31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Mgombea ubunge afungwa jela miaka sita

KULWA MZEE -DAR ES SALAAM

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imemhukumu kwenda jela miaka sita aliyekuwa mgombea ubunge Jimbo la Korogwe Mjini mkoani Tanga mwaka 2015, Salma Mntambo kwa makosa 17, yakiwamo ya kutakatisha fedha.

Katika makosa matatu ya kutoa nyaraka za uongo, kila kosa amehukumiwa kwenda jela miaka mitano na makosa mengine 14 ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kila kosa amehukumiwa miaka sita jela. Adhabu zitakwenda kwa pamoja, hivyo atatumikia kifungo cha miaka sita.

Baada ya kutiwa hatiani, upande wa Jamhuri uliomba mshtakiwa apewe adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine.

Mshtakiwa aliomba apunguziwe adhabu kwa sababu ya afya yake.

Hakimu Mkazi Mfawidhi, Kelvin Mhina, alisema amepitia sababu za upande wa mashtaka na utetezi katika kesi hiyo, hivyo katika makosa matatu ya kutoa nyaraka za uongo, mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka mitano jela kwa kila kosa.

Katika makosa 14 ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, atatumikia kifungo cha miaka sita jela kwa kila kosa.

Alisema huo ndio uamuzi wa mahakama, wanayo haki ya kukata rufaa.

Kuhusu suala la fidia, alisema atatafakari na kufanya utafiti ili atoe oda ambayo ni sahihi Oktoba 2.

Hata hivyo, Hakimu Mhina aliamuru mshtakiwa huyo kutumikia adhabu hizo kwa pamoja, hivyo atakwenda jela miaka sita.

Mshtakiwa aliyekuwa akikabiliwa na mashtaka 24, ametiwa hatiani katika mashtaka 17, yakiwamo ya kutakatisha Sh 1,027,000,000 kutoka kwa Ridhuan Mringo, huku akijua fedha hizo zimetokana na zao la makosa tangulizi ya kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kuwasilisha nyaraka za uongo.

Katika kosa la kughushi, Mntambo alidaiwa kati ya Juni mosi, 2003 na Oktoba 31, 2011 maeneo yasiyojulikana wilayani Ilala, mkoani Dar es Salaam kwa nia ya udanganyifu alighushi risiti yenye namba 001226 ya tarehe 10/06/2003 ili kuonyesha Ridhuan Mringo alinunua nyumba ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) iliyopo Plot namba 710 Mtaa wa Mfaume Upanga kwa Sh milioni 70, wakati akijua ni uongo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles