31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mheshimiwa Bashe nilimwambia hayo Waziri Mwijage!

BasheNI vizuri kuwa na ndoto, tena ndoto kubwa kubwa! Ndoto ni mwanzo kukusaidia kufanya tafakari, kufanya mikakati ya kuhakikisha unachokitaka, unachokiota, kinafanikiwa… ukiwa na mikakati na mikakati ambayo kweli ina tafsiri mazingira halisi ya utekelezaji wa ndoto yako.

Nchi inapaswa kuwa na ndoto. Ndoto yetu kama Tanzania ni kufikia uchumi wa kati, hata sielewi maana yake nini na sijaelimishwa tunafikiaje hapo. Nasikia kuwa uchumi unakuwa kwa asilimia saba. Nalo silielewi, maana kinachokuja sijui ni kitu gani, ongezeko la fedha kutokana na kodi kutozwa kikamilifu na kuziba mianya au kutokana na viwanda vya akina Dangote au uchimbaji wa gesi ambavyo havina uhusiano wa moja kwa moja na wananchi ila kama tunataka kuhisi tunakula pilau kwa kuweka hiliki puani…. Mimi sioni, ninachofahamu ni kuwa mfumo wa kweli wa kuinua maisha ya wananchi kuwa na shughuli za uchumi ambazo kwa kuanzia, zina manufaa ya moja kwa moja mwananchi ili awe na uhakika wa kesho na keshokutwa. Sijaona Dangote na Gesi na GGM na TBL na kadhalika vinavyotujengea uhakika wa kesho wa sisi pangu pakavu tia mchuzi na Mheshimiwa Hussein Bashe umesema nilichowahi andika kwa kaka Mwijage!

Tena niliandika katika ukurasa huu huu, gazeti hili hili! Kama miezi mitatu na ushee iliyopita. Nilikuwa naona ajabu, kama unavyoona ajabu wewe, kuhusu kufufua kiwanda fulani kule Morogoro, katika kipindi cha miezi sita. Nikaandika, nikamweleza Kaka yangu Mwijage, kuwa hili halitawezekana. Najua miezi mitatu imeshapita, sijui kama ufufuaji ule umefikia kiwango gani. Lakini aliniandikia ujumbe kusema anajua anachokifanya na kuwa lazima litekelezwe! Kaka mkubwa akisema, unanyamaza. Ninasubiri hilo. Na baadaye watendaji wake walinipigia simu kutaka kujibu nilichoandika… nikawapa utaratibu wa kuwasiliana na mhariri… sijui kilichoendelea baada ya hapo! Lakini nilichokuwa nasema ni hiki. Na cha kwanza umekitaja, mkakati sio kampeni za uchaguzi wa mwaka 2020. Nchi ilipaswa kuanza na kujenga mkakati ‘Strategic plan’ na hapo inaanza na kufanya utafiti wa kutosha juu ya kilichopo ‘Situational analysis’. Nilisema huwezi kuanza na kufufua viwanda vilivyopitwa na wakati kiteknolojia… General Tyre bilioni 60 kufufua. Hujaenda mashambani kuwatayarisha wakulima, maafisa ugani na miundombinu muhimu, ili mpira uzalishwe. Pale kwa Baba yangu, kijijini kwetu, Mwaya, Mang’ula, Kilombero, kuna shamba la Mpira… nadhani tulikwisha jigawia… sijuia watakuja kutunyang’anya, baada ya karne nyingi za kufa kwa General Tyre. Na shamba hilo hadi leo linaitwa hivyo, General Tyre. Sasa tunafufuaje kwa bilioni 60.

Tunaota ndoto ya ukweli tulioua wenyewe kwa tamaa ya gawio la asilimia kumi zilizokuwa zikitoka kwa watu waliotushauri kuua viwanda ili tukumbatie bidhaa za kutoka nje. Nakumbuka wakati, tena juzi juzi tu, Idd Simba alisema tuzuie matairi chakavu, kukilinda General Tyre. Tena wakati huo kilikuwa bado kinachechemea na kingelindwa kwa namna hiyo, lakini nani alimsikiliza… kichaa cha kuendesha biashara zetu binafsi zilizokuwa zinaua viwanda vyetu kwa kuvinyima soko la uhakika, kilitushika. Kilituchukua na nadhani hatujapona na hatutapona… ukishafufua General Tyre, hao Wachina wanaoleta matairi yao na siye akina yakhe ambao tunaagiza matairi chakavu ili tujipatie riziki, utatuweka wapi! General Tyre kitakufa tena… ni lazima tukubali kufanya uamuzi mgumu sana kama unataka kufufua viwanda… ningekuwa Mmarekani ningesema—‘Do you see what I mean! Na ningeongeza tena kwa kimombo kingine—‘you can’t have it both ways! See what I am sayin! kuwa unataka kuridhisha matakwa ya wakubwa na wafanyabiashara ya kuweka soko huria, halafu unataka kufufua viwanda ambavyo wakubwa hao na wafanyabiashara wanaviagiza na wamejaza soko! Pirelli, Yana, Yokohama, Treadstone, lukuki! Halafu wewe unataka kufufua general tyre. Fanya uamuzi mgumu, utalindaje kiwanda chako!

Unajua nilimwambiaje tena kaka yangu Mwijage, unapokuwa na teknolojia ya zamani kama ya General Tyre, unafufuaje mitambo iliyochoka na kuwa na kutu… au kiwandani hapo kuna karakana? Lakini karakana zote za utengenezaji vipuri tuliuza kwenye chuma chakavu…. Nakwambia hivi Mheshimwa Bashe, nchi huendelea kiteknolojia kwa kuwa na viwanda vya kutengeneza vipuri… machine making tools… huna hivyo hutaendelea. Nakwambia na kuna siku utanieleza.. sisi tulipoamua kuua Mang’ula, UFI, Mbeya ZZK, Kilimanjaro, Nyumbu, Tanzania Cables na kadhalika, tulikuwa tunaua msingi wa maendeleo yetu…. Hicho chuma cha Liganga au Mchuchuma unaipeleka wapi… kuuza nje? Au kutengenezea nondo za kujengea nyumba na madaraja?

Nyerere alipozungumzia chuma alikuwa akitaka kuikarisha viwanda vya msingi- Basic Industry- viwanda vya kutengenezea viwanda… sio kuchimba madini tukatengenezee consumer goods, spoku za baiskeli, visu na viti vya kukalia na mageti…. Kama tunafikiria kuwa tuchimbe chuma ili tuuze rejareja… turudi tena kule kwenye mipango—drawing board! Nitaonekana kichaa kwa hilo, lakini najua miaka 10 ya Magufuli haitakuwa na maana kama msipotaka kunielewa na sitaki kueleweka…. Lakini kwa vile Hussein Bashe, wewe ni wa CCM kama wao, pengine watakusikiliza, sisi wengine ni no name, no chama, basi tunaonekana machizi… na hasa ukizingatia kuwa bado tunahoma ya ushindi wa uchaguzi mkuu! Hatusikilizi walioshindwa na mimi nilishindwa ati, ndio maana sisikilizwi…nchi inaendelea kwa kujenga mkakati. Niliandika katika mtandao wa Facebook, niliweka mchoro ukionyesha ambavyo nchi iliyokuwa pagale, kama sio mahame, kama yetu, inapaswa kuanza- situational analysis, stragegic plan, prioritization, unafuatilia utekelezaji baada ya kuwa na resource mobilization ya kutekeleza hivyo vipaumbele!

Nampenda Magufuli kwa sababu anayo nia kutoka moyoni ya kuona nchi hii inaendelea… lakini mawaziri wake hawafikirii kimkakati kumshauri… wanaendesha kampeni… nchi inafufuliwa uchumi kwa kufikiria yafuatayo kwa mfano… Kuna viwanda vidogo vidogo vya kuongeza thamani- alizeti, juisi, asali, korosho na kadhalika. Hivi vinagusa wananchi, hivi vinahitaji mtaji mdogo na kulindwa katika soko. Kwani nani anatulazimisha lazima tuwe na maviwanda makubwa makubwa! Tuanze na hivyo… viwanda vidogo vidogo.. tuna SIDO, VETA, na wataalamu hapa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam sijui na wapi kwingine- hujataja TBS na TFDA… hawa kazi yao nini! Sioni tukiwatumia wataalamu hao kusaidia wajasiriamali waongeza thamani… tukifanya uamuzi mgumu, tukawalinda katika soko, tukawaelimisha, tukawapa mitaji, vitakuwa viwanda vikubwa na nina uhakika wananchi watamchagua Magufuli.  Ukiwa na viwanda vya Dangote 10 nchini, havitaweza kushinda kiwanda kimoja cha kuongeza thamani ya alizeti pale Nzega jimboni kwako…maana kila kaya itapata pato, sio wachache wanaoajiriwa kwenye maviwanda na kupeleka fedha kwa aliyeajiriwa tu….Serikali inapaswa kujifikirisha kimkakati na sio kuwa na maneno ya kikampeni kuwaridhisha wao wenyewe waonekane wanafanya kazi. Najua hizi zitaonekana hekaya za mlevi.. lakini miaka kumi ijayo. Mtakuja kunieleza!

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles