27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

MIAKA MIWILI YA JPM NA MABADILIKO SEKTA YA ELIMU

Na MWASU SWARE-DODOMA


SEKTA ya elimu ni mtambuka, hii ni kwa sababu inagusa maisha ya kila siku ya binadamu.

Kutokana na hali hiyo, mataifa mbalimbali ikiwamo Tanzania tumekuwa na mikakati kadhaa ya kuhakikisha elimu kuanzia ya awali, msingi, sekondari na chuo kikuu inakidhi vigezo vya kitaifa na kimataifa.

Novemba 5, mwaka huu, Rais Dk. John Magufuli ametimiza miaka miwili madarakani, ambapo kwa uwezo wake mara baada ya kuapishwa kuiongoza nchi, miongoni mwa ahadi alizotoa wakati akihutubia Bunge Novemba 20, 2015 ni kutoa elimu bure.

Utekelezaji wa Sera hii ya Elimu Bure ni kuanzia awali hadi kidato cha nne, ambapo michango na ada zote sasa zinagharimiwa na Serikali na hivyo kuwapunguzia wazazi/walezi gharama ambazo zilikuwa kero kwao na wakati mwingine kuzolotesha mahudhurio ya wanafunzi shuleni.

Katika kutekeleza Sera ya Elimu Msingi Bila Malipo, kuanzia Januari, mwaka jana, kila mwezi Serikali imekuwa ikituma fedha moja kwa moja shuleni takribana Sh bilioni 18.77 kwa ajili ya ruzuku ya uendeshaji kwa shule za msingi na sekondari.

Kutokana na utekelezaji wa sera hii, wazazi wamekuwa na mwamko wa kuhakikisha watoto wote ambao walikosa fursa ya kusoma sasa wanapata elimu kwa kuwa gharama zote zinalipwa na Serikali, hivyo kufanya idadi ya wanaoandikishwa darasa la kwanza kuongezeka kutoka wanafunzi 1,568,378 mwaka 2015 hadi 2,078,379 mwaka 2017 sawa na ongezeko la asilimia 32.5.

Kuwapo kwa fursa hiyo kumeibua changamoto mbalimbali ikiwamo upungufu wa madarasa, matundu ya vyoo na madawati.

Kutokana na changamoto hizo, Serikali kupitia kampeni na wadau mbalimbali imeweza kutengeneza na kusambaza madawati kwa shule za msingi na sekondari na hivyo kutatua changamoto hiyo kwa asilimia 95.

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, imekuwa ikitekeleza shughuli za ujenzi na ukarabati wa vyumba vya madarasa.

Uboreshaji miundombinu

Sekta ya elimu kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo (Development Partners), imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali kwa kutumia Mfuko wa Pamoja  na kufadhili baadhi ya miradi moja kwa moja.

Kupitia mfumo huu, fedha hutolewa kwa kukidhi vigezo (Disbursed Linked Results – DLRs) vilivyokubalika baada ya kufanyiwa uhakiki na kuthibitika utekelezaji wake umefikiwa. Huu ni mfumo wa ufuatiliaji unaohakikisha vipaumbele vya sekta ya elimu vinatekelezwa kwa kuzingatia mipango na bajeti iliyoidhinishwa na Bunge kwa mwaka husika.

Hadi sasa, wamefanikiwa kujenga na kukarabati madarasa 1,405, matundu ya vyoo 3,394, ofisi za walimu sita, mabweni 261, mabwalo tisa, nyumba za walimu 11, majengo ya utawala katika shule 13 na maabara tatu.

Pia wameweka uzio katika shule nne,  maktaba mbili na uwekaji wa umeme katika shule mbili upo hatua nzuri na hadi sasa halmashauri 129 zimenufaika kupitia mpango huu.

 

Usambazaji wa vitabu

Kwa kipindi hiki, Serikali ilipokea vitabu 1,030,000 vya masomo ya Fizikia, Kemia, Biolojia na Hisabati kutoka Serikali ya India kwa ajili ya wanafunzi wa shule za sekondari wa kidato cha tatu hadi cha sita wanaosoma mchepuo wa Sayansi.

Kupatikana kwa vitabu hivi kwa wanafunzi vimeongeza ari ya wanafunzi kusoma masomo ya sayansi lakini pia itawasaidia wanafunzi kuvitumia vitabu kama njia ya kujifunzia pale ambapo mwalimu wa somo husika atakosekana.

Sayansi ndiyo kauli mbiu ya serikali ya awamu ya tano, uchumi wa viwanda hauwezi kukua kama nchi haitakuwa na wataalamu wa kutosha katika masuala ya sayansi, sasa ili kufikia malengo hayo hizi ndizo jitihada zinazofanyika katika kuhakikisha malengo yanafikiwa.

 

Ukarabati shule kongwe

Tanzania ina jumla ya shule kongwe za sekondari 88 ambazo ni za umma. Miundombinu ya shule hizo kwa sasa imechakaa.

Hivyo, Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kushirikiana na OR – TAMISEMI imeanza kukarabati shule kongwe  za sekondari, hii ni kwa sababu siku zote elimu bora huenda sambamba na uboreshaji wa mazingira ya kufundishia na kujifunzia.

Katika kipindi cha mwaka 2016/17 Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia inakarabati shule 42 katika awamu hii ya kwanza ambapo kati ya hizo, shule 25 zinakarabatiwa na Programu ya Lipa Kulingana na Matokeo – EP4R na 17 zinakarabatiwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania.

Shule kongwe za sekondari ambazo zinahusika na ukarabati kwa awamu hii ya kwanza kupitia EP4R ni Jangwani, Azania, Kibaha, Kigoma, Tosamaganga, Songea Wasichana, Malangali, Milambo, Minaki na Nangwa zinaendelea kukarabatiwa chini ya usimamizi wa Wakala wa Majengo Tanzania – TBA.

Nyingine ni shule za sekondari Mpwapwa, Musoma Ufundi, Mtwara Ufundi, Ifakara, Kantalamba, Tanga Ufundi, Ifunda Ufundi, Moshi Ufundi, Bwiru Wavulana na Kibiti. Shule hizi zinakarabatiwa kwa usimamizi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya – MUST,  na shule za sekondari Iyunga, Chidya, Ndwika na Kisutu zinakarabatiwa chini ya uongozi wa shule na bodi zake.

Shule za sekondari 17 ambazo ni Ilboru, Same, Pugu, Mwenge, Nganza, Mzumbe, Kilakala, Tabora Wavulana, Tabora Wasichana, Msalato Wasichana, Dodoma, Ruvu, Korogwe, Bwiru Wasichana, Sengerema, Bihawana na Kondoa Wasichana zinakarabatiwa kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA).

 

Ununuzi na usambazaji wa vifaa

Wakati  Serikali ya Awamu ya Tano inatimiza miaka miwili, imefanikiwa kununua na kusambaza vifaa vingi vya wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

Tangu nchi ipate uhuru mwaka 1961 haijawahi kununua vifaa vingi vya wanafunzi wenye mahitaji maalumu kama ambavyo imefanya ndani ya miaka miwili. Jumla ya Sh bilioni 3.6 zimetumika kununua vifaa hivi na vimelenga kutatua changamoto ya upungufu wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu.

Vifaa hivyo vinajumuisha mashine za kuandikia maandishi ya nukta nundu ambazo zipo mashine 932; karatasi za kuandikia maandishi ya nukta nundu 2548; karatasi za kudurufishia maandishi ya nukta nundu ‘ream’ 1150; mashine sikio (hearing aid), 1150 na vifaa vya upimaji kielimu.

Aidha, P4R iliagiza na kusambaza vifaa vya maabara vya masomo ya Sayansi ya Fizikia, Kemia na Biolojia kwa shule za sekondari 1696. Vifaa hivi vinathamani ya zaidi ya Sh bilioni 16.9.

Kati ya shule hizo shule 1625 ni za wananchi, maarufu kwa jina la shule za kata na 71 ni kongwe. Shule hizi za kata ni jumla ya shule zote zilizokamilisha ujenzi wa maabara hadi kufikia Desemba mwaka jana.

 

Mafaniko yatokanayo na KKK

Wanafunzi wengi sasa wanapenda Kusoma, Kuandika na Kuhesabu kutokana na mbinu zinazotumika katika kufundishia. Miongoni mwa mbinu zinazotumika ni kuimba, kucheza na kuchora ambapo watoto huelewa kwa urahisi zaidi.

Mahudhurio ya wanafunzi yameendelea kuimarika kutokana na wanafunzi kupenda shule. Mbinu mpya za KKK zimesidia kuwaweka walimu karibu na wanafunzi na hivyo kubaini kiurahisi changamoto zinazowakabili na kuzitatua mapema. Mfano Mwalimu anapoimba au kucheza na wanafunzi basi ile inawaweka karibu zaidi.

 

Madeni kwa walimu 86,234

Serikali imelipa madai ya walimu 86,234 yasiyo ya mishahara kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2015/2016 na 2016/2017. Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2015/2016 hadi kufikia Juni, 2016. Jumla ya Sh bilioni 22,629,352,309 zililipwa kwa walimu 63,814 na katika kipindi cha mwaka wa fedha 2016/17 hadi Machi, 2017 Sh bilioni 10,505,160,275 zimelipwa kwa walimu 22,420.

 

Mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu

Katika mwaka wa fedha 2016/17, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ilitoa mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 483.8 kwa wanafunzi 122,374  ambapo wanafunzi 28,785 ni wapya.

Mkopo wao uligharimu Sh bilion 104.6  na wanafunzi 93,559 ni wanaoendelea na masomo ambao mkopo wao uligharimu Sh 379.2.

Mwaka 2017/18 Serikali imetenga Sh bilioni 427.55 kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wanufaika 122,000 wanaonza na wanaoendelea na masomo.

Mwandishi wa makala hii ni Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Wizara ya Elimu, Sayasi na Teknolojia.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles