31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Mgambo waonywa kupiga wananchi

FRANCIS GODWIN -IRINGA

MKUU wa Wilaya ya Kilolo, Asia Abdallah, amepiga marufuku mgambo kutumia nguvu kupiga hadi kuumiza watuhumiwa wa makosa mbalimbali wanapowakamata.

Badala yake, amewataka kutumia akili zaidi badala ya mabavu yasiyohitajika katika ukamataji watuhumiwa.

Alisema mgambo kupewa jukumu la ulinzi na usalama wa wananchi, si kibali cha kuwanyanyasa au kuwapiga virungu na kuwajeruhi wakati wa kuwakamata.

Akizungumza katika Kijiji cha Ilawa jana, wakati wa kufungua mafunzo ya mgambo wa Kata ya Image, Asia alisema umezuka mtindo wa mgambo kugeuka miungu watu na kunyanyasa wananchi.

“Mimi tangu niwe mkuu wa wilaya hii, nina vyombo mbalimbali vya ulinzi, sijawahi kuagiza kupiga wananchi, nataka ninyi tumieni medani ya mafunzo mliyopewa katika kukamata watuhumiwa,” alisema.

Asia alisema siku zote nguvu hutumika pale mtuhumiwa anapotumia nguvu zaidi ambayo inaweza kuhatarisha usalama.

Alisema hatasita kuchukua hatua kwa mgambo yeyote atakayebainika ama kulalamikiwa na wananchi.

“Nikikukuta umetumia vibaya nafasi yako kwa kumpiga mwananchi au umetumia nguvu eneo ambalo nguvu haikuhitajika, nitakushughulikia,” alisema Asia.

Katika hatua nyingine, aliwaagiza mgambo kuendelea kuwa walinzi wa usalama katika vijiji vyao na kuchukua hatua ya kudhibiti majanga ya moto pindi yanapojitokeza.

Alisema kupitia mafunzo hayo, vijana wanaweza kujiajiri kwa kuanzisha vikundi vya ulinzi na vya kiuchumi.

Katika mafunzo hayo vijana zaidi ya 150 walihitimu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles