27.5 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mgombea Mwakalebela aeleza atakavyoirejesha Yanga ya kimataifa

SOSTHENES NYONI-DAR ES SALAAM

MGOMBEA wa nafasi ya Makamu wa Rais wa Yanga katika uchaguzi mkuu wa klabu ya Yanga, Frederick Mwakalebela, ametaja vipaumbele vyake ikiwa atafanikiwa  kushinda kiti hicho.

Uchaguzi Mkuu wa Yanga unatarajia kufanyika Jumapili hii ambapo wanachama wa klabu hiyo watawachagua viongozi wao katika nafasi za mwenyekiti, makamu mwenyekiti na wajumbe wa kamati ya utendaji.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwakalebela ambaye pia ni Katibu Mkuu wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),alitaja vipaumbele hivyo kuwa ni mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo kongwe, kuiboresha zaidi nembo ya Yanga, kuboresha benchi la ufundi kwa kuiongezea thamani nafasi ya Kocha Mkuu kutoka kuwa kocha hadi meneja wa timu kama ilivyo klabu za Ulaya.

Alisema atahakikisha anaboresha benchi la ufundi katika maeneno mawili ambayo ni utawala linalowahusu viongozi na ufundi linalohusu soka la wanawake na vijana.

Mwakalebela aliendelea kumwaga sera kwa kuwebayana vipaumbele vingine kuwa ni kuboresha Uwanja wa Kaunda ambao kwa sasa hadhi ya kutumika, pia kumshauri mwenyekiti kuongeza wanachama zaidi kwenye matawi na suala la mapato na matumizi,  sambamba na kuboresha zaidi katiba kwa kuwatambua wachezaji na wazee wa timu hiyo.

Aidha Mwakalebela alisema mipango yake mingine ni kudhibiti uuzaji holela wa bidhaa za klabu hiyo kama jezi, kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Jeshi la Polisi na wadau wengine.

Alisema ili kudhibiti bidhaa feki za klabu hiyo watatangaza tenda kwa kampuni mbalimbali na ile itakayoshinda ndiyo itakayopewa kazi ya kuzalisha.

Uchaguzi wa Yanga umepangwa kufanyika Mei 5, mwaka huu, hivyo kila mgombea atapata fursa ya kuelezea sera zake ili kuwashawishi wanachama wampigie kura katika uchaguzi huo.

Viongozi watakaoingia madarakani watapata nafasi ya kuiongoza klabu hiyo yenye maskani yake Mtaa wa Twiga na Jangwani jijini Dar es Salaam kwa miaka minne.

Gumbo amwaga sera za nguvu

Kwa upande wake, Mgombea wa nafasi ya Ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo, Rodgers Gumbo, ameahidi kasi ya mabadiliko ndani ya klabu hiyo.

Gumbo ambaye amejitosheleza kiuchumi, alisema endapo atafanikiwa kuingia katika Kamati ya Utendaji, atahakikisha ndani ya kipindi kifupi Yanga inapata maendeleo ya haraka kwa kupitia vitega uchumi vyake mbalimbali.

“Mimi si kama wale wa kukaa ofisini na kupewa taarifa, nitahakikisha naifanyia kazi Yanga kwa moyo wangu wote, furaha yangu ni kuona siku moja tunatamba Afrika,” alisema Gumbo.

Gumbo alisema Yanga inaweza kuwa klabu tajiri kupitia Uwanja wake wa Kaunda, Majengo na wanachama lakini pia matajiri wengi wanatamani kuwekeza ndani ya klabu hiyo.

“Yanga si timu masikini isipokuwa viongozi waliopita ndio waliotufikisha hapa, wawekezaji walishindwa kuwekeza kutokana na aina ya viongozi tuliokuwa nao,” alisisitiza Gumbo.

Wagombea waliopitishwa katika zoezi la usaili ni pamoja na Baraka Igangula, Dk. Jonas Tiboroha, Elias Mwanjala na Dk. Mshindo Msola katika nafasi ya mwenyekiti.

Kwa upande wa makamu mwenyekiti, wagombea ni Fredrick Mwakalebela, Janeth Mbene, Titus Osoro na Yono Kevela.

Wajumbe ni Said Mohamed Khimji, Hassan Yahya, Arafat Hajji, Suma Mwaitenda, Hamad Isalm, Shafiru Amour Makosa, Bahati Mwaseba, Leonard Mwarango, Haruna Batenga, Athanas Kazige, Ramadhani Said na Salim Rupia.

Wengine ni Dominick Francis, Sharif Amir, Benjamini Mwakasonda, Christopher Kashiririka, Ally Msigwa, Frank Kamugisha, Said Kambi na Silvester Haule.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles