26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

MFUMO RAFIKI UTAONDOA UDHALILISHAJI WATOTO

Na Willbroad Mathias


MFUMO  rafiki  wa  sheria  za  makosa ya jinai ni kati ya haki za watoto ulioainishwa katika vifungu vya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mfumo  rafiki ni maboresho yaliyofanyika katika miaka ya karibuni  kwa kufuta Sheria  ya zamani ya  Watoto  na Vijana  ya  mwaka1937  na  kutungwa kwa  Sheria  ya  Mtoto  ya  mwaka 2009 ambayo pamoja na mambo mengine ilianzisha Mahakama ya Watoto.

Kuanzishwa kwa mfumo huu  rafiki  wa  sheria  za  kijinai  kwa  watoto  ni  kipimo  sahihi  cha  namna  Serikali  inavyoweza kutekeleza  matakwa  mbalimbali  ya  mikataba  ya  kimataifa na  sheria  na  sera  za  watoto.

Mbali na lengo hilo mfumo huu ulikuwa na lengo  la kuondoa  ukatili  kwa  watoto na  kujenga  mfumo  mbadala  ambapo  haki  zao zitazingatiwa na pia  watalindwa dhidi ya ukatili wakati wote.

Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) kinasema  pamoja na kuwapo na nia njema ya  Serikali kupambana na hali hiyo, bado kuna upungufu.

TAWLA inasema licha ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania kutoa haki  za  kijumla  kuhusiana  na  masuala ya makosa  ya  jinai  kama  haki  ya  kutokuonekana  mhalifu  mpaka  uhukumiwe, haki ya dhamana, haki ya kupata msaada stahiki wa kisheria na haki ya kusikilizwa na kutoa maoni, bado kuna pengo linalohitaji kujazwa hasa kuhusiana na haki za watoto wenye kukinzana na sheria.

Inasema katika eneo hilo, yapo  masuala  maalumu  kuhusiana  na  watoto  wanaoingia  katika kukinzana  na sheria  ambayo si  rahisi  kuyashughulikia katika  mfumo  wa  jinai  uliopo  katika Katiba ya  sasa ambao unatazama na kushughulikia zaidi haki za watu wazima.

Wataalamu hao wanasema, baadhi ya masuala hayo maalumu ni  pamoja  na  kutazama  masilahi  mapana  ya  watoto  na  ulinzi  wao, hivyo  Katiba kama sheria  mama  ni  lazima  itambue  vigezo  hivi  muhimu  wakati  wa  kutunga  ibara  zinazomgusa mtoto.

TAWLA inasema kwa kufanya hivyo, Tanzania itakuwa inaingiza katika Katiba kanuni muhimu zinazohusu watoto kama zinavyotambuliwa na mikataba ya kimataifa kuhusu watoto.

“Vilevile  ni  vizuri  kufahamu  kuwa  madhumuni  ya  kuwa na mfumo  rafiki  wa  jinai  kwa  watoto  ni kuwarekebisha  watoto  waliohukumiwa  kwa  jinai  na  kuwafanya  wawe  raia  wema. Hivyo  kuna  tofauti  kubwa  sana  na  mfumo  wa  kawaida  wa  jinai  unaolenga  kumfanya  mtu  atubu, asifanye  uhalifu tena na usiolenga katika kumrekebisha mtuhumiwa na kumbadili awe raia bora,” inasema moja ya taarifa za utafiti wake wa hivi karibuni.

Chama hicho cha wanasheria kinasema, ni  vizuri  pia  kutambua  kuwa  vipo  viwango  vya  kimataifa  kuhusu  mfumo  rafiki  wa  jinai  kwa watoto  unaotokana  na  mikataba  mbalimbali.

TAWLA inasema, viwango  hivi  vinaelekea  sasa  kuwa sheria za asili za kimataifa na  kwa kutambua hili nchi nyingi duniani zimeanza kuvizingatia   kama viwango ambavyo ni lazima nchi na taasisi mbalimbali katika nchi hiyo ivifikie wakati wa kutunga sheria na taratibu za kuongoza mfumo rafiki wa jinai kwa watoto.

“Tunatambua pia maboresho yaliyofanyika katika siku za karibuni kwa kufuta Sheria  ya zamani ya  Watoto  na Vijana  ya  mwaka1937    na  kutunga  Sheria  ya  Mtoto  ya  mwaka 2009 ambayo pamoja na mambo mengine ilianzisha Mahakama ya Watoto. Hata hivyo, sheria hii mpya tayari imeonyesha kuwa na mapungufu yanayohitaji kufanyiwa kazi,” inasema ripoti hiyo.

Wanasheria hao wanasema, katika utafiti uliofanyika mwaka 2011 imeonekana kuwa hakuna mfumo maalum wa kuwalinda  Watoto na ukatili na kudhalilishwa ikiwa ni pamoja na ukosefu wa huduma tofauti kwa wahalifu wengine.

Wanasema hali   hii   inahitaji   matamko   na   nguvu   za   ziada   kuhakikisha   uwepo   wa   mfumo utakaohakikisha  haki  za  watoto  zinalindwa  na  kuzingatiwa  na  wakati  huo bora.

TAWLA wanasema upungufu huo pia ndio umekuwa ukichangia pia kukosekana hata mazingira hayo rafiki katika Mahakama  ya  Watoto.

Wanasema pamoja na sheria za uanzishwaji wa mahakama hizo kueleza kuwa mambo mengi ikiwamo na mashauri ya watoto kusikilizwa kwenye majengo tofauti na zinaposikilizwa kesi za watu wazima, lakini katika tafiti zao mbalimbali wamekuwa wakikuta hali tofauti  na maelekezo ya sheria hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles