27 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

MGODI TANZANITE ONE HOI

Na Masyaga Matinyi – Manyara


MGODI wa madini ya Tanzanite unaomilikiwa kwa ubia kati ya Kampuni ya Sky Associates na Serikali kupitia Shirika la Madini la Taifa (Stamico) umesimamisha shughuli za uchimbaji madini, huku miundombinu iliyopo chini ya ardhi ikiendelea kuharibika na kuikosesha mapato Serikali.

Mbali ya kuwapo hali hiyo, mamia ya wafanyakazi wa mgodi huo maarufu kama Tanzanite One uliokuwa wa kisasa, hawajalipwa mishahara kwa takribani miezi 11 sasa.

Awali, mgodi huo ulikuwa ukimilikiwa na Kampuni ya Tanzanite One kupitia kampuni mama, Richland Resources Limited ya Afrika Kusini ambayo mwishoni mwa mwaka 2014 iliuza hisa zake kwa Sky Associates.

Wakurugenzi wa Sky Associates ni Faizal Shaibhal, Hussein Gonga na Ridhiwan Ullah ambao tangu wanunue hisa za mgodi huo, hawajawahi kufanya uwekezaji wowote ili kuuboresha.

Hata Stamico ambayo ni mwakilishi wa Serikali katika ubia wa asilimia 50 kwa 50, nayo haijawahi kuwekeza mtaji wowote.

ZIARA YA WAZIRI KAIRUKI MIRERANI

Akiwa katika awamu ya kwanza ya ziara ya kikazi katika eneo hilo siku chache zilizopita, Waziri wa Madini, Angela Kairuki, alifanya mkutano wa hadhara mbele ya geti la ukuta wa Mirerani.

Mkutano huo mkubwa ulihudhuriwa na wachimbaji (wana-Apolo), wamiliki wa migodi, wakiwamo wakurugenzi wa Sky Associates, viongozi wa Serikali, vyama vya siasa, wabunge, wafanyabiashara wakubwa na wadogo wa madini ya vito pamoja na wananchi.

Katika mkutano huo, baadhi ya wananchi walipata fursa ya kuzungumza na kero kadha wa kadha ziliwekwa bayana na Kairuki alizitolea majibu.

Lakini tukio lililovuta hisia za wengi, ni pale mama aliyejitambulisha kwa jina la Rehema Mbando ambaye ni mjamzito, alipodai kuwa anateseka kwa kutolipwa mshahara kwa zaidi ya miezi 10.

“Waziri wewe ni mama kama sisi, wenzako tunateseka, wakurugenzi wetu hawataki kutulipa mishahara, mimi ni mjamzito wa miezi minane, nateseka, kila ukiwapigia simu wanakuzungusha, tumechoka mama, tusaidie,” alisema mama huyo huku akilia.

Baada ya kumaliza kuzungumza, wakurugenzi wawili wa Sky Associates waliokuwapo mkutanoni; Faizal na Gonga, waliitwa mbele ya hadhara na Kairuki, huku wakizomewa na kutakiwa kutoa majibu yenye uhakika kuhusu suala la mshahara kwa wafanyakazi wao.

Akijibu hoja kuhusu mishahara, Faizal alikiri kutowalipa wafanyakazi wao kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo migogoro ya kiutendaji na kibiashara na aliahidi kulishughulikia suala hilo ndani ya miezi miwili hadi mitatu.

“Ni kweli hatujalipa mishahara, na suala la huyu mama tunalifahamu, naomba tuondoke naye, kesho hadi saa tano asubuhi tutampa mshahara wake wote anaodai.

“Ila kwa wafanyakazi wengine, tunaomba muda wa miezi miwili hadi mitatu, tutawalipa mishahara ya miezi miwili, baada ya hapo tutaendelea kuwalipa malimbikizo taratibu,” alisema.

Alipoulizwa kwa mwezi mmoja wanapaswa kulipa kiasi gani cha fedha, Faizal alisema gharama za mishahara kwa mwezi ni karibu Sh bilioni moja au Dola za Marekani zaidi ya 400,000.

Kutokana na maelezo hayo, Kairuki, aliwataka kueleza ni lini shughuli za uchimbaji zitaanza na Faizal alisema wao kama wakurugenzi, kila mmoja atatoa kiasi cha fedha watakachokubaliana na walitarajia uzalishaji kuanza jana, jambo ambalo halikufanyika, huku mgodi huo ukiwa umesimama kufanya kazi tangu mwishoni mwa mwaka jana.

Baada ya maelezo hayo, Kairuki aliwataka kuhakikisha wanatekeleza kila kitu kama walivyoahidi na aliwahakikishia wananchi waliohudhuria mkutano huo kuwa atarudi Mirerani kufuatilia utekelezaji wa maagizo yake.

WAKURUGENZI WANUSURIKA KUPIGWA

Katika hali isiyo ya kawaida, baada ya mkutano kumalizika saa 12 jioni, wakurugenzi Faizal na Gonga wakiwa wameongozana huku watu wakiwazonga, walitoa burungutu la fedha na kumpa mtu mmoja ili agawe.

Baada ya kitendo hicho, mtu aliyepewa fedha alivamiwa na watu na kutokea patashika kubwa, huku kundi jingine la watu likiwavamia wakurugenzi hao na kudai fedha.

Kwa takribani dakika 10 hali ilikuwa mbaya na ilibidi baadhi ya wasamaria wema kuingilia kati kuwaokoa wakurugenzi hao, ambao baada ya kupata mwanya, waliingia ndani ya gari na kukimbia kusalimisha maisha yao.

GONGA AZUNGUMZIA  HALI YA MGODI

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili ofisini kwake, Gonga, alikiri hali ya mgodi kuwa mbaya na zinahitajika fedha nyingine kuurudisha katika hali ya kawaida.

“Kaka pale zinahitajika dola karibu milioni tano ili kurekebisha mambo na kazi ianze, wakati tumesimamisha uzalishaji tukiwa katika mazungumzo na Serikali, kulifanyika hujuma kadha wa kadha.

“Baadhi ya watu waliingia katika eneo letu kinyume cha sheria na kupiga baruti, hivyo wameharibu hadi nguzo na kuna kazi kubwa ya kuvuta maji yaliyojaa mgodini,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles