambia washuke nami niwahishwe ofisini haraka, tukiwa njiani tulinusurika ajali eneo la Uhasibu kutokana na mwendo kasi.

“Tulivyofika pale kuna askari wenzangu walinizuia, kutokana na hasira niliyokuwa ikabidi tutoleane lugha kali, baadae wakaniambia niende mimi na yule kijana wangu akalazimika kubaki, sababu nilitaka aniwahishe haraka lakini ikashindikana hivyo nikalazimika kutembea.

“Nilivyofika pale nikamkuta bosi wangu, Senior Assistant Kamishna, Elia Kakundi, ambaye ni Kamanda wa Mkoa wa Temeke, nikamsalimia nikamwambia nimekuja, akaniambia tunatakiwa tuuzime ule moto,” anasema Mwageni.

Kazi ya kuzima moto

Anasema alipofika eneo la tukio, alikuta ndiyo moto umetanda na kitu cha kwanza alichobaini kuwa kemikali ya kuzimia moto imeisha na yakawa yanatumika maji ya kawaida tu kuzima moto.

“Nilivyofika pale niliona gati ikiwa inavujisha mafuta, wao walikuwa wanapambana kwenye pampu zinazosukuma, kumbe tanki inayoruhusu mafuta koki namba saba ilikuwa wazi, ikabidi nipande niangalie nikawaambia hii ikitokea imeshindikana kudhibitiwa kule juu ikija hapa hakuna atakayebaki salama.

“Mitungi ya lake ikitokea imelipuka inaweza kufika hata Morogoro, kama ingetokea mlipuko basi madhara yake yangekuwa ni makubwa kwani pale kuna matanki mengi ambayo kwa kipindi hicho yalikuwa na mafuta.

“Ndiyo maana afande aliniambia kuwa tanki namba saba lipo wazi inatakiwa ikafungwe, alipotuita nikaona wenzangu wanarudi nyuma, lakini mimi nikaona nimpe moyo nisimuangushe,” anasema Mwageni.

Mwageni anasema kutokana na kutoka nyumbani haraka bila ya kuchukua vifaa alipofika eneo la tukio akisubiri kuletewa vifaa ikiwa ni pamoja na nguo maalum, maji yaliyokuwa yakitumika kuzima moto yaliisha.

“Baada ya maji kukata, moto ukaanza kuja upande wetu, nilichokifanya nikaaga nikasema jamani mimi nakwenda kama nikifa basi naomba nipelekee salamu kwa familia yangu na mke wangu mjamzito mwambieni nimekufa kwa jili ya kuokoa taifa, kwani inatakiwa muda mwingine kuwa mzalendo kwa ajili ya wengine kuweza kupona bila kujali utapata nini.

“Nilichofanya nikachukua fire extinguisher nikafungua pini kisha nikapiga sehemu ile kwa ajili ya kukata moto sababu isingekuwa hivyo zile gari na watu wote wasingetoka. Baada ya moto kupungua nikalazimika kuingia ndani kabisa ya moto kwa kupanda ngazi.

“Kule juu kulikuwa na joto kali, hewa hakuna zaidi ya kusambaa kwa petroli, ilitakiwa kuwa na ujasiri wa hali ya juu kuweza kuingia. Katika wale wenzangu sita ambao tuliteuliwa awali wakakataa, wawili walikuja wakati huo mimi natafuta koki, wakaniambia aisee koki iko huku,” anasema Mwageni.

Anasema baada ya ile koki kuonekana, wakaitikisa kwa nyundo ili iweze kulegea na kisha waifunge upya.

“Wakati naingia wahusika waliniambia kuwa tanki namba saba ndiyo ilikuwa inafanyiwa kazi muda mfupi uliopita, nikamwambia mwenzangu aigonge ile koki ili ilegee, lakini alipoona joto linazidi wote wakakimbia.

Ikabidi niwaambie wawe wananipiga na maji mgongoni ili kusaidia kupunguza joto na kupata hewa. Kweli walifanya hivyo, nilivyoingia kule ndani ikanibidi niwe navuta hewa kwa ndani, nikawa navuta kidogo tu huku nafunga ile koki.

Baadae nilipogeuka nyuma nikajikuta niko mwenyewe lakini sikukata tamaa niliendelea na kazi iliyonipeleka, moto ukawa unapungua na upande wa pili wakaanza kuzima na maji hivyo kazi ikawa rahisi.

“Nilitumia kama dakika tatu kufunga huku eneo zima nikitumia dakika tano, nilivyomaliza kufunga nikawa nimeishiwa nguvu kutokana na joto na harufu ya petroli, nikajivuta kusogea pembeni, nikawaona wenzangu wanakuja kwa ajili ya kunisaidia kwani miguu ilikuwa imeishiwa nguvu,” anasema.

Alivyohaha kutafuta huduma

Anasema baada ya kukamilisha zoezi hilo ikabidi Katibu Tawala (DAS) Wilaya ya Kigamboni, Rahel Mhando, aagize apelekwe kwenye matibabu jambo ambalo alikubaliana nalo.

“Walikuja wakanivua nguo pale na viatu nikabaki na suruali, DAS akasema nipelekwe Hopsitali ya Tungi, nikaingizwa kwenye gari la wagonjwa hadi hospitali, kufika pale daktari akajibu kuwa  wana wagonjwa wengine wa dharura nisubiri, baada ya majibu hayo kuna maji ambayo yalikuwa pale nikajimwagia kichwani nikaita pikipiki ili niondoke,” anasema.

Anasema wakati akiwa anasubiri pikipiki aondoke eneo hilo, DAS alipiga simu kwa daktari wa hospitali hiyo kutaka kujua kama amehudumiwa na ndipo daktari husika alipoanza kumtafuta.

 “Baada ya DAS kupiga simu ndipo daktari akaanza kuniulizia nikamwambia ‘tokeni zenu kwani hadi mpigiwe simu?’

Anasema alipotoka hospitalini hapo alirudi kwenye eneo la moto na kumkuta Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Sarah Msafiri akiwa amefika eneo hilo.

“Alinipongeza na kuagiza tena nipelekwe Hospitali ya Mnazi Mmoja, lakini kufika pale bado nikaambiwa kuwa natakiwa kuwa na bima ya afya au nitibiwe kesho yake niende kulipa.

“Nikaona bado wananivuruga nikatembea hadi kituo chetu cha faya nikiwa sina shati wala viatu, nilipofika pale kuna mfanyakazi mwenzetu nikamuomba anipatie nguo akanipa na viatu japo vilikuwa vya kike, nikavaa na kuondoka kwenda nyumbani,” anasema.

Mzozo na familia

Anasema baada ya tukio hilo alianza kupata lawama kutoka kwa ndugu zake ambao walimsihi kutorudia kwenda kwenye matukio ya namna hiyo.

Anasema aliwajibu kuwa hiyo ni sehemu ya kazi kama zilivyo kazi nyingine, kwa hiyo hakuna hatari kwa kuwa anafanya hivyo kwa ajili ya kuisaidia jamii, huku akibainisha kuwa hilo siyo tukio lake la kwanza.

“Kwangu mimi hili siyo tukio langu la kwanza, kuna matukio mengi ambayo nimeyafanya ikiwamo kuopoa miili ya watu mbalimbali, ndiyo maana kwangu mimi naona hili ni jambo la kawaida tu kwani najitolea kwa ajili ya nchi yangu lakini watu wananishangaa.

“Hivyo shukurani zote hizi zinazotolewa ziende kwa Mungu kwa kuwa ndiye kila kitu,” anasema.

Maisha binafsi

Mwageni ni mzaliwa wa tatu kati ya watoto nane wa familia ya Mwageni. Yeye na mkewe Agatha wamefanikiwa kupata watoto watatu ambao ni Alison (13), Alison (11) na Edson (4) huku wakitarajiwa kupata mtoto mwingine.

Elimu yake

Mwageni anasema amepata elimu katika Chuo cha Azani ngazi ya Stashahada ya sheria, huku mwaka jana alifanikiwa kuhitimu Shahada ya Sheria katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

Anataja malengo yake kuwa ni kuona siku moja akifikia ndoto yake ya kuwa jaji. Anasema awali alitamani siku moja kuwa Padri lakini ndoto hiyo iliyeyuka kutokana na changamoto za maisha alizokutana nazo akiwa mdogo.

“Nilikuwa na ndoto ya kuja kuwa Padri lakini safari yangu ya elimu ilikuwa imesheheni misukosuko mingi kiasi kwamba nilifukuzwa shule na kushindwa kufanya mtihani wangu wa kuhitimu kidato cha nne,” anasema Mwageni.

Historia ya kazi

Anasema awali baada ya kupata mafunzo, alijiunga na Kampuni binafsi ya Night Support, lakini kutokana na juhudi zake aliweza kupata nafasi ya kujiunga na Jeshi la Zimamoto.

DC Kigamboni

Mkuu wa Wialaya ya Kigamboni, Sara Msafiri, anasema ushujaa huo wa Mwageni, umesaidia kuokoa uchumi wa mataifa sita kwa sababu matanki hayo hutumika kusambaza mafuta kwa nchi sita zinazoizunguka Tanzania.

“Kwa tukio lilivyokuwa ilikuwa ni lazima mtu mmoja ajitolee maisha yake kwa ajili ya kuokoa uchumi wa nchi yetu na nchi nyingine sita zinazotegemea mafuta kutoka hapa.

“Hivyo hiki ni kilelezo cha juu kabisa cha kazi za kishujaa ambazo wamekuwa wakizifanya maaskari wetu,” anasema Sara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles