30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

MIAKA 40 YA CCM ‘WATU WAMETAMBUA WALIPOKOSEA WANATAKA KUJISAHIHISHA’

Na NORA DAMIAN,

JUMAPILI wiki hii Chama Cha Mapinduzi (CCM), kitaadhimisha miaka 40 tangu kuzaliwa kwake huku Rais Dk. John Magufuli akihudhuria kwa mara ya kwanza tangu achaguliwe Julai mwaka jana kuwa Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho.

Chama hicho kinasherehekea miaka 40 huku kikiandika historia mpya ya kuwa na mabadiliko ya muundo wa chama kwa kupunguza idadi ya vikao na wajumbe wa ngazi zote

Mageuzi hayo ya kiuongozi, kimfumo na kiutawala yalifanywa mwishoni mwa mwaka jana na Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho, Rais Dk. John Magufuli wakati wa kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM (NEC).

Kuelekea katika kilele cha maadhimisho hayo ambayo yatafanyika mkoani Dodoma, ngazi mbalimbali za chama hicho zimekuwa zikiendesha makongamano kwa lengo la kujadili kilipotoka, kilipo na kinapoelekea.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, CCM Wilaya ya Ilala, kilifanya kongamano ambalo lilishirikisha viongozi wa kata mbalimbali, kamati za siasa, jumuiya na waasisi ambapo mada kadhaa zilijadiliwa zikiwamo ‘Miaka 40 ya CCM changamoto na mafanikio yake, Uchaguzi wa CCM na jumuiya zake na Mikakati ya ushindi dhidi ya upinzani’.

Kada wa chama hicho, Dk. Lucas Kisasa ambaye alikuwa mmoja wa watoa mada katika kongamano hilo anasema; “Katika umri wa miaka 40 CCM kimefanya mambo makubwa, kushika dola ndio lengo kubwa kwa chama chochote cha siasa…CCM kina demokrasia marais wanaachiana madaraka.

Hata hivyo anasema licha ya chama hicho kufanikiwa kushika dola lakini bado kinakabiliwa na changamoto ambazo zimesababisha kuwapo kwa mitafaruku na mipasuko.

Dk. Kisasa anaainisha baadhi ya changamoto hizo kuwa ni upungufu wa mapato ya chama katika ngazi zote, udhibiti hafifu wa miradi na kushindwa kutunza na kukarabati rasilimali zilizopo.

“Nidhamu ya maadili imekiathiri chama mtu hawezi kuchaguliwa hadi atote fedha mambo yote haya yanapunguza mvuto wa chama kwa wananchi, CCM kijiimarishe kihakikishe kinapata viongozi sahihi bila rushwa au ujanja ujanja,” anasema Dk. Kisasa.

Naye Mwenyekiti wa CCM Ilala, Assah Simba, anasema nidhamu na maadili ya viongozi bado ni tatizo kubwa kwani kumekuwa na kutoheshimiana kati ya wanachama na viongozi jambo ambalo ni hatari kwa chama.

Anasema chama kinaongozwa kwa kufuata taratibu, kanuni na miongozo hivyo ni vizuri wanachama na viongozi wakazingatia ili kuepuka kukipeleka chama kusikotarajiwa.

“Tusome katiba ya chama chetu ituongoze kwenda kule tunakotarajia. Hatutaki migawanyiko isiyokuwa na tija, tuwe na dhamira moja ya kukitumikia chama na si kuwa na dhamira mbadala,” anasema Simba.

UCHAGUZI 2015

Simba anasema katika uchaguzi uliopita kulikuwa na wasaliti wengi ndani ya chama hicho na hadi sasa wako wengine ambao wamevuliwa uanachama baada ya uchunguzi kufanyika na kubainika kuwa ni wasaliti.

“Viongozi wana baridi yabisi kwa sababu ya unafiki, ndani ya wana CCM wapo watu si wakweli, tukiwa na viongozi wa namna hiyo yaani wako nusu nusu ni hatari kwa ustawi wa chama. Wapo watu hawafanyi kazi za chama na hata wachache wanaofanya wanafanya kwa kubahatisha tu na chaguzi zilizopita zimedhihirisha tuna viongozi waliosaliti,” anasema Simba.

Anasema ingawa wanachama wanaonekana kuwa wengi lakini kwenye chaguzi wamekuwa wakishindwa na kusema kuwa hali hiyo inamaanisha kuna wasaliti wengi.

 “Taarifa zilizoko makao makuu zinaonyesha Mkoa wa Dar es Salaam bado hatujapeleka wasaliti kulinganisha na mikoa mingine na inaonekana tunalindana kwa sababu ya mazoea na ushirika. Kama mnashindwa kutaja wasaliti maana yake na viongozi wa juu ni wasaliti.

“Wako waliopotea si kwa sababu ya kupenda bali kushawishiwa na kwenda kutoa kura zao upande wa pili lakini bado wako CCM…tabia hii tuiache,” anasema.

Hata hivyo anasema wana mwelekeo mzuri katika uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka 2019 na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

“Jitihada zinazofanywa na viongozi wa matawi na kata zinaonyesha watu wametambua walipokosea na sasa wanataka kujisahihisha,” anasema. 

Mwenyekiti huyo wa CCM Ilala, anasema hawatawakumbatia wanachama wanaoonekana kuwa na ndimi mbili kwani ni bora kuwa na wanachama wachache waaminifu badala ya kuwa na wanachama wengi wadanganyifu.

UCHAGUZI WA NDANI

Kila baada ya miaka mitano chama hicho hufanya uchaguzi wake wa ndani na mwaka huu pia kinatarajia kuufanya.

Kada wa chama hicho, Dk. Lucas Kisasa, anasema CCM kinatakiwa kuwa makini ili kuhakikisha kinachagua viongozi wenye uwezo wa kuhimili vishindo vya ushindani wa kisiasa katika ngazi zote za uongozi.

Dk. Kisasa anataja baadhi ya sifa za kiongozi bora kuwa ni lazima awe mtu anayejiheshimu, anayejitambua na kujielewa katika kutetea siasa za chama hicho, ajitolee, awe mfano wa tabia nzuri kwa vitendo, atosheke na asiwe na tamaa.

“Mtu hawezi kuchaguliwa hadi atoe fedha mambo yote haya yanapunguza mvuto wa chama kwa wananchi…uongozi utokane na watu wa nchi hii bila rushwa au vitisho, watu wasipate nafasi kwa ujanja unjanja,” anasema Dk. Kisasa.

MIKAKATI

Katibu wa Mwenezi wa CCM Ilala, Said Sidde, anasema wanaendelea kufanya maboresho mbalimbali ili kuendana na mageuzi ya kiuongozi, kimfumo na kiutawala ambayo yanalenga kukirejesha chama hicho kwa wanachama.

"Tumefanya ziara katika kata mbalimbali na tumefanikiwa kurudisha wana CCM waliokwenda upinzani, tutajenga historia kubwa mwishoni mwa uongozi wetu," anasema Sidde.

Kauli mbiu ya maadhimisho ya miaka 40 ya CCM ni ‘CCM Mpya,Tanzania Mpya’.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles