30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

MIAKA MIWILI YA MAGUFULI: WAWEKEZAJI WAVUTIWE, WAKWEPA KODI WABANWE

Na RODGERS SWAI

WAKATI Watanzania na Bara la Afrika kwa ujumla wakiwa katika tafakari ya miaka miwili ya Rais Dk. John Magufuli madarakani, ni muhimu pia kutazama kwa mapana baadhi ya mambo au uamuzi mzuri ambao Serikali imeufanya.

Ni rahisi kusema kwamba, Rais Magufuli amefanya hiki au kile, lakini ni muhimu kutazama kwa mapana mambo hayo. Kuna mambo makubwa yaliyotokea nchini ambayo ni muhimu kuyaeleza, kwa vile miaka mingi baadaye yatabaki kuwa kama sehemu ya hiba (legacy) yake.

Ni wazi kuwa, ujumbe wa kwanza ambao Rais Magufuli ameutuma kwa Watanzania na jamii ya kimataifa ni kwamba yeye havumilii rushwa kwa namna yoyote ile. Hii maana yake ni kwamba, Serikali yake inawakaribisha wawekezaji wote kuja kuwekeza Tanzania ili mradi wakae mbali na vitendo hivyo.

Ndiyo sababu, ripoti ya karibuni ya Taasisi ya RMB imeonyesha kwamba Tanzania imepanda kwa nafasi mbili katika orodha iliyopewa jina la “Where to Invest in Africa”, inayotoa taarifa kuhusu nchi zinazovutia wawekezaji kwenda kuwekeza.

Hii inaweza kumaanisha jambo moja tu kwamba, jitihada hizo za Rais Magufuli zimeanza kuwavutia wawekezaji kutoka nje wanaoona kwamba mazingira ya Tanzania ya kufanya uwekezaji hayana harufu ya rushwa na kama mtu ametimiza vigezo na masharti yote hatafanyiwa mizengwe.

Pia, ukali huu wa Serikali ya Magufuli haufanyiki kwa wawekezaji kutoka nje pekee kama tulivyoona katika sakata la Barrick/Acacia kuhusu sakata la mchanga wa madini (makinikia) au kwa Kampuni ya Petra Diamonds, lakini tumeliona pia kwa wafanyabiashara wa ndani.

Kwa mfano, mfanyabiashara maarufu nchini, Yusuf Manji. Huyu anafahamika kama mmoja wa wafanyabiashara wakubwa zaidi na wanaoheshimika kwa ukwasi wake nchini. Lakini katika muda wa miaka miwili ya Rais Magufuli, Manji ameshitakiwa kwa makosa mawili.

Mosi ni kutuhumiwa kutumia dawa za kulevya (mahakama ilimuachia huru), pili;  kosa la kukutwa na vitambaa vya sare za JWTZ (Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DPP) aliifuta kesi hiyo baada ya kuwasilisha mahakamani nia ya kutoendelea nayo).

Kimsingi, kwa sasa Watanzania wanajua na wafanyabiashara matajiri wanajua kwamba kama watakosea, basi hawatasalimika kwa sababu ya utajiri au ushawishi wao.

Bahati nzuri ni kwamba, Rais Magufuli mwenyewe ameonyesha kuwa mstari wa mbele katika vita hii kwa kusisitiza kila mahali alikokuwa akienda kwamba yeye ni Rais wa wote na haogopi kufanya chochote kwa maslahi ya Watanzania. Hakuna namna ambayo mtu anaweza kutofautisha msimamo huo na Rais mwenyewe aliyeko madarakani.

Tayari ujumbe umeshatumwa nje ya nchi kupitia Acacia na Petra Diamonds kwamba Tanzania pamoja na kuvutia wawekezaji, lakini si tena ‘shamba la bibi’ ambako wawekezaji wanaweza tu kuja kuchuma na kuondoka kadri watakavyo.

Ndiyo sababu ni jambo la msingi kwa kila mmoja wetu kumpongeza Rais Magufuli kwa sababu katika kipindi chake cha miaka miwili tu madarakani, amefanya vitu vitakavyoweka alama ya kudumu kwa vizazi vingi vijavyo na vitamuweka katika rekodi ya miaka mingi baada ya kutoka madarakani.

Pamoja na mambo mengine, huu pia unatakiwa kuwa wakati sahihi wa kuwapongeza wafanyabiashara na wawekezaji wanaofanya biashara zao kwa kufuata taratibu zote na kusaidia ujenzi wa Taifa letu.

Kwa taarifa tu, zipo kampuni nyingi nchini (za ndani na nje ya nchi) ambazo uwapo wake umesaidia kuongeza ajira na kulipa kodi inayosaidia kuboresha huduma nyingine na kuongeza uwezo wa watu kumudu mahitaji yao ya kila siku.

Kwa hiyo, kufurahia juhudi hizi za Rais Magufuli katika miaka yake miwili madarakani ni kufurahia pia uwapo wa biashara na wafanyabiashara walioona kwamba inawezekana kufanya shughuli za kiuchumi kwa uhalali kwa kufuata sheria za nchi na ukafanikiwa ukiwa ndani ya Taifa hili.

Pia, kitendo cha kuwa mkali dhidi ya baadhi ya walioonekana kwenda kinyume cha sheria za nchi, Rais Magufuli ameonyesha kwamba wafanyabiashara na wawekezaji wanaofanya shughuli zao zenye kufuata sheria hizo hawana sababu za kuhofia chochote.

Wito wangu kwa Serikali ya Rais Magufuli, ikiwa sasa inaingia katika mwaka wake wa tatu ni kwamba, inatakiwa izidishe juhudi za kuwaleta wawekezaji kutoka nje, pia iendelee kuziba mianya kwa wafanyabiashara wa ndani wasiokuwa wazalendo kutokana na vitendo vyao vya kukwepa kodi ili kujinufaisha.

Hii ni kwa sababu kuna taarifa ziliwahi kutolewa siku za nyuma kwamba, kuna ufisadi mwingi ulikuwa unafanyika uliohusisha baadhi ya wafanyabiashara na watumishi wachache wa umma wasiokuwa waadilifu na ulisababisha upotevu mkubwa wa mapato ya Serikali.

Pia ni jambo jema kwamba sasa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) nayo imeanza kazi ya kuchunguza uozo uliokuwapo na kuchukua hatua dhidi ya wahusika.

Kwa bahati nzuri, hakuna tena mfanyabiashara au mwekezaji atakayekwepa kulipa kodi ya Serikali halafu ataachwa bila sheria kuchukua mkondo wake na heko zote hapa zinakwenda kwa Rais Magufuli mwenyewe.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles