26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

MGOGORO WA ARDHI: UKATILI WA KUTISHA, MKULIMA ACHOMWA MKUKI MDOMONI

Mkazi wa Kijiji cha Dodoma- Isanga, Agustino Mtuti akiwa na kipande cha mpini wa mkuki aliochomwa mdomoni na wafugaji wilayani Kilosa mkoani Morogoro juzi. Picha ndogo kulia ikionyesha sehemu ulipotokea, baada ya kufanyiwa operesheni.
Mkazi wa Kijiji cha Dodoma Isanga, Agustino Mtuti akiwa na kipande cha mpini wa mkuki aliochomwa mdomoni na wafugaji wilayani Kilosa mkoani Morogoro juzi. Picha ndogo kulia ikionyesha sehemu ulipotokea, baada ya kufanyiwa operesheni.

Na Ramadhan Libenanga-Morogoro.

NI ukatili wa kutisha. Ndivyo unavyoweza kusema kutokana na mtu mmoja kunusurika kifo, baada  ya  kuchomwa mkuki mdomoni na kutokea nyuma ya  shingo.

Mbali na ukatili huo, watu wengine wanane wamejeruhiwa vibaya na  kulazwa  Hospitali  ya Wilaya  ya Kilosa mkoani Morogoro kutokana na mapigano  ya  wakulima  na  wafugaji yaliyotokea Kijiji cha Dodoma  Isanga juzi.

Mapigano hayo yamekuja siku mbili baada ya Askofu Mkuu  wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Fredrick Shoo,  kuonya juu ya Taifa kunyemelewa na hatari ya kuingia katika machafuko, kutokana na dalili mbaya zilizoanza kujitokeza.

Alisema hali hiyo inachangiwa na uwepo wa migogoro mingi ya ardhi inayosababishwa na Serikali kugawa maeneo makubwa na kuwamilikisha wawekezaji wa nje kama njugu.

Akizungumza  na MTANZANIA jana, mkulima wa kijiji hicho, Stanley George  alimtaja mtu aliyekumbwa na mkasa huo kwa jina la Agustino Mtuti.

Alisema  tukio hilo lilitokea  juzi  saa tano  asubuhi, baada ya kuibuka mapigano makali.

Stanley, alisema  akiwa  katika  shughuli zake  za uchomaji  mkaa, alisikia  kelele zikipigwa na watu ambao wanaomba msaada, baada ya wananchi kulalamikia kitendo cha  wafugaji  kuingiza  mifugo  katika  mashamba  yao ya mahindi .

Alisema  baada  ya hali  hiyo, Mtitu alifika eneo la tukio na kuhoji sababu za wafugaji  kuingiza mifugo kwenye mashamba  ya wakulima.

“Baada  ya  kuhoji, mmoja wa  wafugaji hao alitoka  mbele  yake na kumchoma  mkuki mdomoni ambao ulitokea upande  wa  pili  wa  shingo,”alisema  Stanley.

Alisema baada  ya   wafugaji  kufanya  tukio  hilo na  kubaini wanakijiji  wamegundua,  walikimbia  na kuacha ng’ombe wao shambani  ambao walichukuliwa  na wananchi.

Alisema  baada  ya muda mfupi, wafugaji  walirudi  kwa lengo  la  kutaka kuwachukua  ng’ombe  wao ndipo mapigano makali yakazuka, huku wakulima wakijeruhiwa vibaya.

DIWANI

 Diwani wa Kata  ya Masanze, Bakari Killo (CCM),   akizungumzia  tukio  hilo, alisema wafugaji  walirudi  mara  ya  pili  na  kufanya  shambulio kubwa  kwa lengo  la  kutaka  kuteka  mifugo yao.

Alisema katika harakati hizo Mwenyekiti wa  Kijiji cha  Dodoma, Stephano Daud, Mwenyekiti wa Kitongoji, George  Andrea  na mkazi wa eneo hilo, Saimo  Luhoga walijeruhiwa vibaya.

Alisema baada  ya kuona machafuko yametulia walifanya jitihada  za  kuwafikisha  majeruhiwa wote Hospitali  ya   Wilaya  ya Kilosa.

Kwa  upande  wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Frank  Jakob  alisema majeruhi Mtitu alipokewa juzi saa 10 jioni na kupelekwa moja kwa moja chumba cha upasuaji  ambako walifanikiwa kumtoa mkuki huo .

“Kutokana na   timu  ya madaktari  wangu  kufanya  kazi  nzuri dakika 80, hivi sasa wanaendelea kushona ulimi, kurudishia fizi na meno…kiujumla hali yake inaendelea vizuri,”alisema  Dk. Jakob.

 MBUNGE

Mbunge  wa Mikumi, Joseph  Haule (Chadema),  amelaani    vikali  tukio hilo na kuiomba  Serikali  kufanya  kazi  ya ziada ili  kupugunguza  mapigano hayo.

Alisema lazima iweke  miundombinu  sahihi  kwa  kila  kundi  ili  kuepuka  mwingiliano na hata mapigano yanayoweza kuzuilika kati ya wakulima na wafugaji.

Akizungumzia tukio hilo Kamanda  wa  Polisi Mkoa  wa Morogoro, Ulurich Matei  alisema hadi jana jeshi hilo limewatia mbaroni wafugaji watatu, huku likiendelea na msako wa kumtambua  mmliki wa mifugo iliyosababisha mapigano hayo.

Juzi Askofu Mkuu  wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Fredrick Shoo, alisema Taifa linakabiliwa na hatari ya kuingia katika machafuko, kutokana na dalili mbaya zilizoanza kujitokeza.

Alisema hali hiyo inachangiwa na uwepo wa migogoro mingi ya ardhi inayosababishwa na Serikali kugawa maeneo makubwa na kuwamilikisha wawekezaji wa nje kama njugu.

Mbali na hilo amesema pia Taifa limegubikwa na tatizo kubwa la rushwa inayosababisha baadhi ya wananchi kuonewa, kudhulumiwa na kukosa haki zao huku wengine wakilazimika kutumikia vifungo magerezani jambo ambalo ni hatari.

Askofu Dk. Shoo aliyasema hayo wakati akitoa salamu za Sikukuu ya Krismasi katika ibada maalumu iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kaskazini , Usharika wa Moshi Mjini, mkoani Kilimanjaro.

Alisema katika kipindi hiki ni vema Serikali ikawa makini na kujitahadharisha na tabia ya kuwamilikisha wawekezaji wa kigeni  maeneo makubwa kwani suala hilo limekuwa likisababisha migogoro mikubwa na wananchi jambo ambalo alidai ni dalili kubwa ya kutokea machafuko nchini ikiwa ni pamoja na kuwagawa Watanzania.

“Tuwe makini katika umilikishaji wa maeneo makubwa ya ardhi kwa wawekezaji wa mataifa mengine jambo hili likiendelea hivi katika siku za usoni litatuondolea amani yetu kabisa.

“Ardhi ni kitu muhimu sana tusigawe kama Karanga, nchi yetu imekuwa na ukarimu wa kumilikisha wageni ardhi  ni tofauti sana na nchi nyingine na iwapo halitaangaliwa upya amani yetu tumeiweka rehani,” alisema askofu Dk. Shoo.

Kutokana na kukithiri kwa migogoro ya ardhi katika Mkoa wa Morogoro, iliilazimu Serikali kupitia Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, kuunda kamati maalumu ya wataalamu ili kuweza kufanya uchunguzi wa suala hilo.

Timu hiyo  ilikuwa ikiongozwa na na Dk. Steven Nindi, Mkurugenzi Mkuu mpya wa tume hiyo ambapo itashughulika na kuhakiki mipaka ya vijiji sita ambavyo vina migogoro ya mara kwa mara ya wakulima na wafugaji na kusababisha maafa wilayani humo.

Vijiji vilivyozungukiwa na timu hiyo ni Bonde la Mpunga la Mgongola ambavyo ni Hembeti, Dihombo, Mkindo Sindoni, Mkindo kwa Boma, Kambala na Kikundi.

Hata mapigano ya kila wakati yamekuwa yakiripotiwa na kubabisha mauaji na mifugo baina ya wakulima na wafugaji kila wakati.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles