23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

MIFUGO 300 YAKUTWA SELOUS IKIWA TAABANI

mifugo-mnadani

Na ASHA BANI

MIFUGO mingine zaidi ya 300 imeonekana katika Kijiji cha Nyaminywili kilichopo Rufiji mkoani Pwani, ikiwa imedhoofika kutokana na kukosa chakula kwa muda mrefu baada ya wamiliki wake wa jamii ya Kimasai kushindwa kuendelea na safari katika Pori la Akiba la Selous.

 

Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi kwa njia ya simu jana Mkuu wa Pori la Selous, Henock Msocha, alisema baada ya kuendelea na msako wa mifugo hiyo wamepatikana 300 wakiwa hoi katika kijiji hicho.

Alisema juhudi zinaendelea kwa msako wa mifugo mengine licha ya kusikia tetesi kuwa kuna mifugo 900 imeonekana katika kijiji cha jirani na kuahidi kuendelea kutolea ufafanuzi hapo baadaye.

“Hadi sasa tayari mifugo 300 imepatikana na juhudi zinaendelea za kusaka mifugo mingine licha ya kusikia taarifa nisizothibitisha kuwa kuna mingine 900 imeonekana kwenye kijiji kingine cha jirani,” alisema Msocha.

Alisema wako katika mkakati wa kuwaruhusu wafugaji hao kutokana na hali zao kuimarika baada ya kupatiwa vyakula na matibabu.

 

Pia alisema jambo la busara kwa wananchi kuelewa ni kwamba, maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya hifadhi yawe hivyo na si vinginevyo ili kusitokee uharibifu wa hifadhi.

 

Alisema kwa sasa wanashirikiana na uongozi wa Chama cha Wafugaji Tanzania (CCWT) kusaka mifugo mingine iliyosalia ili kuweza kuirudisha mikononi mwa wafugaji hao ikiwa mizima.

Juzi Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia askari wa Selous, Kanda ya Kaskazini Mashariki Kingupira, imewaokoa wafugaji 50 waliokuwa wakiwapitisha jumla ya ng’ombe 18,000 ndani ya pori hilo.

Mbali na kuwaokoa pia wamekuta mizoga saba ya ng’ombe ikiwa imekufa katika pori hilo kutokana na ukosefu wa chakula na maji.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi, aliyewatembelea wafugaji hao jana kuwapa pole na kuwapelekea chakula yakiwemo maji na  unga, aliagiza waachiwe huku akitoa wito kwa wananchi kuacha kupita maeneo ya hifadhi kwa vile ni kosa kisheria.

Mmoja wa wafugaji, Lisses Cherahani, alisema walirubuniwa na mwenyeji wa kijiji jirani na Selous aliyejitambulisha kwao kwa jina la Mzigua na kumlipa Sh 5,000,000 ili aweze kuwavusha kwa njia ya mkato kwenda kijiji cha jirani kusaka malisho.

 

Baada ya Mzigua kuwatelekeza na wao kuishiwa chakula na maji kwa muda mrefu, wakaanza kuanguka na kunywa mikojo yao pamoja na damu za kondoo kuokoa maisha yao.

Pori la Akiba la Selous lina ukubwa wa kilomita za mraba 50,000 na limegawanywa katika kanda nane huku Kanda ya Mashariki Kipungira ikiwa moja kati ya kanda kubwa yenye kilomita za mraba 7,650, shughuli zinazofanyika katika pori hilo ni utalii wa picha pamoja na uwindaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles