33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Meneja Barclays adaiwa kuwasiliana na majambazi kupanga wizi

Benki ya Barclays
Benki ya Barclays

NA KULWA MZEE, DAR ES SALAAM

MENEJA wa Benki ya Barclays Tawi la Kinondoni, Alune Kasilika, amedaiwa kuwa aliwasiliana na watuhumiwa wa tukio la ujambazi katika benki hiyo wakiandaa utekelezaji wake.

Hayo yalidaiwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na Wakili wa Serikali, Janeth Kitali, mbele ya Hakimu Mkazi Nyigulile Mwaseba, wakati akiwasomea washtakiwa maelezo ya awali.

Kitali alidai siku ya tukio Aprili 14, mwaka huu, mshtakiwa Alune na Neema Batchu ambao ni wafanyakazi wa benki hiyo, walifika kazini na shughuli za kibenki ziliendelea pamoja na wafanyakazi wengine.

“Mheshimiwa hakimu, mshtakiwa wa kwanza ambaye ni meneja wa benki hiyo, Alune, siku ya tukio alikuwa na mawasiliano na mshtakiwa wa tatu hadi wa kumi ili kuandaa tukio la wizi wa fedha za benki hiyo na hatimaye lilifanyika,” alidai.

Alidai kuwa wizi ulifanikiwa baada ya washitakiwa hao ambao ni wafanyakazi wa benki hiyo kutoa taarifa za kina kuhusu benki kwa mshtakiwa wa tatu hadi wa kumi.

Aidha, alidai kuwa Sajini Iddi na Bundala wakati upelelezi wa kina ukifanyika huku wakijua mshtakiwa wa kwanza hadi wa kumi wanatafutwa kwa wizi, waliwapa taarifa za kiupelelezi ili kuwasaidia wajifiche wasikamatwe na walikimbia kukwepa mkono wa sheria.

Baada ya kumaliza kuwasomea maelezo hayo, washtakiwa walitakiwa kujibu wanayokubali na wanayokataa.

Hata hivyo, washtakiwa wote walikubali majina yao na walikana maelezo yote yanayohusu wizi huo.

Hakimu Mwaseba aliahirisha kesi na kupanga kuanza kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka Septemba 17, mwaka huu.

Kitali aliwakumbusha washtakiwa mashtaka yao ambapo alidai mshtakiwa wa kwanza hadi wa tisa, wanashtakiwa kwa kula njama kutenda kosa la wizi wa fedha za Benki ya Barclays.

Inadaiwa Aprili 15, mwaka huu kwa unyang’anyi wa kutumia silaha, washtakiwa waliiba Sh 390,220,000, Dola za Marekani 55,000 na Euro 2,150 mali ya benki hiyo na kabla ya kufanikisha wizi huo, walimtishia kwa bastola Anifa Ahmed na Anna Tegete.

Washtakiwa walikana kutenda makosa hayo.

Katika shtaka la mwisho, Wakili wa Serikali alidai linawahusu maofisa wa polisi, Sajini Iddi na Bundara.

Maofisa hao wanadaiwa kuwasaidia washtakiwa kutoroka ili wasikamatwe na kufikishwa mbele ya mkono wa sheria. Hata hivyo, walikana pia.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni mameneja wawili wa benki hiyo, Alune Kasilika (28), Neema Batchu (26), mfanyabiashara Hamis Shabani au Carlos (34), mkazi wa Magomeni na dereva Manase Genyeka au Mjeshi (35), mkazi wa Tabata.

Wengine ni wafanyabiashara Kakamie Julius (32), Iddy Khamis  (32), Sezary Massawe (31), Boniphace Muumba (29), Ruth Macha (30) na maofisa wawili wa polisi, Sajini Iddy (33) na Bundala (37).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles