26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Miaka 58 ya Uhuru: Haijatokea

*Magufuli aeleza sababu sherehe za Uhuru kufanyika Mwanza

*Viongozi wakuu wa vyama vya upinzani watoa kauli

*Lowassa, Sumaye, Pinda wanena utendaji wa Rais Magufuli

Bakari Kimwanga-MWANZA

HAIJATOKEA. Ndivyo unavyoweza kusema kutokana na kufana kwa sherehe za miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika ambazo kwa mara ya kwanza zimehudhuriwa na viongozi wote wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na wa vyama vikuu vya siasa.

Sherehe hizo zilifanyika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza jana na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi.

Kutokana na wingi wa watu uwanjani, wengine walilazimika kuwekewa televisheni Uwanja wa Furahisha ili kushuhudia sherehe hizo baada ya kukosa nafasi ya kukaa ndani ya Uwanja wa CCM Kirumba.

Akizungumza kuhusu maadhimisho hayo, Rais Dk. John Magufuli alisema yamefanyika jijini hapa ili kuondokana na kufanya mambo kwa mazoea.

“Ikumbukwe hatukufanya sherehe hizi kwa miaka miwili, mwaka 2015 na mwaka 2018, badala yake fedha zake zilifanya kazi za maendeleo. Hivyo hivyo ndiyo sababu  tukaamua tufanye sherehe hizi mkoani Mwanza, tofauti na ilivyozoeleka… hii ni kwa sababu ya kubadili mazoea,” alisema Rais Magufuli.

Alisema sherehe hizo huambatana na fursa mbalimbali ikiwamo kuchochea maendeleo ya mkoa.

Aliyataja miongoni mwa mambo ya kujivunia tangu nchi ipate uhuru ni kulinda amani, upendo na kudumisha muungano.

“Leo (jana) ni siku muhimu sana  na kwa kweli Mwanza mmefunika, hongereni sana, nimeambiwa uwanja umejaa, kule nje kumejaa, Uwanja wa Furahisha umejaa, hii haijawahi kutokea.

“Siku kama ya leo (jana) Desemba 9, mwaka 1961 Tanganyika ilipata uhuru wake kutoka kwa wakoloni, uhuru huo ulitokana na jitihada za Watanganyika na hii ilitokana na juhudi za kiongozi shupavu Baba wa Taifa Mwalimu Julius  Nyerere, ambaye waliwaunganisha Watanganyika.

“Pia ninawapongeza wazee wetu 17 ambao tarehe 7 Julai, 1954 walishiriki mkutano wa kuanzishwa kwa Tanu ambayo ilifanikisha kupatikana uhuru wetu.

“Hawa wazee wanastahili pongezi kubwa kwa mchango walioutoa katika taifa letu, ingawa wengi wao hawapo na Mwenyezi Mungu aziweke roho zao mahali pema,” alisema Rais Magufuli

Aliwapongeza viongozi waliopita pamoja na Watanzania wote kwa mafanikio yaliyopatikana nchini, jambo ambalo linadhihirisha kwamba wameweza.

Alisema pamoja na mafanikio hayo yaliyopatikana, lakini pia na changamoto hazikosekani kwani suala la kujenga nchi lina changamoto zake pia.

“Pamoja na mafanikio yaliyopatikana changamoto nazo hazikosekani, kama nilivyosema awali, kujenga nchi kuna changamoto zake. Hivyo jukumu la kizazi cha sasa ni kuendeleza pale walipoishia watangulizi.

“Kinachofurahisha zaidi nchi yetu imani imeendelea kuimarika, nchi yetu imekuwa yenye umoja na mshikamano, namshukuru Rais Shein (Dk. Ali Mohamed Shein) ambaye tunashirikiana kulinda muungano wetu kikamilifu,” alisema.

HARAKATI ZA UHURU

Rais Magufuli alisema uhuru ulikuwa ni hatua za mwanzo za harakati za kutaka kulijenga taifa letu.

“Si lelemama, ila ni kazi ngumu ambayo tumevuka milima na mabonde, hivyo inatupa fursa ya kufanya tathmini kuhusu wapi tumefikia, katika ujenzi wa taifa letu.

“Na katika hilo napenda kutumia fursa hii kuzipongeza awamu zote zilizotangulia za uongozi wa nchi yetu kwa kazi kubwa ilizofanya za kuijenga nchi yetu, sio siri katika kipindi cha miaka 58 ya uhuru nchi yetu imepata mafanikio makubwa.

“Na kusema ukweli, kila awamu imefanikiwa kufanikisha haya kuanzia awamu ya kwanza iliyoongozwa na Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, awamu ya pili ya mzee Mwinyi (Ali Hassan Mwinyi), awamu ya tatu mzee Mkapa (Benjamin Mkapa) pamoja na awamu ya nne ya mzee Kikwete (Jakaya Kikwete).

 “Baadhi ya mafanikio tuliyoyapata ni kujenga na kudumisha amani katika nchi yetu. Tangu tumepata uhuru mwaka 1961, nchi yetu imekuwa kwenye amani na hivyo kuifanya isifike sio tu barani Afrika, bali duniani kote kwa ujumla.

MTANDAO WA BARABARA

Rais Magufuli alisema mafanikio kadhaa yamepatikana, ikiwamo kuhakikisha nchi inakuwa na mtandao wa barabara za lami unaounganisha makao makuu ya mikoa na wilaya.

 “Tumepata mafanikio mengine makubwa katika nyanja za kiuchumi na kijamii, na hapa nitatoa mifano michache.

“Wakati tunapata uhuru, baada ya kutawaliwa na wakoloni kwa takribani miaka 76, nchi yetu ilikuwa na barabara za lami zinazounganisha mkoa na mkoa, wilaya na wilaya, zilikuwa kilometa 360 tu.

“Kipande cha barabara ya Dar es Salaam hadi Morogoro pamoja na kipande cha Tanga-Korogwe na Arusha-Moshi,” alisema Rais Magufuli

Alisema kwa sasa mtandao wa barabara za lami zilizopo ni kilometa 12,679.55, aidha kilometa nyingine zaidi ya 2,400 zinaendelea kujengwa kwa kiwango cha lami na wakati huohuo kilometa 7,087 zipo katika hatua mbalimbali za maandalizi kwa kujengwa kiwango cha lami.

MADARAJA NA AFYA

Rais Magufuli alisema Serikali imejenga madaraja madogo madogo zaidi ya 8,000, ya kati zaidi ya 79 na makubwa 17, huku mengine yapo hatua mbalimbali, likiwamo Daraja la Busisi ambalo lilizinduliwa ujenzi wake hivi karibuni kwa kuwekwa jiwe la msingi na Daraja la Salender jijini Dar es Salaam.

 “Ukiachilia barabara, wakati nchi yetu tunapata uhuru ilikuwa na vituo vya kutolea huduma za afya 1,095, yaani hospitali 98, vituo vya afya 22 na zahanati 975, lakini leo hii tuna vituo 7,293, hospitali 178, vituo vya afya 795 na zahanati 6,285.

 “Wakati tunapata uhuru tulikuwa na shule za msingi 3,100, hivi sasa zipo shule za msingi 17,379, shule za sekondari zilikuwa 41, hivi sasa 4,817, vyuo tulikuwa nacho kimoja, leo tuna vyuo vikuu 48.

“Madaktari waliosajiliwa walikuwa 403, ambao kati yao Watanganyika walikuwa 12, leo tuna zaidi ya madaktari 9,400.

“Mwaka 1961 wahandisi wazalendo walikuwa wawili tu, kwa sasa nchi ina wahandisi wazalendo zaidi ya 19,164 waliosajiliwa na bodi,” alisema Rais Magufuli.

Alisema baada ya uhuru wastani wa mtu kuishi ulikuwa miaka 37, lakini kwa sasa wastani Mtanzania kuishi ni miaka 61.

“Lakini pia kwa idadi ya watu wamejitahidi sana Watanzania ambapo wakati uhuru unapatikana nchi ilikuwa na watu takribani milioni 9, lakini hivi sasa wapo zaidi ya milioni 55,” alisema na kuwapongeza Watanzania.

Alisema mafanikio yamepatikana pia katika nyanja za kimataifa, ambapo Tanzania imetoa mchango mkubwa katika ukombozi wa Bara la Afrika.

“Kazi ya kujenga taifa si lelemama, ni kazi yetu sisi kizazi cha sasa tuhakikishe tunayalinda mafanikio yaliyopatikana na pia tunaendeleza pale walipoishia waliotutangulia na hiki ndicho haswa sisi Serikali ya awamu ya tano tunajitahidi kukifanya,” alisema.

UJENZI WA UCHUMI

Rais Magufuli alisema sasa kazi iliyopo ni kujenga uchumi wa nchi, kwani Serikali imeamua kusimamia sekta ya viwanda ambapo ndani ya miaka minne viwanda 4,000 vimejengwa nchini.

Licha ya hayo, alisema Serikali inaendelea na ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli ya kisasa kwani ili kufikia uchumi wa kati nchi inategemea umeme wa uhakika ambapo sasa ujenzi unaendelea katika maporomoko ya Mto Rufiji linapojengwa Bwawa la Nyerere ambalo litakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 2,115.

“Hivi majuzi Shirika la Reli limeanza safari kutoka Dar es Salaam kwenda Moshi kwa akina Mbowe (Freeman) na nimeona wanafurahia ‘aikambee’. Pia tunaendelea na ujenzi wa miundombinu ya bandari.

“Kwa upande wa umeme mbali ya kutumia gesi asili na vyanzo vingine, tumeanza na ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere, tunaendelea na mradi wa kupeleka umeme vijijini (REA), ambako kwa sasa idadi ya vijiji vilivyoongezewa umeme vimeongezeka na hiyo ni kuhakikisha tunafanikiwa katika kuimairisha ujenzi wa viwanda,” alisema Rais Magufuli.

MSAMAHA KWA WAFUNGWA

Katika kuadhimisha Miaka 58 ya Uhuru, Rais Magufuli alitoa msamaha kwa wafungwa 5,533 waliofungwa kati ya siku moja na mwaka mmoja na wale waliofungwa kwa miaka mingi na tayari wametumikia sehemu kubwa ya vifungo vyao na kubakisha kipindi kisichozidi mwaka mmoja.

“Mtakumbuka miezi michache iliyopita nilitembelea baadhi ya magereza, ikiwamo Gereza la Butimba ambapo nilishuhudia kuwapo mlundikano mkubwa wa wafungwa na kwa taarifa niliyopewa hali kama hiyo haikuwa kwenye gereza hilo tu, bali ni kwa magereza yote nchini na mpaka leo tuna wafungwa 17,547 na mahabusu 18,256, kwa pamoja wanakuwa 35,803 hii ni idadi kubwa.

“Baadhi ya wafungwa wamefungwa kwa makosa madogo madogo kama kuiba kuku, kumtukana rafiki yake, kujibizana na mpenzi wake au mshikaji wake na wengine kwa kukosa mawakili wa kuwatetea vizuri katika kesi zao, lakini wengine kwa kushindwa kulipa faini na kuna wengine wamefungwa kwa kuonewa.

“Kama binadamu hali niliyojionea pale Butimba ilinihuzunisha na kunisikitisha sana, ilikuwa hali mbaya, hivyo kwa kutambua kuwa hakuna mwanadamu aliye mkamilifu, na wote tumeshatubu na kuomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu, na kwa kutambua wafungwa wengi wanajutia makosa yao na hawako tayari kuyarudia, ninapenda nitumie kwa mujibu wa madaraka niliyopewa ya kusamehe au kufuta adhamu ya mtu aliyetiwa hatiani na mahakama, nimeguswa na nimeamua kusamehe jumla ya wafungwa 5,533,” alisema Rais Magufuli.

Aliagiza wafungwa hao waachiwe mara moja bila kucheleweshwa wala kuwawekea mizengwe kwani orodha ya majina yao yote anayo.

VIONGOZI WA VYAMA

Akiwa anahutubia katika sherehe hizo za uhuru, Rais Magufuli aliwaita viongozi wa vyama vya upinzani pamoja na wastaafu kutoa salamu zao.

Aliyekuwa wa kwanza kuzungumza ni Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, John Shibuda ambaye alizungumza kwa lugha ya Kisukuma ambapo muda wote alikuwa akimsifu Rais Magufuli.

JOHN CHEYO

Mwenyekiti wa Chama cha DP, John Cheyo, aliwapongeza  Watanzania kwa sherehe za miaka 58 ya Uhuru.

“Mimi nilisherehekea Uhuru nikiwa na miaka 15, nilicheza dansi usiku kucha, sasa leo ni miaka 58, hongereni Watanzania wote,” alisema Cheyo.

PROFESA LIPUMBA

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba alianza na ombi la uwapo wa demokrasia.

Akitumia salamu ya chama chake ya ‘haki’, Profesa Lipumba alisema pamoja na hatua kubwa ya maendeleo inayopigwa, ni jukumu na wajibu wa Rais Magufuli na Serikali kuendeleza misingi ya demokrasia.

FREEMAN MBOWE

Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema na Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe, alisema Rais Magufuli anayo dhamana ya kuhakikisha si tu demokrasia inalindwa na kukuzwa, bali pia uwepo wa haki na usawa kwa wote bila kujali tofauti zao.

“Nimekuja kushiriki sherehe za miaka 58 ya Uhuru kama uthibitisho wa kuwapo maridhiano, upendo na mshikamano wa Watanzania. Siku ya leo (jana) ifungue milango ya kupendana, kuvumiliana na kuheshimiana

“Rais unayo nafasi ya kipekee kuweka historia ya kuweka maridhiano kwani wapo wanaolalamika kuumia, tunaomba uweke utangamano.

“Nimeshiriki maadhimisho haya kuthibitisha misingi ya umoja, mshikamano na undugu miongoni mwa Watanzania.

“Nakuomba Mheshimiwa Rais kutumia nafasi na dhamana yako kulinda demokrasia. Kusiwe na wanaofurahi huku wengine wakilalamika,” alisema Mbowe.

MIZENGO PINDA

Aliyekuwa wa kwanza kuitwa na Rais Dk. Magufuli jkwa upande wa viongozi wastaafu ni Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda, ambaye alimshukuru kiongozi huyo wa nchi huku akiwataka Watanzana kulinda amani.

“Ninamshukuru rais kwa kunipa nafasi, tunajitahidi kumuunga mkono. Kubwa tu ninawaomba Watanzania tushikilie amani na utulivu wa taifa letu kama msingi muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu,” alisema Pinda.

EDWARD LOWASSA

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, alisema alipendezwa na hotuba ya Rais Magufuli kuhusu amani ya nchi.

“Nimependezwa sana na hotuba yako, Mwalimu Nyerere wakati wa Azimio la Arusha aliwaambia Watanzania akija mtu jeuri na fedhuli akakuuliza nini Watanzania mnataka nini, mjibuni kiungwana tuna amani.

 “Lakini msingi huo ndio msingi anaotumia Rais Magufuli leo kuongoza nchi yetu kuleta mshikamano na umoja kwa nchi yetu, nampongeza sana anafanya kazi nzuri sana. Kama akiachiwa akapiga miaka yake 10 nchi hii itabadilika, itakuwa nchi kubwa ya ajabu na yenye maendeleo makubwa sana.

“Kwa hiyo nawaomba tumuunge mkono, tumsaidie nchi yetu iende mbele, Rais nakupongeza sana hongera,” alisema Lowassa akimalizia kwa kuimba ‘mchaka, mchaka’ huku wananchi wakiitikia ‘chinja’ na mwisho akamalizia na salamu ya CCM ya ‘CCM oyeee’.

FREDERICK SUMAYE

Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye, alipongeza kazi kubwa inayofanywa ya kujenga uchumi wa nchi.

“Leo (jana) tunasherehekea uhuru ambao tuliupata, lakini kama alivyosema Rais (Magufuli), bado tuna kazi kubwa ya kuupata uhuru wa kiuchumi ili nchi yetu isiwe tegemezi, kwani bado tuna tatizo la utegemezi.

“Lakini naamini kwa kazi inayofanywa na Serikali hii ya awamu ya tano na zingine zote za nyuma, ninaamini tutakua sana, tunakaribia kupata uhuru wa uchumi. Mheshimiwa Rais tunakupongeza sana kwa kazi njema,” alisema Sumaye.

JOHN MALECELA

Waziri Mkuu na Makamu wa Rais wa Kwanza mstaafu, John Malecela alipongeza kazi kubwa ya maendeleo inayofanywa na Serikali.

“Kwa mimi ninayetoka Mkoa wa Dodoma, ningependa niseme ushahidi wa kinachofanyika awamu ya tano, ukitaka kuona halisi nenda mjini Dodoma, kwa maendeleo tunapaa.

“Tunakushukuru sana Rais Magufuli kwa kazi kubwa unayofanya na niungane na wenzangu waliotoa wito kwamba tukusaidie katika mapinduzi unayoleta katika kujenga Tanzania mpya,” alisema.

ALI HASSAN MWINYI

Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi aliwataka Watanzania waendelee kulinda umoja, usalama na amani ya nchi.

“Kwa umoja wetu tuendelee kulinda umoja wetu, usalama na amani. Amani ni jambo linalohitaji watu wengi ila uovu auhitaji watu wengi kama wapo waache maana halina sababu. Tuendelee kulinda amani,” alisema Mwinyi.

MBOWE NA SUMAYE

Sherehe hizi zilionekana kama jukwaa la kuwakutanisha wana siasa waliohama Chadema na kujiunga na CCM na wale waliobaki chama hicho cha upinzani.

Hii ni karibu wiki moja sasa, baada ya Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye atangaze kujiondoa ndani ya Chadema.

Kwa mara ya kwanza jana alikutana na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.

Mbali na Sumaye, pia Mbowe alikutana na aliyekuwa mgombea urais wa Chadema katika uchaguzi wa mwaka 2015, Edward Lowassa ambaye naye alijiondoa ndani ya chama hicho na kurejea CCM Machi  Mosi mwaka huu.

Mbowe alihudhuria maadhimisho ya Uhuru baada ya kukosekana miaka mitatu.

Aliambatana na Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kati, Lazaro Nyalandu ambao kila mmoja alikuwa amevalia suti nadhifu na mashati meupe ndani na si makombati kama vazi maalumu la chama hicho.

Katika uwanja hakukuwa na wanachama wa Chadema waliovaa sare za chama hicho, huku wenzao wa CCM baadhi yao walionekana wakiwa na mavazi yao maalumu yenye rangi za chama hicho za kijani na njano.

Akiwasili uwanjani, Mbowe aliongozana na Nyalandu ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii katika Serikali ya awamu ya nne ambao kwa pamoja waliingia kwa kupita katika lango la viongozi wa kitaifa na kupokewa kwa heshima zote kama ilivyofanyika kwa viongozi wengine.

Baada ya kupokewa, Mbowe na Nyalandu waliongozwa moja kwa moja na kuonyeshwa eneo la kuketi katika jukwaa kuu waliko viongozi wengine wa kitaifa wa sasa na wastaafu.

Hatua ya kushiriki kwa Mbowe maadhimisho ya mwaka huu, kumehitimisha kile kilichodaiwa kususia sherehe hizo za kitaifa kwa muda wa miaka mitatu tangu mwaka 2015 baada ya Chadema kutoa tamko la kutotambua uchaguzi uliomwingiza madarani Rais Magufuli.

SARE ZA VYAMA

Wakati Mbowe akiingia uwanjani bila kuvaa mavazi ya chama chao, maarufu ‘kombati’, hali ilikuwa tofauti kwa wabunge wa chama hicho waliohudhuria sherehe hizo.

Godbles Lema (Arusha Mjini), John Mnyika (Kibamba) na Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ (Mbeya Mjini) na Meya wa Ubungo, Dar es Salaam, Boniface Jacob, waliingia uwanjani wakiwa wamevalia ‘kombati’ huku wale wa CCM waliokaa jukwaa kuu nao wakiwa na sare zao za kijani.

Wabunge hao waliketi eneo moja na Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Victoria na mbunge wa zamani wa Nyamagana, Ezekia Wenje.

MAMIA WAFURIKA

Wakazi wa jijini Mwanza na vitongoji vyake walijitokeza kwa wingi katika maadhimisho hayo.

Hamasa ya wananchi wa Mwanza na mikoa jirani ya Kanda ya Ziwa, inaonekana kwa jinsi ambavyo walijitokeza kuujaza uwanja huo.

Milango uwanjani hapo ilifunguliwa tangu saa 10 alfajiri ambapo wananchi kuanza kuingia jukwaani.

Kufikia saa 1:30 asubuhi majukwaa ya uwanja huo wenye uwezo wa kuingiza zaidi ya 25,000 yalikuwa yamejaa huku msururu mrefu wa watu wanaotaka kuingia ukiwa bado uko nje.

Akizungumza uwanjani hapo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella alisema wingi wa wananchi waliojitokeza umetokana na mapenzi ya Watanzania kwa Serikali na taifa lao, hamasa na ushirikishwaji wa kila kada ya uongozi uliofanywa na kamati ya maandalizi.

“Tumetoa hamasa kupitia matangazo kwa njia mbalimbali, kuanzia vyombo rasmi vya habari, mitandao ya kijamii, magari ya matangazo mitaani pamoja na viongozi wa Serikali za mitaa,” alisema Mongella.

RAIS MAGUFULI ALIVYOINGIA

Rais Magufuli aliwasili  uwanjani huku akipokewa kwa shangwe na vigelegele kutoka kila kona ya uwanja huo.

Aliingia uwanjani saa 3:14 asubuhi, akiwa kwenye gari la wazi akiongozwa na pikipiki nane, gari, moja mbele na nyingine nyuma.

Alipoingia uwanjani alizunguka akiwapungia wananchi mikono huku akishangiliwa.

Baada ya kushuka katika gari la wazi, Rais Magufuli alipanda jukwaa maalumu lililokuwa limeandaliwa, kisha ukapigwa wimbo wa taifa ulioambatana na mizinga 21.

Ulipopigwa mzinga wa kwanza watu walisikika wakishangilia kwa shangwe, huku wengine wakipigwa na mshangao wakitaka kuangalia mizinga hiyo inapotokea.

Hata hivyo, kadiri ilivyoendelea kupigwa mizinga hiyo, wananchi walionekana kukubaliana na hali hiyo tofauti na ilivyokuwa ikipingwa mizinga ya awali.

Wimbo wa Taifa ulipomalizika kupigwa, Rais Magufuli alikagua gwaride la vikosi vya ulinzi na usalama.

VIONGOZI WALIOHUDHURIA

Viongozi mbalimbali walihudhuria sherehe hizo wakiwamo Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi na marais wastaafu Benjamin Mkapa na Ali Hassan Mwinyi.

Wengine ni mawaziri wakuu wastaafu wa Tanzania, Frederick Sumaye, John Malecela, Mizengo Pinda, Edward Lowassa, Spika wa Bunge mstaafu, Anne Makinda na Spika wa Bunge, Job Ndugai.

MABALOZI NA VYAMA

Pia, walikuwapo mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao pamoja na wakuu wa mashirika ya kimataifa.

MAONYESHO

Baada ya kukamilika shughuli za gwaride, yalifanyika maonyesho ya ndege za kivita ambazo zilipita kwa mwendo kasi na kuonyesha mbwembwe nyingi.

Pia kikosi cha makomandoo wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) walishuka kwa helkopita na kuonyesha namna ya kuokoa kiongozi mkubwa kutoka kwa watekaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles