33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mfumo TANCIS kutumika  Zanzibar kuimarisha ukusanyaji mapato

Na KOKU DAVID-DAR ES SALAA



MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) inatarajia kuanza kutumia Mfumo wa Kuingiza na Kuondosha Mizigo kwa njia ya Kielektroniki (TANCIS) visiwani Zanzibar mapema mwaka 2019.

Mfumo huo wa TANCIS ni kichocheo muhimu katika kuipa mamlaka teknolojia ambayo itaiwezesha kuendana na matakwa ya ukuaji wa biashara ya kimataifa.

Lengo la matumizi ya mfumo huo ndani ya TRA ni ili kuwezesha mamlaka hiyo kukusanya mapato hadi kuvuka lengo, kurahisisha shughuliza forodha ikiwa ni pamoja na kuongeza tija.

Kutokana na hali hiyo, hivi karibuni wajumbe wa Kamati ya Fedha, Biashara na Kilimo ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar walitembelea ofisi za TRA ili kujifunza namna mfumo huo wa TANCIS unavyofanya kazi katika vituo vya forodha.

Naibu Kamishna Mkuu wa TRA, Adolf Ndunguru ambaye aliwakaribisha Wajumbe wa Kamati ya Fedha, Biashara na Kilimo ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar anasema kuwa kujifunza kile ambacho mtu anakifanyia kazi ni wajibu ili kuweza kuongeza ufanisi katika kazi.

Anasema wajumbe hao kutoka Zanzibar walitembelea ofisi za TRA ili kujifunza namna ambavyo mfumo wa TANCIS unavyofanya kazi katika vituo vya forodha.

Anasema kuwa mfumo wa TANCIS unaisaidia mamlaka kurahisisha shughuli za forodha, unaongeza tija ikiwa ni pamoja na kuongeza mapato ya serikali.

Anaongeza kuwa ni kichocheo muhimu katika kuipa TRA teknolojia ambayo inaendana na matakwa ya ukuaji wa biashara ya kimataifa.

Ndunguru anasema TRA ina wajibu wa kusimamia kodi zote za muungano na zile za Tanzania bara na kwamba mapema mwakani 2019 wanatarajia mfumo huo wa TANCIS utaanza kutumika Zanzibar hasa katika bandari na uwanja wa ndege.

Naye Meneja wa Mfumo huo wa TANCIS, Tinkasimile Felix anasema kuwa mfumo huo unahusisha sehemu kuu za utendaji zinazohusisha ufuatiliaji, ukaguzi na usambazaji wa kielektroniki wa orodha ya mizigo, usimamizi wa mizigo iliyoondoshwa na taarifa zake, usimamizi wa usafirishaji mizigo au kontena kutoka sehemu au ushushaji kwenda sehemu ya uhifadhi.

Anasema, mfumo huo pia unasimamia dhamana  na usafirishaji wa bidhaa zilizo katika dhamana na kutoa tamko kabla ya kuwasili kwa mzigo na namna ya kulipia pamoja na usimamizi wa viashiria vya hatari kwa mzigo kuendana na mazingira.

Anaongeza kuwa TRA imekuwa ikiwahusisha wadau wa mfumo huo katika kila hatua ikiwa ni pamoja na kuandaa mafunzo mbalimbali ili kuhakikisha kuwa kila mdau anakuwa na uelewa kuhusiana na mfumo wa TANCIS kwa ajili ya kuutumia.

Felix anasema mfumo wa TANCIS unawezesha usimamizi wa mizigo tangu inapoingia hadi inapoondoshwa katika muda muafaka.

Anasema pia unatoa ripoti kamili ya utendaji na kutunza takwimu na hivyo kurahisisha shughuli za forodha na kuongeza mapato ya serikali ambayo hutumika katika kutekeleza mambo mbalimbali ya maendeleo.

Mwenyekiti wa kamati aliyeongoza msafara huo, Dk Mwinyihaji Makame anasema kuwa mafunzo hayana mipaka pia ni wajibu wao kujifunza kile wanachokifanyia kazi na kwamba mafunzo waliyopata anaamini yatawasaidia katika kuboresha utendaji kazi na kusaidia kuongeza mapato ya serikali.

Anasema TRA inafanya kazi kubwa na kwamba imefanikiwa kuongeza wigo wa walipakodi, kusambaza elimu ya kodi ikiwa ni pamoja na kuinua mapato ya serikali ambayo yananufaisha sehemu zote mbili za muungano.

Anasema wananchi wanatakiwa kuungana na serikali kwa kuwa na uzalendo wa kulipa kodi kwa hiyari kama sheria inavyoelekeza ili kuiwezesha serikali kutekeleza majukumu yake ya kufanya maendeleo kwa wananchi wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles