31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Miaka 30 mkataba wa mtoto: Kisa cha watoto waliodaiwa kulawitiwa na kuelekezwa kulawiti wenzao

LEONARD MANG’OHA -ALIYEKUWA MISUNGWI

WAKATI Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto wa (ICRC) ukitimiza miaka 30 tangu kupitishwa kwake mwaka 1989, bado jamii inakabiliwa na changamoto nyingi za kufikia malengo yake.

Mkataba huo unalenga kuhakikisha kila mtoto anakuwa na haki ya kuishi katika mazingira mazuri na kupata chakula bora, haki ya kukua, kupata elimu bora na kucheza, haki ya ulinzi kutoka kwa wazazi, walezi, jamii na serikali dhidi ya udhalil­ishaji wa aina yoyote na kushiriki katika masuala yote yanayomhusu.

Ili kufanikisha kufikiwa kwa malengo ya ICRC, nchi zilizoridhia mkataba huo zilitakiwa kuhakikisha kuwa na mifumo ya kisera na sheria inayozingatia haki hizo.

Ni kutokana na mkataba huo, ambao Tanzania iliuridhia Julai 10, 1991, ulitoa msukumo wa kutungwa kwa Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 ambayo imeweka mifumo na taratibu za ulinzi wa haki za mtoto katika mazingira ya Kitanzania.

Pamoja na kuridhiwa kwa mkataba huo, kutungwa kwa Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 bila kusahau juhudi ambazo zimeendelea kuchukuliwa na wadau mbalimbali nchini, bado jamii imeendelea kushuhudia vitendo vya ukatili ua ukiuk­waji wa haki za watoto.

Mathalani, Ripoti ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), ya mwaka 2018, inaonesha ongezeko la vitendo vya ukatili dhidi ya watoto kutoka 4,728 mwaka 2017 hadi 6,376 mwaka 2018. Ukiukaji huu pia umeshuhudia ongezeko kubwa la ukatili wa kingono, hasa ubakaji na ulawiti.

Matukio hayo yameongezeka kutoka 759 katika kipindi cha miezi sita ya mwan­zo ya 2017 hadi kufikia matukio 2,365 katika kipindi kama hicho mwaka 2018.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, asilimia 91 ya matukio ya ukatili dhidi ya watoto yaliyoripotiwa na vyombo vya habari na kukusanywa na kituo hicho, yalikuwa ni ya ukatili wa kingono. Katika takwimu hizo, asilimia tisa yalikuwa ni matukio ya ukatili wa kimwili na kisaikolojia.

Mikoa ya Mwanza, Dar es Salaam, Kili­manjaro, Mbeya, Iringa na Singida ilikuwa na kiwango cha juu cha matukio hayo kati ya mikoa 10 iliyotembelewa na LHRC wakati wa utafiti.

Utafiti wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), mwaka 2011 unaonesha kuwa takribani asilimia 28 ya wasichana na asilimia 13 ya wavulana wamefikwa na ukatili wa kijinsia kabla ya kutimiza miaka 18.

Pia utafiti huo unaonesha kuwa karibu wasichana watatu kati ya 10 na mvulana mmoja kati ya saba waliripoti kutendewa walau tukio moja la ukatili wa kijinsia kabla ya kutimiza umri wa miaka 18.

Kuwapo kwa matukio hayo kunakwen­da kinyume cha ibara ya 3(2) ya mkataba wa kimataifa wa ulinzi wa mtoto wa 1989 ambao unayataka mataifa yote wana­chama kuhakikisha kunakuwapo ulinzi na huduma bora na muhimu kwa ustawi wa mtoto.

Uchunguzi uliofanywa na MTAN­ZANIA katika Wilaya ya Misungwi, hivi karibuni, umebaini kuwapo kwa matukio kadhaa ya ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto. Miongoni mwa matukio hayo ni lililomhusisha mkazi wa kijiji cha Old Misungwi, Saddala Sahaban (45), anayedaiwa kuwalawiti Emmanuel Juma na Yasin Hamis (si majina yao halisi), huku akidaiwa kuwaelekeza wawafanyie vitendo kama hivyo watoto wenzao.

WAZAZI WASIMULIA ALIVYOBAINIKA

Sofia Mabula (si jina halisi), mama mzazi wa Emmanuel, anadai kuwa aligundua mwanawe anafanyiwa kitendo hicho baada ya kukamatwa shuleni akifanyiwa hivyo na Yassin ambaye pia ni mwathirika wa vitendo hivyo.

Anasema akiwa safarini, alipigiwa simu na kupewa taarifa za tukio hilo na baada ya kufika ndipo walipobaini kuwa mtoto mwenzake waliyekamatwa naye alifundishwa na Saddala.

“… akamwambia na wewe uwe un­awafanyia watoto wengine hivi nilivy­okufanyia na kweli mwanangu alikutwa anafanyiwa na huyo mtoto. Baada ya kukamatwa, alikuwa anaficha ila wavulana wenzake wakamwambia kwanini unany­amaza unatudhalilisha sisi watoto wa kiume wenzako.

“Nilipopigiwa simu, nikawaambia liwekwe hadharani, lisiishie kuwapa watoto adhabu kwa sababu lina madhara makubwa,” anasema Sofia.

Baada ya suala hilo kufikishwa polisi ndipo mtoto huyo alimtaja Saddala na kuelezea jinsi alivyokuwa akimtendea ki­tendo hicho kwa muda wa miaka mitatu.

“Mwanangu ndiye alikuwa akitendewa kwa muda mrefu, yule mwingine nadhani alimtendea mara moja au mbili. Mtoto ameharibiwa zaidi kisaikolojia hadi sasa nahangaika na saikolojia ya mwanangu,” anasema Sofia.

Kutokana na tukio hilo, mama huyo amelazimika kubadilisha ratiba za kazi zake ili kumsimamia mwanawe kwa ka­ribu jambo linalokwamisha shughuli zake za kujitafutia kipato.

“… nikikaa hata saa moja sijamwona mtoto ninakuwa na mawazo, hata akienda shule ninakuwa na mawazo, inaonekana ameanza kumchezea muda mrefu mimi sijui kwa sababu nilikuwa nafanya bi­ashara nashinda huko,” anasema Sofia.

Anasema licha ya Yassin kukamatwa shuleni akimtendea mwanawe kitendo hicho, alilazimika kumsamehe yeye na familia yake kwa sababu alitambua kuwa hata yeye tayari amepata shida.

“Wale watoto wako chini ya umri wa miaka 18 hawaruhusiwi kupewe adhabu ya kufungwa miaka kadhaa na kweli walivyo­soma nilijisikia kuumia, lakini nikasema siwezi kupingana na sheria nikaridhika,” anasema Sofia.

Anaeleza kuumizwa na kitendo cha mtuhumiwa kuachiwa huru miezi mich­ache tangu alipohukumiwa kutumikia kifungo cha maisha jela.

“Wanasema kwamba atatufanya nini sisi ni ukoo mkubwa najisikia vibaya kwa sababu na yeye ana watoto pale shuleni alipokuwa anasoma mwanangu na hawa­jadhurika kwa lolote,” anasema Sofia.

SADDALA

Mtuhumiwa katika kesi hiyo jinai namba 43 ya mwaka 2019, Saddala Shaban, anasema wanafunzi wa shule hiyo walim­zoea kwa sababu alikuwa na shamba jirani na shule, na kwamba anashangaa kitendo cha watoto kumtaja baada ya kukamatwa wakitenda vitendo hivyo. “… mimi nina shamba kule karibu na shule wakawa wanakuja kuchukua maembe, kukawa na mazoea hadi ikafikia hatua kwenye mchakamchaka wananiimba nikawa kama babu yao.

“Sasa yale mazoea tu, wamefanya mam­bo yao huko wakaniingiza na mimi humo ndiyo yaliyonigharimu,” anasema Saddala.

Saddala anasema kutokana na kutori­dhishwa na hukumu hiyo, aliamua kukata rufaa ambapo Mahakama ya Rufaa ilimkuta hana hatia.

Mashahidi waliotoa ushahidi katika kesi hiyo ni pamoja na Dk. Mussa Mishamo wa Hospitali ya Wilaya ya Misungwi, Baraka Nestory, askari mwenye namba E.8001 D|CPL Wilson na wengine watatu ambao majina yao yanahifadhiwa.

BABA WA YASSIN

Hamis Mabula (si jina lake halisi) baba mzazi wa Yassin, anasema kutokana na vitendo hivyo, mwanawe alianza kuvijaribu kwa watoto wake wengine jambo lililowa­fanya wamhamishie kwa mjomba yake ambako hakukuwa na watoto ili kuwanu­suru wenzake.

Wakati wakiendelea kufuatilia mwenen­do wa mtoto huyo, ndipo lilipoibuka kumla­witi Emmanuel.

“Sasa sijui aliombwa au ni utundu wao, wazazi wote na wa yule aliyefanyiwa hivyo tukaenda pale shuleni ndipo likaibuka suala la huyu Saddalla kwamba ndiye anawachezea watoto wa shule.

Hamis anadai kuwa baadhi ya walimu walitaka wazazi wakubaliane ili kumaliza suala hilo kuepusha aibu. “Nilichukia na kama huyo bwana angekuwa karibu tungerushiana hata ngumi,” anasema Hamis na kuongeza:

“Lakini mwalimu mkuu alikuwa upande wangu, hakutaka ile kesi iishe kwa sababu hata kama ni kijana wangu akikutwa ana matatizo kama ni kwenda kufungwa akaf­ungwe tu, nikamwambia mwalimu mkuu twende polisi.

“Kesi ikafunguliwa mtoto wangu akashi­takiwa na akahukumiwa kuchapwa viboko sikumbuki ni vingapi. Baadaye, huyo mvu­lana akasema Saddala alishamwingilia mara nyingi anampa mipira na pesa kidogo.

“Ikafunguliwa kesi kati ya huyo mtoto na Saddala ambaye alihukumiwa vizuri tu akapelekwa Butimba. Sasa hivi yule bwana yupo mtaani, sijui amefanya kitu gani aka­toka gerezani, lakini kwa jinsi tulivyopele­leza anaharibu watoto wengi.

“Hata leo (hivi karibuni), ameanza kuvizia tena watoto, kwa hiyo inaonekana ameathirika kisaikolojia hawezi kuacha na amerudi aendelee kufanya uhar­ibifu. Nilikuwa sifikirii kwamba hili tukio limetokea kwangu, nilivyoletewa sikulala nikawa najiuliza vipi haya matukio am­bayo tunayasoma kwenye Biblia hivi kweli yametokea?anahojiHamis.

Hata hivyo, Hamis anasema wakati tukio hilo linamtokea mwanawe aliamini ni kwa sababu hakumlea yeye tangu akiwa mdogo.

Ustawi wa jamii

Ofisa Ustawi wa Jamii, Sidney Mdoe, ali­yekuwa akifuatilia kesi hizo anasema wakati wa uendeshaji wa kesi kuna watu upande wa yule mtuhumiwa (Saddala) walione­kana kufuatilia ile kesi wakiamini kwamba hakutenda kosa, lakini hakimu kutokana na vielelezo na ushahidi wote uliotolewa mahakamani alitoa hukumu na kumfunga kifungo cha maisha.

Sidney anadai kuwa mtoto huyo pia ali­kuwa akiingiliwa na watoto wengine wawili ambao ni wanafunzi wa Shule ya Sekondari Misungwi akiwamo mjomba wake aliyeku­wa akilala naye. Vitendo hivyo vilimfanya Emmanuel aadhibiwe na bibi yake.

Anasema mtoto mwingine aliyekuwa akimtendea Emmanuel vitendo hivyo alikuwa akimuita aende kwao kuchukua CD za muzuki na wakati wa usiku wanaporudi ndipo humfanyia vitendo hivyo anavyodai alimfanyia zaidi ya mara tatu.

Watoto hao wote walihukumiwa kuchap­wa viboko na kisha wakaondolewa shuleni kutokana na kosa hilo kwenda kinyume cha sheria na taratibu za shule.

HUKUMU

Mei 14 mwaka huu, Saddala alihukumiwa kwenda jela maisha kwa kosa la kumlawiti Yassin mwenye umri wa miaka 13.

Uamuzi huo wa Mahakama ya Wilaya ulitolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Eric Marley, baada ya kusikiliza shauri hilo ambapo upande wa mashitaka ulikuwa na mashahidi saba.

Ushahidi uliotolewa na marafiki wa Emmanuel pamoja na Dk. Mussa Mishamo, ambaye alimfanyia uchunguzi wa kitabibu na kubaini kuwa njia ya haja kubwa ilikuwa wazi kwa mm 12, huku mishipa ya haja kubwa ikiwa imefunguka kiasi cha kidole cha kati kuingia bila shida.

Taarifa zinaeleza kuwa miongoni mwa siku ambazo mtoto alifanyiwa vitendo hivyo aliwaomba rafiki zake wamsindikize kwa mtuhumiwa kisha wao wakaondoka na kumwacha hapo, siku iliyofuata aliwaeleza kuwa alilawitiwa na kupewa Sh 700.

KAULI YA MWALIMU

Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule ya Msingi Misungwi, Hilda Magayana, anasema licha ya kujitahidi kuhakikisha ulinzi wa watoto shuleni hapo ni vigumu kumlinda mtoto anapokuwa ametoka katika mazingira ya shule.

“Lakini pia kuna muda watoto wanatoka wanakwenda kula. Ule muda huwezi kujua wakati anakwenda nyumbani anakutana na mangapi, lakini pia wanavyokuwa hapa shu­leni tunajitahidi kadri ya uwezo wetu, lakini hatuna uzio,” anasema Mwalimu Hilda.

KAULI YA DC

Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Juma Sweda, anaonesha kutofurahishwa, pia kutofautiana kwa uamuzi wa Mahakama ya Wilaya na ile ya Rufaa licha ya kukiri kuwa haki ilitendeka katika kutoa hukumu.

Hata hivyo, anasema kuwa hilo hali­wakatishi tamaa kwani wataendelea ku­pambana kukomesha vitendo hivyo, huku akisisitiza wananchi wanatambua hatua wanazozichukua.

“Hatuwezi kuingilia mahakama, lakini inarudisha nyuma jitihada za mapambano ya kulinda watoto,” anasema Sweda.

Anaongeza: “Hatuwezi kuacha kwa sababu ya kesi moja, kesi nyingi tunafanya vizuri na wananchi wametambua mchango wetu, polisi nao hawawezi kukata tamaa kwa sababu hiyo cha msingi ni kwamba tunajifunza,” anasema Sweda.

Tayari amewaelekeza waathirika wa tukio hilo ikiwa hawakuridhishwa na ua­muzi wa Mahakama ya Rufaa wawasilishe taarifa kwa mwanasheria wa wilaya ili kuangalia hatua zinazoweza kuchukuliwa ili kuhakikisha haki inatendeka.

“Kama sisi viongozi hatujaridhika na wao hawajaridhika na hatua, stahiki ziko wazi tutafanya hivyo na wanasheria tayari tumewaelekeza wafanye hivyo ili kuhakik­isha haki inatendeka, ni lazima tuwalinde watoto,” anasema Sweda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles